Jumamosi John Terry alicheza Mechi yake ya 500 kama Nahodha wa Chelsea na kusema anasikia fahari kuongoza Timu hiyo.
Terry, alivishwa Unahodha na kucheza Mechi yake kama Kepteni wa Chelsea Desemba 5, Mwaka 2001 walipofungwa kwao Stamford Bridge Bao 1-0 na Charlton Athletica na Jumamosi, akicheza Mechi yake ya 500 tangu Siku hiyo, aliiongoza Chelsea kuichapa Crystal Palace Bao 2-1 kwenye Mechi ya Ligi Kuu England na kendelea kutamba kileleni.
Mchezaji ambae alikuwa anashikilia Rekodi ya kuwa Nahodha kwa Mechi nyingi hapo Chelsea ni Lejendari Ron 'Chopper' Harris alieiongoza kwa Mechi 324.
Akielezea hali hiyo, Terry, mwenye Miaka 33, alisema: “Ukweli ni kuwa nafurahia Ukepteni. Napenda. Lakini ipo Siku nitakabidhi utepe na kutungika Buti. Kwa sasa niko safi, nacheza vizuri katika Kikosi kizuri na lengo letu ni kutwaa Mataji.”
Terry alitoa shukrani kubwa kwa Makepteni waliopita wa Chelsea, Marcel Desailly na Dennis Wise, ambao walimpa fursa na kumsaidia sana.
Alieleza: “Nakumbuka nilipopata Unahodha, Marcel alikuwa ndie Kepteni na akaitisha Mkutano na Menejimenti na Dennis. Walisema wakati wangu umefika. Nilikuwa bado Kijana lakini walinipa utepe na kuniongoza. Sitasahau hilo. Bila yao nisingeweza kufanya haya!”