|
Mheshimiwa
Freeman Mbowe (mwenye miwani kushoto) na viongozi wengine wa CHADEMA
Taifa wakijadiliana jambo kabla ya kukabidhi msaada kwa wahanga wa mvua
kubwa ya mawe, kushoto kwa Mbowe ni mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Ally
Rufunga.
|
Sehemu
ya umati wa wafuasi wa CHADEMA walioongozana na mwenyekiti wao wa Taifa
Freeman Mbowe wakati wa kukabidhi msaada wa wahanga wa mvua ya mawe
iliyosababisha vifo vya watu 47. |
|
|
Mwenyekiti
wa CCM mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja akijiandaa kukabidhi msaada wa
fedha kwa niaba ya waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa.
|
Tafadhali
pokea msaada huu kwa niaba ya mheshimiwa Edward Lowassa kwa ajili ya
waathirika wote waliobomolewa nyumba zao kutokana na mvua kubwa ya mawe
pamoja na rambirambi kwa waliofiwa na jamaa zao, ndivyo anavyoeleza,
Khamis Mgeja (kulia) |
Maskini mtoto huyu hajui kitu gani kilichowasibu hadi kuwa katika hiyo ya maisha. |
|
Haya ndiyo makazi ya muda kwa sasa kwa wakazi wa kijiji cha Mwakata Kahama - Shinyanga. |
|
VIONGOZI wawili wa
kisiasa nchini wameungana na watanzania wengine katika kuwapa pole na
kuwafariji wahanga wa mvua kubwa ya mawe iliyonyesha na kubomoa nyumba
kadhaa za wakazi wa kijiji cha Mwakata wilayani Kahama mkoani Shinyanga
na kusababisha vifo vya watu 47 huku familia 450 zikibaki bila makazi.
Viongozi
hao ni pamoja na mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa
ambao kwa ujumla wao walikabidhi msaada wa fedha jumla ya shilingi
milioni 15.
Akikabidhi
msaada kwa niaba ya familia ya waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa,
mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja
alisema mara baada ya kutokea kwa maafa yaliyotokea, waziri mkuu mstaafu
na familia yake waliguswa na tukio hilo na hivyo kuona umuhimu wa
kuwasaidia wahanga wa maafa hayo.
“Mheshimiwa
mkuu wa mkoa wa Shinyanga na wakazi wote wa kijiji cha Mwakata, kwa
niaba ya familia ya waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa, naomba nikabidhi
msaada wa shilingi milioni tano kwa ajili ya wahanga waliokumbwa na
tatizo hili ikiwa ni pole na rambirambi kwa familia ya watu waliopoteza
maisha,”
“Binafsi
yeye mwenyewe alikuwa aje lakini kutokana na majukumu aliyonayo
ameniomba mimi mjumbe mwenzake wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC)
nifikishe salaam za pole na mchango wa kusaidia matatizo yaliyojitokeza
hapa, pia ameniomba niwaeleze kuwa anaungana na watanzania wote kutoa
pole zake za dhati kwa janga hili lililotokea,”
“Anasema
yeye yuko pamoja nanyi na anaungana na watanzania wengine wote na
kwamba janga hili siyo lenu peke yenu bali ni la watanzania wote na
ameahidi kuendelea kushirikiana nanyi kwa hali na mali mpaka pale hali
zenu zitakaporejea kuwa za kawaida, na pia anatoa pole kwa uongozi wa
serikali mkoani Shinyanga,” alieleza Mgeja.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CHADEMA wa Taifa Freeman Mbowe
mbali ya kukabidhi msaada wa shilingi milioni 10 kwa niaba ya chama
chake aliwataka watanzania wote hasa viongozi wa CCM kutochanganya mambo
ya siasa pale panapotokea janga lolote la kitaifa na kwamba tukio la
Mwakata ni janga la Taifa.
Mbowe
alisema kwa kawaida maafa yanapotokea hayana itikadi ya chama chochote
cha siasa na kwamba si vizuri kwa viongozi wa vyama vya kisiasa kugeuza
maafa ya kitaifa kuwa mashindano ya kisiasa na hakuna sababu yoyote ya
kushindana kuona nani katoa zaidi katika kuwafariji wahanga.
“Ndugu
zangu sisi CHADEMA tumeguswa sana kwa tukio hili, kwa hali hiyo tumeona
tutoe kitu kidogo ili kuwasaidia wenzetu walioathiriwa na mvua hii
kubwa, kwa sasa tutatoa shilingi milioni 10 ambazo hata hivyo tutaomba
mtueleze ni vitu gani mnavyohitaji, kama ni vifaa au vyakula mtueleze,”
“Tunasema
hivi kwa sababu tunaweza kuja na unga hapa kumbe kinachohitajika ni
mafuta ya kula, au tukaja na maharagwe kumbe wengine wameishaleta ya
kutosha na kinachohitajika ni mabati au mifuko ya saruji, hivyo baada ya
msaada huu wa leo, tunatarajia kufanya mkutano mkubwa mjini Kahama kwa
ajili ya kuchangia wahanga,” alieleza.
Akipokea
misaada hiyo mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga aliwapongeza
waziri mkuu mstaafu Lowassa na Mbowe kwa jinsi walivyoonesha kuguswa na
tukio hilo na kwamba misaada waliyoitoa itasaidia kupunguza makali ya
matatizo yaliyojitokeza baada ya mvua kubwa iliyoleta madhara kwa wakazi
wa Mwakata.
“Kwa
niaba ya mkoa wa Shinyanga tunawashukuru wote walionesha moyo wa upendo
wa kuwasaidia wahanga hao, na kwa upande wa mheshimiwa Mbowe nikupongeze
binafsi kwa jinsi ulivyoamua kuweka kando masuala ya kisiasa na
kutanguliza mbele uzalendo, tunakushukuru sana, mpaka sasa tunaendelea
kupokea misaada mbalimbali kwa ajili ya kaya 649 zilizoathiriwa na mvua
hiyo,” alieleza Rufunga.
Mpaka
Machi 9, mwaka huu idadi ya watu waliokufa kutokana na mvua kubwa ya
mawe iliyopewa jina la Tornado iliyonyesha hivi karibuni ilifikia watu
47 baada ya majeruhi mwingine aliyekuwa amelazwa katika hospitali ya
serikali mjini Kahama kufariki dunia juzi. Majeruhi wanne walikuwa
wakiendelea na matibabu katika hospitali rufaa ya Bugando jijini Mwanza.