Na Adam Mbwana, Dar es salaam
Ilikuwa
ni vita kali kati ya mafahali wawili ambao naweza kusema kila mmoja wao alikuwa
na azimio tofauti kichwani mwake juu ya mwenzie. Vita hii huwezi kuifananisha
na na zile za mwaka 1914 na 1939 ambazo ndio vita kubwa kuwahi kutokea duniani
pale ambapo mataifa makubwa yalikuwa yalikuwa yakiwania utajiri kwa kutumia
silaha kali na hatari duniani, lakini pia vita hii huwezi kuifananisha na ile
maarufu ya miaka ya 1960 kati ya Urusi na Marekani wataalamu wakiita vita
baridi ambayo haikutumia silaha kama sehem ya mapigano bali silaha ikitumika
kama sababu kubwa ya vita hiyo
Lakini
vita hii ni tofauti kabisa kwani inapiganwa katika mji ambao hauonekani kwa
macho huku vyombo vya habari vikitujuza uwepo wake wakati wahusika wake wakuu
wakiwa ni Romelo Lukaku na Josee Mourinho vita ambavyo havikuhitaji usuluhishi
bali kuisha kwake kulihitaji mmoja wao akubali masharti ya mwenzake au kama si
hivyo basi ilihitaji watu hawa kutengana kwa muda kama sio moja kwa moja.
Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho
Wahusika
hawa walikuwa na mawazo tofauti vichwani mwao, Lukaku akihitaji kuhakikishiwa
namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha Chelsea huku Mourinho naye
akimtaka Lukaku apiganie nafasi yake katika timu mbele ya washambuliaji wengine
kwenye timu kama Fernando Torres, Diego Costa na Didier Drogba. Na hapo ndipo
vita iliponoga zaidi.
Tangu
kusajiliwa kwake Chelsea August 2011 akitokea katika klabu ya Anderlecht ya
Ubelgiji kwa paundi milion 17, Romelo
Lukaku ameshindwa kabisa kuonyesha uwezo mkubwa katika klabu hiyo ya Chelsea
kama ambavyo wengi walitegemea.
Wengi walidhania kuwa Lukaku ndiye atakuwa
mrithi sahihi wa Didier Drogba katika safu ya ushambuliaji ya Chelsea kutokana
na ukweli kwamba wawili hawa wanafanana sana kwa maumbo yao makubwa, staili ya
kucheza kwa kutumia nguvu na hata kuwa na uwezo wa kuhimili beki zaidi ya
mmoja.
Diego Costa
Lakini hata hivyo mshambuliaji huyo mzaliwa wa Anrwerp nchinj Ubelgiji
alimaliza msimu wake wa kwanza darajani akiwa mchezaji wa kikosi cha akiba.
Hali
hiyo ilimfanya kupelekwa kwa mkopo msimu uliofuata wa mwaka 2012 katika timu ya
Westbromwich Albiol ambapo aliweza kufunga magoli 17 na kumaliza katika nafasi
ya sita ya wafungaji bora wa ligi kuu ya uingereza kwa msimu huo. Msimu
uliofuata wa 2013-2014 alipelekwa tena kwa mkopo katika klabu ya Everton ambapo
ambako nako alizifumania nyavu mara 15
katika mechi 31 alizocheza na kuisaidia Everton kumaliza katika nafasi
ya 5 ya ligi huku akiwa na uwiano mzuri wa magoli zaidi ya washambuliaji wa
chelsea Fernando Torres, Samuel Eto'o na Demba Ba ambao kwa pamoja waliweza
kufunga magoli 19 tu.
Maneno
yalianza kuibuka katika vyombo vya habari huku wachambuzi wa soka wakihoji
nafasi ya Lukaku katika safu ya ushambuliaji ya Chelsea ambayo ilionekana
kupwaya msimu uliopita chini ya kocha Josee Mourinho ambaye mara kwa mara
alikuwa akiwalalamikia washambuliaji wake hao kwa kushindwa kuzifumania nyavu
mara kwa mara.
Didier Drigbo amerudi Chelsea
Wachambuzi
hao walimpa Lukaku sababu ya kuanza kudai nafasi ya kudumu katika kikosi cha
Chelsea baada ya kumalizika kwa mkataba wake wa mkopo na Everton huku Mourinho
akiweka pamba msikioni na kuendelea na mpango wake wa kumsajili mshambuliaji
Diego Costa kutoka Atletico Madrid baada ya kuondoka kwa Samuel Eto'o na Demba
Ba.
Kwa
Lukaku hizi zilikuwa ni habari mbaya sana na ikawa ni moja ya sababu kubwa ya
kuchochea vita kati yake na Mourinho kwani yeye alitegemea baada ya kuondoka
kwa Etoo na Ba kungempa yeye nafasi ya kurudi kuchukua nafasi yake aliyokuwa
akiisubiri kwa muda mrefu lakini badala yake akaletewa kipingamizi kingine
ambaye ni Costa huku Mourinho akimpaka mafuta kwa mgongo wa chupa na kumwambia
kuwa apiganie nafasi yake. Lakini kilichommaliza nguvu kabisa Lukaku na kurejea
kwa Drogba klabuni hapo. Hapo ndipo Mourinho akamthibitishia Lukaku
hakumuhitaji tangu mwanzo. Kwahiyo Lukaku alishuhudia makombora na vifaru vya
kivita vikiingia kwenye ghala la silaha la Mourinho huku naye akishuhudia kwa
macho yake.
Hatimaye
Lukaku yakamshinda baada ya kuona adui yake hawezekaniki. Sasa ameamua kubwaga
manyanga na kunyoosha mikono juu kama ishara ya kusalimu amri baada ya
kukamilisha usajili wake wa kudumu katika klabu ya Everton wenye thamani
inayotajwa kufikia paundi million 28.
Lakini
suala la msingi la kujiuliza hapa ni Je, Mourinho alikuwa anataka nini cha
ziada kutoka kwa Lukaku ili aweze kumpa nafasi? na Je, madai ya Mourinho kuwa
Lukaku hakutaka kugombania nafasi kikosini ni ya kweli au ni kujisafisha tu
mbele ya vyombo vya habari? na swali la mwisho ni Je, kwanini Torres abaki
kikosini na kumuuza Lukaku ambaye msimu uliopita amefanya mambo makubwa zaidi
ya Torres licha ya kuwa na umri mdogo?
Waswahili
husema "funika kombe mwanaharamu apite". Hicho ndicho alichokifanya
Lukaku baada ya kuamua kukubali kushindwa dhidi ya Mourinho. Ameamua kuanza
maisha mapya Everton huku akimuacha Mourinho na pamba zake masikioni. Ama kweli
asiyekubali kushindwa sio mshindani.