Thursday, June 18, 2015


Klabu ya Liverpool imekataa rasmi ombi la pili la Manchester City la kutaka kumsajili mshambuliaji wa Uingereza Raheem Sterling.
Inaaminika kuwa ombi hilo jipya lilikuwa la kitita cha pauni milioni 35.5 ambacho kingeongezwa na kufika pauni milioni 40.
Sterling mwenye umri wa miaka 20 ambaye amehusishwa na Arsenal pamoja na Real Madrid ana thamani ya pauni milioni 50 kulingana na Liverpool.

Wiki iliopita Liverpool ilikataa kitita cha pauni milioni 25 kutoka kwa Manchester City.
Sterling alijiunga na Liverpool kutoka QPR mwaka 2010 na sasa yuko katika kandarasi hadi mwaka 2017, lakini amekataa ombi la malipo ya kitita cha pauni 100,000 kwa wiki.


Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, imewasili leo asubuhi Visiwani Zanzibar tayari kwa maandalizi ya mchezo wa siku ya jumamosi dhidi ya timu ya Uganda kuwania kufuzu kwa CHAN 2016.
Msafara wa Taifa Stars unajumuisha wachezaji 21 na benchi la ufundi 7 ambao wamefikia katika hoteli ya Nungwi Inn, mchezo dhid ya Uganda utachezwa katika uwanja wa Amani kisiwani Zanzibar jumamosi kuanzia majira ya saa 2 usiku.

Stars inakutana na Uganda katika mchezo huo wa awali wa kuwania kufuzu kwa fainali za mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Rwanda, kabla ya kurudiana wiki mbili baadae katika uwanja wa Namboole jijini Kampala.
Mara baada ya kurejea kutoka nchini Misri kikosi cha Stars kiliendelea na kambi katika hoteli ya Tansoma na kufanya mazoezi katika uwanja wa Karume kabla ya kuondoka leo asubuhi kuelekea visiwani Zanzibar.
Kocha mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij amewaongeza wachezaji watano ambao hawakua katika kikosi kilichocheza dhidi ya Misri, kufuatia wachezaji wa kimataifa wa Tanzania kutoruhusiwa kucheza mchezo huo wa CHAN wikiendi hii.


MSHAMBULIAJI wa timu ya Stand United,Abasarim Chidiebele akizungumza na waandishi wa habari mkoani Tanga mara baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja wa kuitumikia timu ya Coastal Union,Picha na Mwandishi Wetu,Tanga

MSHAMBULIAJI wa timu ya Stand United, Abasarim Chidiebele, amesaini mkataba wa kuitumikia timu ya Coastal Union kwa mkataba wa mwaka mmoja katika msimu ujao wa Ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara.
Chidiebele alitua mkoani Tanga juzi kwa ajili ya kuingia makubaliana na uongozi wa timu ya Coastal Union ambapo utiliaji saini huo ulishuhudiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu wa Coastal Union, Kassim El Siagi, Meneja wa Coastal Union, Akida Machai na viongozi wengine.
Akizungumza mara baada ya kusaini, Chidiebele amesema kuwa amefurahi kusajiliwa na Coastal Union na kuhaidi kutumia uwezo wake aliokuwa nao kwa ajili ya kuipa mafanikio timu hiyo katika michuano ya Ligi kuu msimu ujao.

waliotembelea blog