Mshambuliaji
wa Simba sc, Mkenya Raphael Kiongera (kushoto) akimtoka beki wa Zesco
United, Benard Mapili katika mechi ya Tamasha la Simba Day, Agosti 9
mwaka huu. Msimbazi walilala 3-0 uwanja wa Taifa.
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
KARIBIA mwezi mmoja sasa tangu klabu ya Simba imfungashie
virago aliyekuwa kocha mkuu, Mcroatia Zdravko Logarusic.
Tukio hilo lilijiri muda mfupi baada ya Simba
kubamizwa mabao 3-0 katika mechi maalumu
ya Tamasha la Simba ‘Simba Day’ (Agosti 9 mwaka huu) iliyopigwa uwanja wa Taifa
jijini Dar es salaam dhidi ya Zesco United ya Zambia.
Loga katika mechi hiyo alifanya mabadiliko ya
wachezaji takribani 8 kwa lengo la kuwajaribu, wakiwemo wale waliokuja kufanya
majaribio kutoka Botswana, Kenya na Gambia.
Hata hivyo mabadiliko hayo hayakuinusuruu Simba na
kipigo hicho kilichozua mengi hasa baada ya Loga kuwatamkia maneno mabaya baadhi ya
wachezaji wakongwe kama vile Amri Kiemba na Shaaban Kisiga ‘Malone’.
Loga aliyekuwa ametoka kusaini mkataba wa mwaka
mmoja kuinoa Simba alivunjiwa mkataba huo na uongozi wa Simba na hatimaye
kuajiriwa kwa Mzambia Patrick Phiri.
Kurudi kwa Phiri kulileta faraja kubwa kwa
wachezaji wengi wa Simba waliokuwa wanampinga Loga kutokana na ukali uliozidi
kipimo.
Phiri ni kocha anayeifahamu Simba vizuri kwasababu
hii ni mara ya tatu kuiongoza, na ana rekodi ya kuipa ubingwa bila kufungwa
mwaka 2009.
Ujio wa Mzambia huyo umerudisha morali kwa
wachezaji wa Simba waliokuwepo kikosini kabla ya dirisha la usajili na wale
waliosajiliwa majira ya kiangazi.
Amiss Tambwe (kulia) hatacheza leo
Kwa bahati nzuri kocha huyo anaonekana kupendwa na
wapenzi wengi wa Simba wakiwemo viongozi wa ngazi ya juu kwasababu historia
inamlinda kwa kiasi kikubwa.
Phiri aliweka kambi kisiwani Unguja na huko ndiko
alitumia muda mwingi kuandaa kikosi chake kwa ajili ya ligi kuu soka Tanzania
bara.
Akiwa huko kocha huyu atakayekuwa mpinzani namba moja
kwa Marcio Maximo wa Yanga amekuwa akifanyia kazi mambo matatu makubwa katika
kikosi cha Simba.
Moja; amekuwa akiwafundisha wachezaji wake namna
ya kumiliki mpira kwa asilimia kubwa uwanjani. Lengo la Phiri ni kuifanya Simba
icheze zaidi uwanjani ikiwa na mpira ili kuwafanya wapinzani wachanganyikiwe.
Kumiliki mpira kwa kiwango cha juu husaidia zaidi
kuwapa presha wachezaji pinzani na kufungua mlango wa kupanga mashambulizi.
Pili; kocha huyu amekuwa akihangaika kuwafundisha
wachezaji wake namna ya upigaji wa pasi sahihi. Lengo ni kufuta pasi zisizokuwa
na macho kwa wachezaji wa Simba, Utamaduni wa Simba unaofahamika kwa muda mrefu
ni kupiga pasi fupifupi na haraka.
Phiri analifahamu hilo na ndio maana anawajenga
wachezaji wake katika msingi huo.
Tatu; Phiri amekuwa akihangaika kuwafundisha
wachezaji wake namna ya kupanga mashambulizi ya kasi. Kwa muda mrefu amekuwa
akihangaika na safu ya ushambuliaji na kiungo ili ziwe na ushirikiano mzuri wa
kupanga mashambulizi ya uhakika.
Rais
wa Simba sc, Evans Aveva (wa kwanza kushoto) alishuhudia Simba
ikichapwa 3-0 na Zesco Tamasha la Simba Day. Kulia ni aliyekuwa kocha wa
klabu hiyo, Zdravko Logarusic
Pia Phiri amefanya kazi ya kuwaweka pamoja
wachezaji baada ya presha ya Loga. Lengo ni kurudisha morali kwa wanandinga hao.
Kama ulibahatika kuiangalia Simba ikicheza
Zanzibar akicheza mechi za kirafiki au mazoezi ya Simba kuna kitu kipya
kimeongezeka.
Wachezaji wanaonekana kuonana na kucheza kitimu
zaidi. Hii ni kwasababu ya kocha Phiri ambaye amewaweka pamoja tena.
Leo hii Simba sc inacheza mechi ya kimataifa ya
kirafiki dhidi ya Gor Mahia ya Kenya katika dimba la Taifa jijini Dar es salaam.
Hii ni mechi ya kwanza ya kimataifa ya kirafiki
kwa Patrick Phiri tangu arejea Msimbazi. Kitakuwa kipimo kizuri kwake.
Pia mashabiki wa Simba wanaoishi Dar es salaam
wataiona timu yao ikicheza uwanja wa Taifa chini ya Phiri, lakini kwa bahati
mbaya baadhi ya wachezaji muhimu watakosekana katika kikosi hicho kutokana na majukumu ya timu ya Taifa.
Joram Mgeveke, Haroun Chanongo, Ramadhan Singano ‘Messi’,
Amri Kiemba, hawataonekana leo kwasababu wapo na timu ya taifa ya Tanzania,
Taifa Stars inayojiandaa na mechi ya kirafiki dhidi ya Burundi kesho mjini
Bujumbura.
Pia Amis Tambwe, Piere Kwizera wapo na timu ya
taifa ya Burundi, hivyo watakosekana.
Kocha mkuu wa Simba sc, Patrick Phiri
Hata hivyo wachezaji kama Masoud Cholo, Miraji Adam,
Hussein Sharrif, Ivo Mapunda, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Uhuru Seleman, Shaaban
Kisiga, Said Ndemla, Abdallah Seseme, Abdi Banda, Emmanuel Okwi na wengine
ambao sijawataja wataweza kuiwakilisha Simba.
Kimpira, kikosi cha Phiri kitaathirika kwa kiwango
fulani kwa kukosa wachezaji muhimu, lakini sio sababu ya kufanya vibaya.
Simba ina wachezaji wengi wanaofanya mazoezi na kwa
muda aliokaa Simba tangu aanze kazi, Phiri anajua ni nani anaweza kucheza
kikosi cha kwanza na mbadala wake ni nani.
Katika mechi za kirafiki Zanzibar, Phiri alikuwa
anachezesha vikosi viwili kwa lengo la kupata timu ya kwanza na wachezaji
mbadala wa kikosi cha kwanza.
Kwa kuwa bado hajaamua timu ya kwanza ni ipi, kila
mchezaji anajituma kutafuta nafasi ya kuonwa. Kwa mazingira hayo kila
anayepangwa anapigana kumshawishi Phiri.
Leo hii naitegemea Simba mpya inayocheza pasi za
uhakika, kasi ya kutosha, umiliki wa mpira na mashambulizi ya nguvu. Nasema
hivi kwasababu Phiri amekuwa akiifundisha timu yake katika aina ya mpira wa hivi.
Lakini siwapi Simba asilimia zote za kushinda
mechi ya leo kutokana na aina ya mpinzani wake, ila inaweza kushinda.
Gor Mahia imekaa pamoja kwa muda mrefu na
ilishiriki michuano ya kombe la Kagame iliyomalizika mwezi uliopita mjini
Kigali, Rwanda.
Phiri akiwa kazini
Japokuwa ilitolewa hatua ya makundi, lakini
ilionesha kiwango cha juu na ina wachezaji wazuri wanaoweza kuipa changamoto
nzuri Simba.
Kutokana na ubora wa Gor Mahia, nadhani hesabu za
Phiri zinatakiwa kukaa sawa zaidi ili kuipa ushindi timu yake.
Hii ni mechi ya kirafiki tu, lakini ina maana
kubwa kwa Phiri ili kuwaaminisha mashabiki wa klabu hiyo, ikizingatiwa upande
wa pili wamekuwa wakifanya vizuri na katikati ya wiki waliifunga Thika United
bao 1-0 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Cha msingi ni kwamba, mashabiki wa Simba lazima
watambue kuwa Gor Mahia ni wazuri na si rahisi kuwafunga.
Kama itatokea timu ikacheza tofauti na matarajio
yao, watakiwa kuwa na uvumilivu kwasababu ndio kwanza timu inaandaliwa.
Katika mechi za majaribio, makocha wanaangalia
vitu vingi. Wachezaji wanajaribiwa kwa nafasi tofauti.Kama ukiona Fulani kapangwa
namba tofauti, ujue kuna kitu kocha anakitafuta.
Wanasimba wasiende uwanjani kwa tambo na
kuwaangali Yanga wamefanya nini. Phiri na Maximo ni makocha wawili tofauti na
aina ya wachezaji wao ni tofauti.
Kama Yanga imeifunga Thika United ya Kenya, sio
lazima Simba kuifunga Gor Mahia ya Kenya. Ni timu mbili tofauti.
Phiri ni kocha mzuri na rekodi yake haina wasiwasi
kwa Simba, lakini kwa muda huu bado yuko kipindi cha mpito akitafuta timu ya
ushindani.
Anaweza kuwatumia wachezaji wengi leo hii
kwasababu ni mechi nzuri ya kimataifa ya kirafiki. Lengo lake ni kuona namna
wanasoka wake walivyomuelewe.
Nina imani kubwa na Phiri. Ni aina ya makocha
ninaodhani wanaweza kulisaidia soka la Tanzania, lakini naamini Wanasimba
watampa muda Mzambia huyu.
Rekodi ya nyuma isiwafanye wavimbe vichwa, mpira umebadilika
na kutoka 2009 akichukua ubingwa bila kufungwa mpaka sasa kuna mambo mengi
yametokea katika mpira wa Tanzania.
Kuna Azam fc, Mbeya City FC, Kagera Sugar, Ruvu
Shooting na timu nyinginezo. Upinzani umekuwa mkubwa, hivyo Phiri lazima
atahitaji kushindana zaidi.
Kwa mazingira ya sasa, Phiri sio lazima aweke
rekodi kama za nyuma na ndio maana hata Jose Mourinho aliyetamba na Chelsea
miaka ya 2006, aliporudi msimu uliopita alimaliza bila kikombe.
Sitegemei kuona mashabiki wanaizomea timu kwa
namna yoyote ile, kocha anahitaji muda pamoja na wachezaji wake.
Vijana wamekuwa wakifanya mazoezi magumu na
mepesi, hata miila yao bado haijawa tayari sana kwa kutandaza soka. Tusitegemee
makubwa kutoka kwao katika mchezo wa leo.
Kila la kheri Simba sc katika mchezo wa leo dhidi
ya Gor Mahia ya Kenya.