Uongozi wa Yanga umeweka bayana kwamba hauna mpango wa kumzuia mchezaji yeyote kuondoka iwapo atahitaji kuihama klabu hiyo
Kuelekea mwisho wa msimu Uongozi wa Yanga umetoa ruhusa kwa mchezaji yoyote kuondoka Yanga iwapo tu atafuata taratibu, Katibu wa Yanga Boniface Mkwasa alisema.
“Kama kuna Mchezaji anataka kuondoka basi awe muungwana, atueleze mapema na taratibu zifuatwe, Pia kama kutakuwa na mchezaji ambaye Mwalimu anona hamuhitaji sisi tutafuata taratibu na kumueleza mapema kabisa.” Alisema katibu huyo wa Yanga kwa mujibu wa Shaffih Dauda Blog.
Wakati akiyasema hayo Mkwasa kuna hatari timu ya Yanga ikawakosa wachezaji wengi muhimu ambao mikataba yao inaelekea kuisha ndani ya Yanga, Wazimbambwe wawili Donald Ngoma na Thabani Kamusoko wanaelekea kumaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu huu na uongozi wa klabu hiyo haujaweka bayana kuhusu kuwaongezea mikataba mipya.
Pia mabeki wa kati wazawa Kelvin Yondani na nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ mikataba yao inafikia tamati mwisho wa msimu, kadhalika kwa mshambuliaji Anthony Mateo na beki wa kimataifa wa Togo Vicent Bossou.
Kwa sasa wapo katika maandalizi kwa ajili ya mechi ya kombe la shirikisho Afrika dhidi ya MC Alger katika uwanja wa Taifa na watarudiana wiki moja baadaye huko Algeria.