Saturday, November 16, 2013


Duma waliokamatwa na kukabidhiwa maafisa wa huduma za wanyamapori.

WANAKIJIJI Kaskazini Mashariki mwa Kenya wamewakimbiza Duma wawili ambao wamekuwa wakiwaua Mbuzi wao na kuwakamata.
Wakaazi hao wanaoishi karibu na mji wa Wajir walisubiri hadi majira ya joto nyakati za mchana kuwafukuza Duma hao ambao baada ya kilomita sita walichoka na kusalimu amri.
Jamaa aliyeongoza uwindaji huo amesema aliamua kuchukua hatua baada ya Duma hao kuwaua mbuzi wake 15.
Duma hao walikamatwa wakiwa hai na wamekabidhiwa shirika la wanayapori KWS huku wana kijiji hao wakitaka kulipwa fidia ya mbuzi waliouawa.

Wanakiji hao waliambia BBC kuwa wanyama hao walikuwa wakiwashika Mbuzi wao mmoja baad ya mwingine kila siku.
"Nahitaji kulipwa fidia kwa sababu Duma hawa waliwala mifugo wangu wengi,'' alisema Nur Osman Hassan.
Mifugo ndio njia kubwa zaidi ya kujikimu katika jamii ya wasomali wakenya wanaoishi Kaskazini Mashariki mwa nchi ambako ukame ndio hali ya maisha ya kawaida kwao.
Mzee Hassan alisema kuwa Duma hao waliwaua Mbuzi wake 15 na kuwa walikuwa wakija nyumbani kwake kila siku.
Aliongeza kwamba, aliamua kurejea kijijini kupanga ambavyo angewakamata Duma hao wakati wa mchana ambapo Duma hao huwa wachovu.
"Nilikuwa nakunywa chai wakati nilipowaona wakimla Mbuzi mwingine, '' aliongeza kusema kuwa ulikuwa wakati wa asubuhi.
Alisema alisubiri hadi jua lilipokuwa kali mno na ndiposa walianza kuwakimbiza.
"Niliwaita vijana na kisha tukawakimbiza Mbuzi hao,'' alisema mzee Hassan.
''Tuliwakamata na kisha kuwaleta kwa maafisa wakuu kijijini mwetu.'' BBC



Wanawake wanaodaiwa kufanyabiashara ya ukahaba wakiwa Mahakama ya Jiji la Dar es Salaam, baada ya kukamatwa maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kinondoni. Oparesheni ya kuwakama wanawake hao inafanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni. 
Vijana waliokamtwa wakidaiwa kukutwa wakifanya mapenzi na wanawake hao wakificha sura zao wasipigwe picha.
  



Mwili wa Marehemu Dk. Sengondo Mvungi ukifanyiwa maombi mara baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo.
 
 Wanachama wa NCCR-Mageuzi wakiwa wamelibeba sanduku lililohifandhi mwili wa kiongozi huyo wa NCCR-Mageuzi na Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya.
Waombolezaji waliofika uwanjani hapo kuupokea Mwili wa Dk. Mvungi.
 
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba akiwa uwanjani hapo.
 
Baadhi ya waombolezaji waliofika uwanjani hapo.
Mjane wa Marehemu, Bi Anna Mvungi akiwa uwanjani hapo kuupokea mwili wa mumewe
Ndugu wakilia kwa uchungu…

Mwili wa aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya mabadiliko ya Katiba mpya na Mkurugenzi wa Katiba, Sheria na Haki za Binadamu wa NCCR-Mageuzi, Marehemu Dk. Sengondo Mvungi umewasili nchini kutoka Afrika Kusini.
Makumi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam, ndugu jamaa na marafiki wa Marehemu dk. Sengondo Mvungi walifika uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere upande wa Mizigo na kuupokea mwili wa kiongozi huyo na mwana familia.
Mapokezi ya mwili wa Dk. Mvungi aliyefariki juzi kufuatia majeraha ya shambulizi la majambazi lililomkuta nyumbani kwake nombemba 2 mwaka huu na kupeleka Nchini Afrika Kusini kwa Matibabu, yaliongozwa na Mkewe mama Anne Mvungi.
Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba mpya, Jaji na Waziri Mkuu Mstaafu, Joseph Sinde Warioba, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Sengondo Mvungi, Mwenyekiti wa NCCR-Magezi, na wajumbe takriban wote wa tume ya mabadiliko ya Katiba mpya.
Sanduku hilo lilifunikwa bendera ya Chama cha NNCR-Magezi.
Mwili wa marehemu Dk. Sengondo Mvungi unataraji kuagwa kesho katika viwanja vya Karimjee kabla ya kusafirishwa kwenda kijijini Kwao Kisangara juu, Wilaya ya mwanga mkoani Kilimanjaro kwa Maziko siku ya jumatatu.
________________
MUDA
TUKIO
LEO, NOVEMBA 15, 2013 – UWANJA WA NDEGE WA MWALIMU JK NYERERE
Saa 12:50 jioni
Kuwasili kwa mwili wa Marehemu – Uwanja wa Ndege wa Mwalimu JKN
KESHO, NOVEMBA 16, 2013 – VIWANJA VYA KARIMJEE
Saa 2:00 – 3:30 asubuhi
Kuwasili kwa Wageni, Wananchi na Waombolezaji
Saa 3:30 asubuhi
Kuwasili Mwili wa Marehemu
Saa 4:00 – 5:45 asubuhi
Ibada ya Misa Takatifu, Viwanja vya Karimjee
Saa 5:45 – 6:55 mchana
Salaam za Rambirambi na Neno la Shukurani
Saa 6:55 – 8:40 Mchana
Kuaga Mwili wa Marehemu
Saa 9:00 Alasiri
Msafara kupeleka mwili wa marehemu Kibamba Msakuzi
KESHO KUTWA, NOVEMBA 17, 2013 – NYUMBANI KWA MAREHEMU – KIBAMBA, MSAKUZI
Saa 2:30 – 4:30 asubuhi
Ibada ya Misa nyumbani kwa marehemu
Saa 5:00 asubuhi
Kuanza safari ya kwenda Chanjale, Kisangara Juu, Mwanga, Kilimanjaro
Mshindi wa kiti hicho, Diwani wa Kata ya Daraja Mbili, Prosper Msofe.
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeibuka kidedea katika uchaguzi wa Naibu Meya wa Jiji la Arusha, huku kikisisitiza msimamo wake wa kutomtambua Meya wa jiji hilo, Gaudency Lyimo (CCM).
Ushindi wa CHADEMA ulikuwa wa mteremko baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuacha kuweka mgombea huku mgombea wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Michael Kivuyo naye akijitoa siku moja kabla ya uchaguzi.
Hata hivyo, mshindi wa kiti hicho, Diwani wa Kata ya Daraja Mbili, Prosper Msofe, aliibua mzozo kwa madiwani wa CCM baada ya kutangaza msimamo huo wa CHADEMA kutomtambua meya.
Uchaguzi huo ulifanyika jana wakati wa kikao cha mwisho wa mwaka cha Baraza la Madiwani ambapo kulitanda ulinzi mkali wa polisi waliovalia kiraia, Usalama wa Taifa na wale wa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Kufanyika kwa uchaguzi huo, kumekata kiu ya wananchi wengi wa jiji hili, hasa kwa kuzingatia kwamba nafasi hiyo imekuwa wazi tangu Desemba 2010 baada ya uchaguzi uliofanyika awali kwa kumweka madarakani Lyimo, kudaiwa kuwa haukukidhi vigezo kisheria.
Hatua hiyo, ilimlazimu naibu meya aliyekuwa amechaguliwa kushika nafasi hiyo, Kivuyo (TLP) kujiuzulu.
Katika uchaguzi huo wa jana, Msofe aliibuka mshindi baada ya kupata kura 25 za ndiyo na mbili za hapana huku moja ikiharibika hali inayodhihirisha wazi kuwa madiwani wa CCM pamoja na wabunge wao nao walimchagua.
Habari toka ndani ya kikao hicho, zinadai kuwa mara baada ya Msofe kutangazwa kuwa naibu meya, alimweleza meya kuwa hamtambui kwani taratibu zilizotumika kumweka kwenye kiti hicho hazikuwa halali.
Akizungumza na Tanzania Daima nje ya kikao, Meya Lyimo alikiri kutolewa kwa kauli hiyo huku akidai kuwa inashangaza kwani yeye ndiye aliyesimamia uchaguzi uliomweka naibu meya huyo madarakani sasa inakuwaje asimtambue.
Alisema kuwa hakuna uchaguzi mwingine wa meya kwa sasa kwani sheria iko wazi kuwa uchaguzi hufanyika kila baada ya miaka mitano wanapochaguliwa madiwani wengine.
Katika uchaguzi wa kamati za kudumu za Mipango Miji, Mazingira na Ujenzi, Diwani wa Moshono, Paul Matthysen (CCM) aliibuka mshindi kwa kupata kura 11 dhidi ya moja aliyopata Diwani wa Elerai, Injinia,Jeremiah Mpinga ambapo kamati hiyo inaundwa na madiwani watano wa CHADEMA na sita wa CCM.
Uenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Elimu na Afya ulichukuliwa na Diwani wa Ngarenaro, Doita Isaya (CHADEMA) aliyepata kura tisa dhidi ya mbili alizopata Diwani wa Kata ya Engutoto, Elibariki Marlley (CHADEMA).
Wakizungumza na waandishi wa habari, Matthysen aliahidi kusimamia shughuli za kamati hiyo ipasavyo kwa kuhakikisha watendaji wanazingatia sheria kwa kuhakikisha hakuna ujenzi holela utakaoendelea kwenye Jiji la Arusha wala biashara zinazofanyika pembezoni mwa barabara za waenda kwa miguu na magari.
Naye Isaya aliahidi kufanya kazi kwa karibu na wanakamati wenzake pamoja na wakuu wa shule ili kuhakikisha watoto wanapatiwa elimu bora sanjari na kuwapunguzia wazazi mzigo wa michango mingi isiyo na tija.
Wakati huohuo, CHADEMA kimedai kuwa CCM haikusimamisha mgombea kwenye nafasi ya naibu meya kwa kuhofia kushindwa kutokana na kuwa na idadi ndogo ya madiwani.
CHADEMA walikuwa 15 huku wale wa CCM wakiwa 13 kutokana na mbunge wa viti maalumu, Namelock Sokoine kutohodhuria.

WATEJA katika mikoa inayopata umeme kwenye gridi ya Taifa wanatarajiwa kupata adha ya upungufu wa umeme kwa siku 11 kuanzia leo, kutokana na upungufu wa gesi kutoka katika Kisiwa cha Songosongo kilichopo wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi.
 
Hali hiyo imetajwa inatokana na kuwapo kwa matengenezo ya kiufundi kwenye visima vya gesi unaofanywa na Kampuni ya Pan African Energy Tanzania Limited (PAT).
 
Meneja Uhusiano wa TANESCO, Badra Masoud aliyasema hayo Dar es Salaam jana, akisema upungufu huo utatokea kati ya Novemba 16 hadi Novemba 26, mwaka huu na itahusisha maeneo yaliyopo katika mikoa iliyounganishwa katika gridi ya Taifa.
 
Tumepata barua kutoka kwa kampuni ya Pan African inayotuuzia gesi, wakisema inafanya matengenezo hayo kuboresha upatikanaji wa gesi ya kutosha kwenye visima hivyo. Uongozi unaomba radhi kwa usumbufu utakaojitokeza kwa baadhi ya maeneo yatakayokuwa yakikosa umeme,” alisema.
 
Kwa mujibu wa Masoud, kutokana na matengenezo hayo mikoa iliyounganishwa katika gridi ya Taifa itaathirika kwa kukosa umeme kwa baadhi ya maeneo na kwa nyakati tofauti na kuongeza huduma ya umeme ni muhimu kwa kila Mtanzania kwa ajili ya kujiinua kiuchumi na kipato, lakini matengenezo hayo ni muhimu kwani itaboresha upatikanaji wa gesi kwa ufanisi zaidi.
 
Aliitaja mikoa na maeneo yatakayokumbwa na upungufu wa umeme kuwa ni Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Dodoma, Morogoro, Singida, Mwanza, Mara, Mbeya, Iringa, Tabora, Shinyanga, Manyara na Zanzibar.
 
Masoud alisema gesi imekuwa ikiwawezesha kutoa Megawati 100 katika kituo cha Ubungo 1, Megawati 100 katika kituo cha Ubungo 2, kituo cha Tegeta Megawati 45 wakati Kampuni ya Songas imekuwa ikitoa Megawati 182 na kuongeza kutokana na matengenezo hayo kutakuwa na upungufu wa Megawati kati ya 150 na 200 na kwamba uzalishaji wa umeme kutumia mafuta na maji utaendelea.
 
Alisisitiza kuwa upungufu huo wa umeme sio mgawo ila ni kupitisha matengenezo ya kiufundi ya Kampuni ya Pan African ambayo alidai kuwa ilishaiomba Tanesco miezi miwili iliyopita ikitaka kufanya matengenezo hayo ambayo hayaepukiki na yenye lengo la kuleta ufanisi zaidi.
 
Masoud alitoa wito kwa wananchi kuwa wavumilivu siku hizo 11 wakati matengenezo yakifanyika na kuwa lengo ni kuboresha upatikanaji wa gesi ya kutosha kwa ajili ya kuzalisha umeme wa kutosha na kutoa huduma inayoridhisha ya nishati ya umeme kwa wateja wake.
Dar es Salaam. Marekani imetoa ripoti inayozungumzia usafirishaji wa binadamu ya mwaka 2013, huku ikiitaja Tanzania kuwa kinara wa kunyanyasa wasichana, kuwatumikisha katika ngono na usafirishaji wa binadamu.
 
Ripoti hiyo iliyotolewa na idara ya nchi hiyo inayohusika na diplomasia (US Department of State, Diplomacy in Action), pia inaitaja Tanzania kuwa ni kitovu cha njia ya kusafirisha wanawake, watoto na wanaume ambao hutumikishwa kwenye kazi za mashambani na biashara ya ngono.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa Julai mwaka huu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Seneta John Kerry inaweka bayana kwamba biashara ya usafirishaji wa binadamu hufanywa na baadhi ya ndugu na marafiki ambao hutoa ahadi kwa wahusika kwamba wanakwenda kuwasomesha au kuwatafutia ajira nzuri mijini.

Unyonyaji wa wasichana wadogo na utumikishaji majumbani ndilo tatizo linaloongoza, ingawa kesi za watoto kusafirishwa kwa ajili ya biashara ya ngono katika mpaka wa Tanzania na Kenya zinaongezeka. Pia, wasichana wananyonywa kwenye maeneo ya utalii,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto kutoka Burundi na Kenya, watu wazima kutoka Bangladesh, Nepal, Yemen na India wanatumikishwa kufanya kazi kwenye sekta za kilimo, madini na majumbani nchini Tanzania.

Baadhi ya raia kutoka nchi jirani huingia Tanzania kwa hiari yao, lakini hulazimishwa kufanya kazi majumbani kabla ya kupelekwa kutumikishwa kwenye biashara ya ngono Afrika Kusini, Ulaya na Mashariki ya Kati,” inaeleza.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki alimtaka mwandishi kumtumia ripoti hiyo kwa njia ya baruapepe ili aweze kuisoma na kuitolea maelezo.

Alipotafutwa siku ya pili, alisema kuwa ameipokea na kuikabidhi ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) ili ifanyiwe kazi na baadaye kutoa majibu.

“Ripoti niliipata nikaikabidhi ofisi ya DPP kwa kuwa wao ndio wanaoweza kuitolea maelezo baada ya kuisoma. Maoni yangu lazima yawe ya kitaalamu siwezi kusema bila kupata taarifa kutoka kwao,” alisema.

Lawama kwa Serikali

Ripoti hiyo inaitupia lawama Tanzania kwa kutokuwa na sheria thabiti za kupambana na biashara haramu ya kusafirisha binadamu, huku ikitolea mfano namna ilivyoshindwa kuwasaidia raia wake waliokuwa wakinyanyaswa nje ya nchi.

Kamati ya Serikali ya kupambana na usafirishaji binadamu, haijachukua hatua za kutosha katika kutekeleza mpango mkakati wa kupambana na vitendo hivyo,” inaeleza na kuongeza:

“Serikali imeshindwa kutenga fedha kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa usafirishaji wa binadamu kama ambavyo inaelekezwa kwenye sheria ya kudhibiti biashara hiyo ya 2008.”

Taarifa hiyo inaitaka Tanzania kuongeza nguvu katika kutekeleza sheria ya kudhibiti biashara ya kusafirisha binadamu ya 2008 kwa kuwakamata na kuwashtaki wahusika wote, lakini ikaikosoa kwa kusema inatoa adhabu ndogo kwa mtu anayebainika kufanya makosa, ikiwa ni pamoja na kumhukumu kwenda jela miaka 10, kulipa faini au vyote viwili kwa pamoja.

Sheria hiyo haifanani na nyingine kama za mtu anayepatikana na kosa la kubaka au kufanya kosa jingine la jinai. Mamlaka imesema ina kesi nne inazozichunguza, saba zipo mahakamani toka mwaka jana, zikiwepo mbili mpya,” inasema ripoti.

Pia, Serikali ya Tanzania imelaumiwa kwa kushindwa kuripoti maendeleo ya uchunguzi wa maofisa wake waliotuhumiwa kujihusisha na biashara ya usafirishaji binadamu.

LHRC na TGNP

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema tatizo la usafirishaji wa binadamu pia linachangiwa na wasichana kuwa na tamaa ya maisha mazuri, hivyo kukubali ahadi ambazo hupewa kwamba wanapelekwa kusoma, wasifahamu wanarubuniwa.

“Wengi wanatamani kwenda ‘majuu’ wakidhani watapata elimu, lakini baadaye wanaingizwa kwenye vitendo vinavyowafedhehesha na kuwafanya wakate tamaa kabisa,” alisema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Usu Mallya alisema katika siku za karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wasichana waliochukuliwa vijijini kwenda mijini kufanya kazi.

Alisema pamoja na tatizo hilo kuongezeka hapa nchini, hakuna tafiti za kutosha ambazo zimefanywa na wadau mbalimbali kuonyesha madhara yaliyopatikana hadi sasa.

Katika siku za usoni kumekuwa na ongezeko kubwa la vitendo vya kunyimwa chakula, kupigwa na kufukuzwa kazi huku wasichana wengine wakitumika kwenye biashara ya ngono,” alisema na kuongeza:

Ripoti hii isiishie kwenye makabrasha bali ifanyiwe kazi ili jamii yote ijue kuwa hili ni tatizo.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa watu 47,000 pekee ndio walioweza kuokolewa mwaka jana kutoka kwenye mazingira ya utumikishwaji kati ya milioni 27 waliopo katika hali hiyo duniani.

Tanzania imetajwa kuwa ni miongoni mwa nchi 44 ambazo zinajaribu kupambana na biashara hiyo, lakini hali inazidi kuwa mbaya zaidi

waliotembelea blog