Thursday, July 17, 2014




Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Julai 18, 2014, saa 2:41 asubuhi
WAGONGA nyundo wa Mbeya, Mbeya City fc wapo katika mkakati mzito wa kurejea na nguvu mpya kwenye michuano ya ligi kuu, msimu wa 2014/2015 unaotarajia kuanza kushika kasi septemba 20 mwaka huu.
Klabu hiyo inayonolewa na kocha maarufu nchini na kocha bora wa msimu uliopita, Juma Mwambusi ina nia ya kutwaa ubingwa msimu ujao baada ya kumaliza nafasi ya tatu katika msimu wake wa kwanza.
Ikiwa ni sehemu ya kujiweka sawa, Mbeya City fc itacheza mechi za kirafiki za kimataifa nchini Malawi na Zambia .
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Mussa  Mapunda alisema wanatarajia kucheza angalau mechi mbili za kirafiki za kimataifa nchini Zambia kabla ya kwenda Malawi kwa maandalizi zaidi.
“Malengo yetu ni kutwaa ubingwa msimu ujao. Nina uhakika tutaweza kufanikiwa”. Alisema Mapunda.
Mapunda alisema maamuzi ya kuweka kambi nchi jirani  yamechagizwa na kitendo cha shirikisho la soka Tanzania kusogeza ligi mbele mpaka septemba 20 mwaka huu.
Kocha wa Mbeya City fc, Juma Mwambusi (kushoto)
Kwa upande wake, kocha Juma Mwambusi alisema amepanga programu nzuri ya mazoezi kwa vijana wake, na anaamini watafanya kazi nzuri msimu ujao.
Mwambusi alisema kikosi chake hakijabadilika sana kwasababu karibu wachezaji wote wamebaki, achilia mbali wachache walioongezwa akiwemo Them Ferlix `Mnyama` kutoka klabu ya Kagera Sugar.
“Malengo yetu ni kufanya vizuri zaidi ya msimu uliopita. Tunajiandaa vizuri ili kukabiliana na changamoto iliyopo mbele yetu”. Alisema Mwambusi.
Msimu uliopita, Mbeya City ilimaliza katika nafasi ya tatu kwa kujikusanyia pointi 49. Walifungwa michezo mitatu tu.

Walifungwa bao 1-0 na Yanga katika dimba la Taifa, wakafungwa 2-0 na Coastal Union, Mkwakwani Tanga na mechi ya mwisho kufungwa ni dhidi ya mabingwa Azam fc ambapo walilala mabao 2-1 katika uwanja wao wa nyumbani wa kumbukumbu ya sokoine jijini Mbeya.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog