Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
YANGA SC itakutana na Azam fc katika mchezo mkali
wa Ngao ya Jamii kuashiria kupenuliwa kwa pazia la ligi kuu soka Tanzania bara
jumapili (septemba 14 mwaka huu) uwanja wa Taifa, jijini Dar es salaam.
Kuelekea katika mchezo huo, mshambuliaji Jeryson
Tegete hayuko fiti kucheza kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya nyonga.
Mbali na nyota huyo mzaliwa wa Mwanza,
mshambuliaji mwingine wa Yanga, Mbrazil, Andrey Coutinho yupo hatarini kukosa
mechi hiyo kutokana na majeruhi ya mguu aliyoyapa jumatano ya wiki hii katika
mechi ya kirafiki dhidi ya Polisi Dar es salaam.
Mechi hiyo iliyomalizika kwa suluhu pacha ya bila
kufungana ilipigwa uwanja wa Shule ya Sekondari, Loyola, Mabibo jijini Dar es
salaam.
Kwa sasa Yanga wameweka kambi katika Hoteli ya
Tansoma, iliyopo eneo la Gerezani, Dar es salaam.
Baada ya Coutinho kuumia siku hiyo, leo hii Polisi
Dar wamesikitishwa na majeruhi hayo na
kumuombea dua njema ili awe fiti kwa ajili ya mechi ya keshokutwa uwanja wa
Taifa.
Kocha na mratibu wa Polisi Dar, Kennedy Mwaisabula
‘Mzazi’ kwa niaba ya klabu hiyo amemtakia afya njema Coutinho akimuombea apone
haraka.
“Kama kocha na mratibu wa Polisi Dar, kwa niaba ya timu yetu tunamtakia afya njema
na apone haraka Andrey Coutinho mchezaji wa Yanga, Raia wa Brazil aliyeumia kwa bahati mbaya mno
dhidi ya mechi yetu siku ya jumatano.”
Amesema Mwaisabula dakika chache zilizopita kupitia akaunti yake ya mtandao wa
kijamii ya facebook.
Coutinho ameonekana kuwateka mashabiki wa Yanga
kwa uwezo wake wa kupiga mashuti ya mbali, kumiliki mpira, kupiga mipira ya
adhabu ndogo na kupiga pasi za uhakika.
Nyota huyo amemzidia kete, Mbrazil mwenzake,
Geilson Santos Santana ‘Jaja’ ambaye mpaka sasa hajakubalika miongoni mwa
mashabiki wa Yanga wakidai ni mzito sana anapokuwa uwanjani.