Baada ya kuwepo na taarifa
mbalimbali zinazozagaa kwenye mitandao ya kijamii zinazotokana na habari
iliyoandikwa na kuchapishwa kwenye gazeti la Jambo leo la June 24 2016,
toleo namba 2482 yenye kichwa cha habari “Sasa ukimwi kupimwa nyumba
kwa nyumba”.
June 28 2016 Ofisi ya Taifa ya
Takwimu ‘NBS’ imetoa ufafanuzi kwamba UKIMWI hautapimwa nyumba kwa
nyumba bali itafanya utafiti wa viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania
kuanzia September 2016 ambapo UKIMWI utapimwa kwenye kaya chache ambazo
zimechaguliwa kitaalam nchi nzima ili ziweze kuwakilisha kaya nyingine
nyingi ambazo hazitahusika moja kwa moja katika utafiti huo.
Taarifa iliyotolewa na NBS imesema utafiti huu utajumuisha kaya zipatazo 16,000
ambazo ni sampuli iliyochaguliwa kisayansi kutoka mikoa yote ya
Tanzania Bara na Zanzibar na utahusisha watu wazima wasiopungua 40,000 wakiwemo watoto takribani 8,000.
Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa katika utafiti huo kutakuwa na kupima homa ya ini, kupima wingi wa chembechembe za damu yaani CD4, kupima wingi wa virusi katika damu na kupima kiwango cha ufanisi wa dawa za kufubaza VVU kwa watu wanaotumia dawa hizo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa,
utafiti huo wa viashiria na Matokeo ya UKIMWI wa mwaka 2016 unafanyika
nchini kwa mara ya 4 ambapo utafiti wa kwanza ulifanyika mwaka 2003, wa
pili ulifanyika mwaka 2007 na wa tatu ulifanyika mwaka 2011.
Hivyo, Ofisi ya Taifa ya
Takwimu inapenda kuwatoa hofu wananchi kwakuwa utafiti huu sio mpya
katika nchi yetu na watanzania ambao wamekuwa wakipitiwa na utafiti huu,
wamekuwa wakitoa ushirikiano kwa zaidi ya asilimia 90.