SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) leo limesaini Mkataba wa udhamini wa miaka mitatu na mdhamini Mkuu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, wakati maandalizi ya ligi kuu yakiendelea.
Kampuni ya Vodacom Tanzania inayoongoza hapa nchini kwa huduma za mawasiliano imekuwa mdhamini wa ligi kuu kwa miaka minane iliyopita, na sasa imeingia mkataba mpya wa udhamini kwa miaka mitatu na TFF, mkataba utakao liwezesha shirikisho hilo kupokea fedha za udhamini kwa miaka mitatu.
Ligi kuu ya Vodacom 2015/16 inayotarajiwa kaunza katika siku za karibuni itachezwa katika viwanja mbalimbali na kushirikisha timu 16, zikiwemo timu za Mwadui na Africa Sports ambazo zimepanda daraja msimu huu.
Rais wa TFF, Jamali Malinzi (kushoto) pamoja na Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa kampuni hiyo Kelvin Twissa (kulia) wakiwa wameshika Mkataba mpya wa udhamini wa ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara 2015/16. Anayeshuhudia (katikati) kulia ni Ofisa Mkuu Mtendaji wa bodi y Ligi, Boniface Wambura.
Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Kelvin Twissa (katikati) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusiana na mkataba mpya wa miaka(3) wa udhamini wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliosainiwa baina TFF na kampuni hiyo, kushoto ni Rais wa TFF, Jamali Malinzi pamoja na Ofisa Mkuu mtendaji wa Ligi, Boniface Wambura (kulia)
Mkuu wa Mawasiliano na Masoko wa kampuni hiyo Kelvin Twissa, amesema kuwa kampuni ya Vodacom iko katika mstari wa mbele katika kuunga mkono maendeleo na shughuli mbalimbali za kimichezo ndani ya nchi.
“Wanamichezo wote ni mabalozi wazuri katika nchi. Ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa tunawaunga mkono katika kutambua na kukuza vipaji vyao kadri tutakavyo weza,” alisema Twissa na kuongeza kuwa, “Kama jina linavyojulikana ligi kuu ya Vodacom, ligi hii ni maarufu nchini na nje ya nchi na inafuatiliwa na mamilioni ya washabiki wa soka nchini .”
Twissa amejivunia kampuni hiyo kuwa wadhamini wa ligi kuu kwa kipindi kingine, na kufafanua kuwa mpira wa miguu ndio unaongoza kitaifa na unapendwa na Watanzania wengi.
Mkataba huu umehusisha pande zote ambazo ni kampuni ya Vodacom Tanzania, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na kamati ya ligi.
Kwa upande wake Rais wa TFF, Jamali Malinzi, ameipongeza kampuni ya Vodacom Tanzania akisema kuwa anaamini kuwa maendeleo ya sasa yatalenga zaidi katika kuunga mkono vipaji vipya na vilivyopo ndani ya nchi.
“Kwa niaba ya TFF, napenda kuwashukuru Vodacom Tanzania kwa kuonyesha nia na kuendelea kuunga mkono mpira wa miguu nchini. Nasi tunaahidi kuendelea kuthamini vipaji vya wachezaji wetu na kuhakikisha tunapata mafanikio zaidi,” alisema Malinzi.