|
Gari la kubeba maiti likiwasili katika eneo la Mvezo Resort kuchukua
mabaki ya miili ya watoto watatu wa Nelson Mandela iliyokuwa imezikwa
kinyemela katika eneo hilo na mjukuu wa kiongozi huyo, Mandela. |
Kwa ufupi
- Hilo ni kosa na ni kinyume cha sheria za nchi.
Maeneo ya makaburi yanalindwa na sheria hivyo ukienda kuchimbua mabaki
ya marehemu pasipo kibali kinachokubalika kisheria kufanya hivyo ni
matatizo na ndicho kilichotokea kwa sababu sheria hazikufuatwa (Profesa
Gutto.)
Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa
Mahakama wa kuamuru miili ya watoto wake watatu iliyohamishiwa Mvezo,
ifukuliwe na kwenda kuzikwa tena Qunu
Pretoria.
Vita ya wapi atakapozikwa Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini,
Mzee Nelson Mandela imefikia tamati na sasa ni rasmi kwamba atazikwa
Qunu uamuzi ambao umeacha ufa na uhasama mkubwa katika familia ya
kiongozi huyo.
Jana, mabaki ya miili ya watoto watatu wa Mandela
ambao ni marehemu ilitarajiwa kuzikwa upya katika eneo la Qunu, yakiwa
ni mazishi ya mara ya tatu tangu walipofariki dunia katika vipindi
tofauti, ukiwa ni utekelezaji wa amri ya Mahakama Kuu ya Eastern Cape.
Uamuzi
huo ulimaanisha kushindwa kwa mjukuu wa Mandela, Mandla ambaye jana
katika mkutano wake na waandishi wa habari alisema: “Sikusudii kukata
rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama,” lakini akahusisha ugomvi katika
familia ya babu yake kwamba ni vita ya fedha na mali za Mandela.
Mabaki
hayo ni ya mtoto wa kwanza wa kiume wa kiongozi huyo, Makgato
aliyefariki dunia 2005, binti yake wa kwanza Makaziwe (mkubwa) ambaye
alifariki akiwa mchanga mwaka 1948 na mtoto wake wa pili wa kiume,
Madiba Thembekile aliyefariki katika ajali ya gari 1969.
Mahakama
Kuu ya Eastern Cape ilitoa uamuzi uliowapa ushindi wanafamilia 16 wa
Mandela ambao walifungua madai wakiongozwa na shangazi yake Mandla,
Makaziwe.
Jaji Lusindiso Pakade katika hukumu yake, mbali na kutoa
amri hiyo alitaja vitendo vya Mandla kuwa ni vya aibu visivyo vya
kibinadamu hivyo kutoa amri ya kufukuliwa miili hiyo na kisha kurejeshwa
Qunu. Mabaki hayo yalihamishwa kutoka kijiji cha Mvezo ambako yalizikwa
mara ya pili kwa kificho miaka miwili iliyopita na mjukuu mkubwa wa
Mandela, Mandla ambaye pia ni kiongozi wa kimila katika kijiji hicho.
Kazi
ya kufukua makaburi ya watoto wa Mandela katika eneo la Mvezo
ilifanyika hadi juzi usiku chini ya ulinzi wa polisi baada ya madalali
wa mahakama kutumia sururu kuvunja lango (geti) kuu la kuingia katika
makazi ya Mandla.
Kwa mujibu wa msemaji wa polisi wa eneo hilo,
Luteni Kanali Mzukisi Fatyela, uchimbuaji wa makaburi ulifanywa na
wataalamu wa Kituo cha Afya cha Mthatha na baadaye kupelekwa katika
chumba cha kuhifadhia maiti cha kituo hicho juzi usiku na jana asubuhi
mabaki ya marehemu hao yalifanyiwa uchunguzi wa kimaabara kabla ya
kupelekwa Qunu kwa maziko.
Madaraka au fedha?
Makaziwe
(60) ambaye ni binti mkubwa wa Mandela na wenzake 15 kutoka katika
familia hiyo, walifungua madai wakitaka kurejeshwa kwa mabaki ya miili
hiyo Qunu wakisema Mandla aliyahamisha bila makubaliano ya familia.
Mandla katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Mvezo jana
alisema ugomvi uliopo ni wa kimasilahi na kwamba familia inawania fedha
za babu yake.
Alisema chimbuko la kuandamwa linatokana na msimamo
wake wa kukataa kuondolewa katika bodi ya ya mfuko wa Mandela baadhi ya
watu wakiwamo Wakili George Bizos na Waziri wa Makazi Tokyo Sexwale.
“Sasa wameamua kunilenga mimi kama mlengwa dhaifu.”
Kabla ya
familia kuamua kufungua kesi Juni 28, mwaka huu kiliitishwa kikao cha
familia na Mandla alihojiwa na kutakiwa arejeshe mabaki ya miili hiyo
Qunu lakini hakukubali na badala yake alitoka na kuacha kikao
kikiendelea, hatua ambayo ilitafsiriwa kuwa ni kudharau familia hiyo.
Mvutano
baina ya Mandla na shangazi yake Makaziwe anayewaongoza wanafamilia
wengine unatafsiriwa na baadhi ya watu kwamba ni vita ya kuwania
madaraka na fedha ikiwa Mzee Mandela atafariki dunia. Juzi, Msemaji Mkuu
wa chama tawala cha ANC, Jackson Mthembu alisema chama hicho hakiwezi
kuingilia masuala ya familia hiyo na kwamba kinaamini wana uwezo wa
kuyamaliza... “Tunasikitishwa na hali hiyo, inaweza kuharibu sifa ya
Mandela ndani na nje ya nchi, lakini tunaamini kwamba familia ina uwezo
wa kuyamaliza.” Inaaminika kuwa Mandela mara kadhaa alisema akifa
angependa azikwe Qunu ambako kuna makaburi ya familia yakiwamo ya watoto
wake, hivyo Mandla aliyahamishia Mvezo ikiwa ni hatua ya kushawishi
babu yake (Mandela) azikwe katika eneo hilo ambalo yeye ni kiongozi
wake.
Uamuzi wa Mahakama una maana kwamba kaburi la Mandela
litakapokuwa ni dhahiri ndipo makumbusho yake yatakapojengwa, hivyo kama
atazikwa Qunu basi makumbusho hayo yatakuwa mikononi mwa familia yake
na kama atazikwa Mvezo yatakuwa chini ya usimamizi wa Mandla ambaye ni
dhahiri tayari amekosa nafasi hiyo.
Katika hati yake ya kiapo
iliyowasilishwa mahakamani Mthatha, Mandla alidai kwamba anataka Mandela
azikwe Mvezo kwani ndiko alikozaliwa na kwamba eneo hilo lina umuhimu
wa kipekee katika historia ya babu yake.
Hivi sasa mjukuu huyo wa
Mandela ambaye pia ni Mbunge wa Eastern Cape, ana hoteli kubwa ya
kitalii yenye thamani ya mamilioni ya Dola za Marekani katika Kijiji cha
Mvezo. Mwaka jana mmoja wa wanakijiji wa Mvezo alimfungulia mashtaka
kwa tuhuma za kufukua makaburi kwa lengo la kujenga hoteli, lakini kesi
hiyo hadi sasa haijasikilizwa.
Mgawanyiko wa familia
Ni
dhahiri kwamba uamuzi wa juzi wa Mahakama umeiacha familia hiyo ya
Mandela vipande kwani Mandla anakabiliwa na kesi nyingine mbili za jinai
ambazo huenda zikafunguliwa siku chache zijazo katika Mahakama Kuu ya
Western Cape baada ya uchunguzi wa kipolisi kukamilika.
Kesi hizo
ni ile inayotokana na wanafamilia kutaka polisi wachunguze madai kwamba
Mandla ‘alichezea’ makaburi hali ambayo inaweza kusababisha uharibifu wa
mazingira kinyume cha sheria za Afrika Kusini na pili uchunguzi
unaolenga kubaini iwapo taratibu za kisheria kwa maana ya afya
zilifuatwa wakati wa uhamishaji wa mabaki ya marehemu hao miaka miwili
iliyopita. Polisi kwa upande mmoja na kituo cha afya kwa upande mwingine
katika eneo la Mthatha wamethibitisha kuanza kwa upelelezi huo dhidi ya
Mandla na ikiwa wataridhika, watamfungulia mbunge huyo mashtaka ya
jinai.
Mandla kwa upande wake jana aliweka bayana kuwa baadhi ya
watu siyo wanafamilia wa Mandela akiwarushia vijembe shangazi zake kwa
maelezo kuwa walishaolewa na kupoteza jina hilo kwani walikuwa wakitumia
majina ya waume zao.
“Sasa inaonekana kwamba kila mtu anaweza
kusema kwamba yeye ni Mandela kudai kuwa mwanafamilia ili kushiriki
katika uamuzi wa kifamilia, wameamua kuzikimbia familia zao na kurukia
katika ‘jahazi’ la Mandela.”
Afya ya Mandela
Mandela
hivi sasa yu mahututi kwa siku ya 28 na amelazwa katika Hospitali ya
Magonjwa ya Moyo, Medclinic iliyopo Pretoria akisumbuliwa na tatizo la
figo kushindwa kufanya kazi na hali yake inaelezwa kuwa ni mbaya.
Kesi
hiyo iliwezesha kufahamika kwa hali ya afya yake kwani kwa mara ya
kwanza, ilithibitika kwamba anapumua kwa msaada wa mashine na hiyo ni
kwa kujibu wa hati ya kiapo ya Makaziwe aliyoiwasilisha mahakamani
katika kesi hiyo ambayo pia inasema: “Matarajio ya kifo chake yamejengwa
kwenye msingi wa uhalisia.” Hati hiyo ya Juni 28, mwaka huu ambayo pia
inawahusisha wanafamilia wengine akiwamo mke wa Mandela Graca Machel na
mtalaka wa Mandela, Winnie inasema afya ya Mandela haitii matumaini huku
ikiweka bayana kwamba hati ya kiapo ya daktari ingewasilishwa
mahakamani kuthibitisha kwamba anasaidiwa na mashine kupumua.
Kadhalika,
hati hiyo inathibitisha kwamba lengo la kesi hiyo ni kuhakikisha
Mandela anazikwa katika eneo ambalo wanafamilia wengine wakiwamo watoto
wake wa kuwazaa wamezikwa na kwamba wanafamilia wanaamini kwamba hatua
ya kuhamishwa makaburi matatu kwenda Mvezo kulifanyika kwa masilahi ya
kifedha.
Hata hivyo, Mandla katika kiapo chake mahakamani alipinga
hoja kwamba Mandela yu mahututi na kwamba hata kama ni kweli suala hilo
halina uhusiano na mahali atakapozikwa.
“Ugonjwa hauna uhusiano
wowote na mahali atakapozikwa na hakuna maelekezo maalumu ya wasia
ambayo yanasema Mandela anataka azikwe Qunu,” inasomeka sehemu ya kiapo
cha Mandla.
Kwa mujibu wa sheria za Afrika Kusini zinazosimamia masuala ya mila na desturi, Mandla asingeweza kushinda kesi hiyo.
Gazeti
la Mail & Guardian lilimnukuu Mtaalamu wa Sheria na Katiba nchini
hapa Profesa Shadrack Gutto akisema kuwa sheria zinamtaka Mandla ambaye
ni kiongozi wa kimila wa Mvezo, Eastern Cape kufuata taratibu kabla ya
kuhamisha masalia hayo.
Profesa Gutto alisema ni dhahiri kwamba
Mandla hakufuata sheria na taratibu hizo kwani akiwa kiongozi wa Mvezo,
alipaswa kushauriana, kisha kukubaliana na kiongozi wa Qunu kabla ya
kufanya alichokifanya.