KINYANG`ANYIRO
cha ubingwa wa ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2013/2014, bado
kinabaki kuwa kitendawili kwa timu zilizopo juu katika msimamo.
Sare
ya bao 1-1 jana uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam baina ya vinara
Azam fc dhidi ya Yanga imezidi kuweka mazingira magumu kwa mabingwa
watetezi, Young African.
Katika
mchezo huo uliovuta hisia za mashabiki, Yanga walikuwa wa kwanza
kufunga bao kipindi cha kwanza kupitia kwa Didier Kavumbagu, lakini Azam
fc walisawazisha dakika za lala salama kupitia kwa kinda, Kevin Friday.
Hiyo
ilikuwa mechi ya 19 kwa Yanga, wakati kwa Azam fc ilikuwa ya 20, huku
wakijikusanyia pointi 44, wakati Wanajangwani wakivuna pointi 40 katika
nafasi ya pili.
Yanga SC wamebakiza mechi 7, wakati Azam fc wamebakiza mitanange 6.
Mtatwaa Ubingwa? : Wachezaji wa Yanga wakishangilia bao la Didier Kavumbagu jana uwanja wa Taifa
Wikiendi
hii timu zote zitashuka dimbani. Yanga watasafiri mpaka mkoani Tabora
kuwafuata maafande wa Rhino Rangers, wakati jumapili machi 23, Azam fc
watawakaribisha JKT Oljoro, uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Rhino Rangers ndio wanaoburuza mkia katika msimamo wakiwa wameshacheza mechi 21 na kujikusanyia pointi 13 tu kibindoni.
Kwa
asilimia kubwa, maafande hawa wa Tabora, wameshachungulia kushuka daraja
na inawezekana hakuna muujiza wa kubaki ligi kuu msimu huu kwasababu ya
mazingira yao.
Mchezo dhidi ya Yanga utakuwa mkali endapo bado Rhino wanahitaji ushindi.
Lakini imani yao imeshuka na wanacheza bora liende na wameshapoteza matumanini ya kuendelea kucheza ligi kuu.
Pointi
13 kwa mechi 21 ni chache sana, zinahitajika nguvu za ziada kushinda
mechi zote 5 walizobakiza, hapo sasa tunaweza kuzungumza mengine.
Yanga wataingia uwanjani wakiwa ma matokeo ya sare ya jana na suluhu ya Mtibwa Sugar wiki iliyopita uwanja wa Jamhuri.