Na Baraka
Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Julai 18, 2014, saa 2:41 asubuhi
WAGONGA
nyundo wa Mbeya, Mbeya City fc wapo katika mkakati mzito wa kurejea na nguvu
mpya kwenye michuano ya ligi kuu, msimu wa 2014/2015 unaotarajia kuanza kushika
kasi septemba 20 mwaka huu.
Klabu
hiyo inayonolewa na kocha maarufu nchini na kocha bora wa msimu uliopita, Juma
Mwambusi ina nia ya kutwaa ubingwa msimu ujao baada ya kumaliza nafasi ya tatu
katika msimu wake wa kwanza.
Ikiwa ni
sehemu ya kujiweka sawa, Mbeya City fc itacheza mechi za kirafiki za kimataifa nchini
Malawi na Zambia .
Mwenyekiti
wa klabu hiyo, Mussa Mapunda alisema
wanatarajia kucheza angalau mechi mbili za kirafiki za kimataifa nchini Zambia
kabla ya kwenda Malawi kwa maandalizi zaidi.
“Malengo yetu
ni kutwaa ubingwa msimu ujao. Nina uhakika tutaweza kufanikiwa”. Alisema
Mapunda.
Mapunda
alisema maamuzi ya kuweka kambi nchi jirani
yamechagizwa na kitendo cha shirikisho la soka Tanzania kusogeza ligi mbele
mpaka septemba 20 mwaka huu.
Kocha wa Mbeya City fc, Juma Mwambusi (kushoto)
Kwa
upande wake, kocha Juma Mwambusi alisema amepanga programu nzuri ya mazoezi kwa
vijana wake, na anaamini watafanya kazi nzuri msimu ujao.
Mwambusi
alisema kikosi chake hakijabadilika sana kwasababu karibu wachezaji wote
wamebaki, achilia mbali wachache walioongezwa akiwemo Them Ferlix `Mnyama`
kutoka klabu ya Kagera Sugar.
“Malengo
yetu ni kufanya vizuri zaidi ya msimu uliopita. Tunajiandaa vizuri ili
kukabiliana na changamoto iliyopo mbele yetu”. Alisema Mwambusi.
Msimu uliopita,
Mbeya City ilimaliza katika nafasi ya tatu kwa kujikusanyia pointi 49.
Walifungwa michezo mitatu tu.
Walifungwa bao 1-0 na Yanga katika dimba la Taifa, wakafungwa 2-0 na Coastal Union, Mkwakwani Tanga na mechi ya mwisho kufungwa ni dhidi ya mabingwa Azam fc ambapo walilala mabao 2-1 katika uwanja wao wa nyumbani wa kumbukumbu ya sokoine jijini Mbeya.