Nikiwa kama mtanzania halisi na mdau mkubwa wa michezo nchini hasa soka niliamua kujitosa katika kugombea uongozi ndani ya shirikisho la soka nchini katika uchaguzi wa shirikisho hilo ambao umepangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi ujao.
Kwa sifa nilizonazo na mapenzi yangu niliamua kuomba kugombea katika nafasi ya kuingia kwenye kamati ya utendaji nikiuwakilisha mkoa wa Dar Es Salaam. Kwenye mchakato wa awali uliofutwa nilichukua fomu na kuzirudisha kama ilivyokuwa kwa wajumbe wengine lakini kwa bahati mbaya jina langu likakatwa kutokana na sababu za kukosa uadilifu kwa kile kilichoelezwa ya kwamba mara baada ya mchakato wa uchaguzi wa DRAF ambao pia nilishiriki kuwania nafasi ya kuuwakilisha mkoa wa Dar Es Salaam kwenye mkutano mkuu wa TFF na nikafanikiwa kupata kura 2,Nilizungumza hovyo juu ya namna uchaguzi ulivyofanyika kwenye vipindi vya michezo vya Clouds Media (Sports Xtra na Sports Bar ) . Nilikata rufaa na nikashinda lakini kutokana na matatizo mengine uchaguzi ukafutwa na FIFA na mchakato ukaamuriwa uanze upya.
Mara ya pili nilichukua fomu na kuzirudisha tena, nikiwa nasubiria majibu ya fomu yangu nikawa nasikia taarifa kwamba jina langu lazima likatwe kutokana na sababu eti nili-publish barua ya FIFA kwenye mtandao wangu (www.shaffihdauda.com ). Sikuziamini taarifa hizo na nikazipuuzia lakini baada ya siku kadhaa TFF ikaitisha mkutano na waandishi wa habari wakatoa matokeo ya baada ya usaili uliofanywa na kamati ya uchaguzi,kwa upande wangu kupitia vyombo vya habari ikatangazwa ya kwamba jina langu kweli limepekwa kwenye kamati ya maadili kwa madai ya kukosa maadili kwa kuianika barua ya FIFA, nikajitetea na nikashinda na jina langu likarudishwa kwenye mchakato wa uchaguzi.
Lakini hivi sasa kutokana na vyanzo vyangu vya taarifa ndani ya TFF kwamba nimeandaliwa zengwe lingine la kuondoa jina langu kwenye uchaguzi huo kwa madai ya kukosa uzoefu. Hii ni sababu isiyo na mashiko kwa kuwa mimi nina uzoefu mzuri unaonipa sifa za kugombea nafasi ninayoomba.
Na hata kama sababu ingekuwa hiyo kwanini wasingesema tangu mwanzo walipokata jina langu mara mbili na nikawashinda. Hizi ni hila za baadhi ya watu wasiotaka kuona Shaffih Dauda anaingia TFF kwa sababu binafsi zisizo na faida kwa soka la Tanzania.
Ninachotaka kuwaambia vikwazo vyao na mizengwe wanayoniwekea haitoweza kunikatisha tamaa katika harakati zangu za kutetea maslahi ya soka Tanzania. Kazi imejihidhirisha siku zote katika kupambana na maovu yote yanayorudisha maendeleo ya soka nyuma. Sasa ninachowaambia kwamba msijaribu kufanya mnachotaka la sivyo kwa mara nyingine tena mtanipa pointi 3 za mezani kwani nina uhakika UZOEFU NINAO NA NDIO MAANA KWENYE MICHAKATO YOTE YA AWALI KUANZIA DRFA MPAKA TFF SIKUWAHI KUONDOLEWA KWA KIGEZO HICHO ( USHAHIDI UPO IKILAZIMIKA KUUWEKA NITAUWEKA ILI WATANZANIA WOTE WAUFAHAMU ). SIKU NJEMA
0 maoni:
Post a Comment