Wachezaji waliowahi kutamba na mabingwa wa ulaya Real Madrid wanatarajiwa kuanza kuwasili nchini wakati wowte katika juma hili kwa ajili ya ziara nchini ikiwemo kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya mastaa wa Tanzania waliomaliza soka lao (Walio staafu).
Hivi sasa katika kila kona ya nchini ziara hii ya nyota hao ambao wanakubalika vilabu mbalimbali ulaya na duniani kwa jumla imekuwa gumzo na mashabiki wa soka nchini wanangoja kwa hamu agosti 23 ifike wakawashuhudie katika uwanja wa taifa.
Kwa muda mrefu toka ziara ya magwiji hao wa soka ianzwe kuzungumza, nimekuwa nikijiuliza ni ipi faida tutakayo ipata sisi wapenda soka la bongo kwa ujio huo wa magwiji wa soka nchini.
Kwa muda mrefu tumekuwa tunalia na kulalama juu ya matokeo mabovu ya timu yetu ya taifa na mara nyingi tulikuwa tunakimbilia kutoa sababu ya kukosa wachezaji wanao cheza ligi ya ushindani katika timu yetu ya taifa kama nchini nyingine za bara letu la Afrika.
Ni dhahiri kuwa ni vigumu kumvuta wakala ama mwakilishi wa kilabu toka kwenye ligi yenye ushindani kuja nchini kuangalia vijana wetu, na hata katika michuano ambayo vilabu na mawakala wanayotolea macho, timu zetu zimekuwa ndoto kupata nafasi ya kushiriki.
Je wenye dhamana na soka letu wanaitumiaje ziara hii, kwa faida ya soka letu, ama ni yale yale ya kuja kusimulia wajukuu kuwa nimesmshuhudia mchezaji bora wa dunia akicheza katika uwanja wetu wa Taifa.
Nikosa kubwa kama magwiji hao wa soka duniani kumaliza ziara yao nchini bila ya kushuhudi mechi walau moja ya vijana wakitanzania chini ya miaka 15 au 17.
Ni imani yangu kwa vipaji tuliovyo jaaliwa watanzania katika wachezaji wa 25 watakao cheza katika mechi hiyo, magwiji hao wasoka hawato kosa wachezaji walau watano wa kwenda kuwazungumzia huko mbeleni na walau siku moja tunaweza kushuhudia mawakala wakipiga hodi, Tanzania kuja kuangalia vipaji ambavyo walivyo visikia toka kwa magwiji hao.
Tanzania tumekosa wabalozi kwenye soka huko kwenye ligi za ushindani ambao, kwa uwezo wao uwanjani wanaweza kuwavutia mawakala kuja kuangalia madini yaliyopo Tanzania.
Tutakuwa kwenye hasara kama ujio wa Magwiji hao, utakuwa ni wakuja na kuondoka bila kuacha athari katika soka letu.
Kama bado hakuna mchezo wowote ulioandaliwa ni wakati wa ratibu wa ziara, TFF, vilabu na akademik kutumia fursa hii ya kuwanadi vijana wetu kwa magwiji hao wa dunia.