Wednesday, August 12, 2015

MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga SC wameibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Prisons jioni ya leo katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Amisi Joselyn Tambwe alianza kuifungia Yanga SC dakika ya tano kabla ya kutoka kipindi cha pili kumpisha Malimi Busungu aliyeingia kufunga bao la pili dakika ya 84.  
Mwinyi Hajji Mngwali wa Yanga SC na Zam Kuffoh wa Prisons, wote walitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 88 baada ya kupigana uwanjani. 
Malimi Busungu amefunga bao la pili leo baada ya kutokea benchi

Huo unakuwa mchezo wa pili mfululizo Yanga SC iliyoweka kambi, Tukuyu, Mbeya kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii Agosti 22, mwaka huu Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam. 
Mchezo wa kwanza Yanga SC ilicheza na Kemondo Uwanja wa CCM Viwawa, Mbozi na kushinda 4-1 mabao yake yakifungwa na Tambwe, Simon Msuva na Godfrey Mwashiuya mawili.   
Yanga SC inayofundishwa na Mholanzi, Hans van der Pluijm itashuka tena dimbani Jumapili Uwanja wa Sokoine kumenyana na Mbeya City.
Yanga SC ilikuwa ina mpango wa kumenyana na timu za Malawi na Zambia pia katika kambi yao ya huko, lakini bado haijajulikana hadi sasa kama mpango huo utafanikiwa.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Mwinyi Hajji, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Thabani Kamusoko, Simon Msuva/Deus Kaseke dk58, Haruna Niyonzima/Salum Telela dk58, Donald Ngoma, Amissi Tambwe/Malimi Busungu dk79 na Godfrey Mwashiuya/Hussein Javu dk85.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog