|
Madhara ya mvua hiyo
|
|
Mbunge wa Jimbo la Msalala Mheshimiwa Ezekiel Maige |
-
- Kufuatia
tukio la kusikitisha na kuhuzunisha lililotokea usiku wa kuamkia Machi
4,2015 huko katika kata ya Mwakata wilayani Kahama mkoani Shinyanga la
watu 42 kupoteza maisha na wengine 91 kujeruhiwa kutokana na mvua kubwa
iliyokuwa imeambatana na upepo na mawe,mbunge wa Jimbo la Msalala
kulikotokea tukio hilo,Mheshimiwa Ezekiel Maige,amezungumzia tukio hilo.
Alichokisema hiki hapa chini:
-
Nimepokea
kwa mshituko mkubwa taarifa za mvua kubwa, yenye upepo na theluji
nyingi iliyonyesha kwa muda wa dakika 35 tu saa 5 usiku wa kuamkia leo
Jumatano Machi 4,2015.
Nimepata taarifa za tukio hilo nikiwa safarini Kigoma kikazi na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa ambayo mimi ni mjumbe.
Kutokana
na uzito wa tukio hili nimesitisha ziara hiyo na kuondoka Kigoma majira
saa 5 asubuhi na hivyo kufika Mwakata saa 2 usiku huu.
Hali niliyoikuta kama wengi walivyokwishatoa ushuhuda ni ya kusikitisha na kushangaza sana.
Sijawahi kuona maafa yatokanayo na mvua katika jimbo langu miaka yote niliyoishi hapa.
Maafa ni makubwa yasiyoelezeka.
Naomba kusema yafuatayo:-
Kwanza, nawapa pole sana familia zote zilizopoteza wapendwa wetu.
Mungu awarehemu wapendwa ndugu zetu waliopoteza maisha katika tukio hili.
Aidha
namuomba Mungu atupe moyo wa ujasiri kuikabili hali hii na atupe nguvu
za kusimama haraka na kurejea kwenye hali ya maisha yetu ya kawaida.
Pia namuomba Mungu atuepushe na mitihani ya kiwango hiki ambayo kwa kweli ni mizito.
Pili, nawashukuru
sana viongozi wa serikali na Chama, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati
ya maafa wilaya ya Kahama ambaye ni mkuu wa wilaya ya Kahama Benson
Mpesya kwa juhudi kubwa walizofanya kuokoa majeruhi na kusaidia
wahanga.
Wamefanya
kazi kubwa sana kwani, hadi jioni nilipofika kwenye eneo la tukio,
majeruhi wote 91 walikuwa wamefikishwa hospitalini na walikuwa
wanaendelea kupata matibabu na miili ya marehemu kadhaa ilikuwa imeanza
kuzikwa.
Aidha nawashukuru kwa kusaidia vitu mbalimbali ikiwemo vyakula.
Tatu, nawashukuru
sana watu wote wenye mapenzi mema ambao wameanza kutupatia misaada
mbalimbali ikiwemo unga, mablanketi, sukari, mikate na vinywaji
mbalimbali.
Nawaomba
watu wote wenye mapenzi mema waendelee kusaidia kwani waathirika ni
wengi, zaidi ya 4,000 hivyo hali itazidi kuwa mbaya jinsi siku
zitakavyosonga mbele endapo ndugu zetu hawatapatiwa msaada.
Nne, mimi
kama Mbunge wa eneo husika, pamoja na kusikitishwa na tukio hili, natoa
wito kwa serikali, hasa Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha maafa,
makampuni, taasisi, mashirika na watu binafsi wasaidie kwa haraka
misaada ya chakula, mavazi na makazi kwa waathirika.
Binafsi nitawasilisha msaada wangu wa tani 5 za unga kesho asubuhi tarehe 5,Machi ,2015 .
Tano, naomba
sana watu wote wenye mapenzi mema wasaidie kurudisha maisha ya
waathirika kwenye hali ya kawaida hasa kwa kuwasaidia vifaa vya ujenzi
kama mbao, bati na theluji.
Sita, ombi
maalum kwa serikali, naomba sana serikali itoe punguzo maalum la ushuru
kwenye simenti, nondo na mabati kwa wananchi wote wa Kahama ambao wengi
wao wana nyumba za tope zilizoezekwa kwa nyasi, na hivyo kutokuwa imara
kuhimili upepo mkali au mvua kubwa.
Inavyoonekana,
mabadiliko ya tabia nchi sasa ni dhahiri kwamba matukio ya kimbunga au
mvua kubwa zenye upepo yanazidi kuongezeka Kahama, kwani ni wiki moja tu
imepita tangu mvua yenye upepo iliponyesha kwenye kijiji changu cha
Segese ambapo nyumba zaidi ya 50 zilianguka au kubomoka na nyingine
nyingi kuezuliwa mapaa.
Tukio hilo liliathiri hata nyumbani kwa mzazi wangu ambapo ukuta wa uzio ulianguka!
Ukiangalia maeneo yaliyoathirika, idadi kubwa ya nyumba zilizoanguka ni nyumba za tope zilizoezekwa kwa nyasi.
Hivyo maafa yanakuwa makubwa maeneo yetu haya kutokana na nyumba zetu kutokuwa imara.
Hivyo
ni lazima sasa wananchi wetu tuwasaidie kujenga nyumba imara
zinazohimili upepo mkali na mvua zenye dhuruba hali inayoonekana kuwa
ikijirudiarudia.
Kwa mara nyingine natoa pole sana kwa wote na kuwaomba wadau wote wasaidie kwa kadiri watavyoweza.
Misaada yote ipelekwe kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala au Mkuu wa Wilaya ya Kahama.