Mratibu
wa Mbio za Uhuru Marathon, Innocent Melleck akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam leo wakati akizungumzia maandalizi ya
uzinduzi wa Mbio hizo kwa Mwaka 2014,ambapo mwaka huu Mbio hizo
zitazinduliwa kwenye Kijiji cha Butiama,Mkoani Mara.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Selemani Nyambui akinzungumza kwenye Mkutano huo.
MBIO za Uhuru (Uhuru Marathon) zinatarajiwa kuzinduliwa
rasmi katika kijiji cha Butiama mkoani Mara, Agosti mwaka
huu, huku lengo kubwa likiwa ni kudumisha amani, umoja na
mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
jana, Mratibu wa Uhuru Marathon, Innocent Melleck alisema,
wameamua kuzindulia Butiama ili kumuenzi Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere ambaye katika uhai wake alipigania
mno mambo hayo.
“Tukumbuke Mwalimu Nyerere alipigania mno amani, umoja
na mshikamano miongoni mwetu, pia ndiye muasisi wa Taifa
hili, hivyo tuliona bora tukazindulie Butiama ili kumuenzi.”
Alisema, mara baada ya uzinduzi huo wanatarajia kuzunguka
nchi nzima kuanzia ngazi ya wilaya, ili kuzitambulisha mbio
hizo na kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa amani,
umoja na mshikamano miongoni mwetu.
Melleck alisema, kiini cha kuanza kampeni ya kuzindua
mbio hizo mapema imekuja, kwani zenyewe zimebeba
ujumbe wa amani, umoja na mshikamano, hivyo ni vyema
kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa kutunza na kuenzi
mambo hayo.
“Amani ya nchi yetu katika siku za hivi karibuni inaonekana
kwenda vibaya hasa kutokana na baadhi ya vyama vya siasa
kufanya siasa kwa visasi badala ya kujenga hoja kukabiliana
na changamoto za kisiasa, hivyo ni jukumu letu kuilinda,”
alisema.
Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT),
Selemani Nyambui alisema, kuanza maandalizi mapema kwa
mbio hizo ni faraja kwao na watahakikisha wanakabiliana na
changamoto zote ili ziweze kufana.
Mbio hizo zinatarajiwa kufanyika Desemba 8, mwaka huu na
kwa mara ya kwanza zilifanyika mwishoni mwa mwaka jana
na kushirikisha wanariadha kutoka nchi mbalimbali.