Zile stori za viongozi wa shirikisho la mpira wa miguu duniani FIFA
kutuhumiwa kula rushwa na kutumia madaraka vibaya, bado zinazidi
kuchukua nafasi katika vyombo vingi vya habari duniani, September 25
kutoka mtandao wa dailymail.co.uk umetangaza kuwa ofisi ya mwanasheria mkuu Uswiss imemfungulia mashitaka Rais wa FIFA Sepp Blatter.
Taarifa kutoka ofisi ya mwanasheria mkuu inamtuhumu Blatter
kwa makosa kadhaa ikiwemo ya utawala mbovu, kuingia mikataba mibovu ya
haki za matangazo ya TV akiwa pamoja na aliyekuwa Rais wa mpira wa miguu
wa CONCACAF Jack Warner mwaka 2005. Blatter pia anatuhumiwa kumlipa pound milioni 1.3 kinyume na taratibu Rais wa Shirikisho la soka barani Ulaya (UEFA) Michel Platini mwaka 2011 ikiaminika kuwa zilitumika kwa kampeni.
Ofisi ya mwanasheria mkuu Uswiss imeripoti kumfungulia mashitaka Sepp Blatter September 24. Ofisi ya Rais wa FIFA Sepp Blatter imechunguzwa mchana wa September 25 mjini Zurich Uswiss kama sehemu ya kuendelea kufanya uchunguzi kwa mamlaka husika.