SIKU chache baada ya msanii wa filamu na muziki wa mduara, Zuwena Mohamed ‘Shilole’, kutishia kumpa kisago msanii mwenzake ambaye pia ni mtangazaji, Christina John ‘Sinta’, mtangazaji huyo amefunguka na kumtaka aache mambo ya kizamani.
Shilole, majuzi kupitia mitandao ya kijamii, aliandika kukerwa na Sinta kwa kumbeza kuwa hawezi kuimba na mwanamuziki maarufu wa Marekani J. Lo na kuwa hizo ni ndoto za mchana, hivyo anamsaka na popote wakikutana atampa kipigo cha mbwa mwizi.
Akizungumza kwa simu na mtandao wa Gumzo la Jiji, Sinta alisema amekuwa akiambiwa na watu hasa wanaofuatilia mitandao kuwa eti anatafutwa kupigwa na Shilole, jambo linalomshangaza, kwani msanii huyo anapajua nyumbani kwake.
“Ninachoshangaa…huyo Shilole anapafahamu kwangu, aje basi anipige au ofisini kwangu anapajua, namkaribisha vizuri sana jamani!” alisema Sinta na kuongeza: “Mimi huwa sio mtu wa maneno, yeye aje tu anipige na sio kutangaza kwenye mitandao kuwa ananitafuta anipige, hayo mambo ya bifu siku hizi watu wanayachukulia upuuzi.
“Kutafuta pesa ndio mpango mzima, hivyo mimi namshauri Shilole kama ‘underground’ wa sanaa nchini, aachane na bifu, badala yake akazane kwenye mambo yake ya kutafuta pesa kwa ajili ya maisha yake na familia, kwani uzee unakuja.”
Chanzo cha ugomvi huo ulitokana na Sinta kuandika habari kwenye mtandao wake kuwa Shilole hawezi kuimba na Jennifer Lopez wa Marekani, bora hata Linah wa THT, kwa hiyo Shilole aache kuidanganya jamii.
Aidha mashabiki mbalimbali hasa wasomaji wa kwenye mitandao, wamemuunga mkono Sinta kuhusu kauli yake.
“Ni kweli jamani, Shilole hawezi kuimba na Jennifer Lopez, hayo ni masihara jamani, kwenda Marekani ndio aje kuongea ulojo kiasi hicho; kwanza ikumbukwe kuwa wasanii wote wa Tanzania kule Marekani hawajulikani hata, hasa kwa sisi tunaofuatilia tunajua,” alisema shabiki aliyejitambulishia kwa jina la Hamu Juma.