Friday, September 12, 2014


 
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
YANGA SC itakutana na Azam fc katika mchezo mkali wa Ngao ya Jamii kuashiria kupenuliwa kwa pazia la ligi kuu soka Tanzania bara jumapili (septemba 14 mwaka huu) uwanja wa Taifa, jijini Dar es salaam.
Kuelekea katika mchezo huo, mshambuliaji Jeryson Tegete hayuko fiti kucheza kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya nyonga.
Mbali na nyota huyo mzaliwa wa Mwanza, mshambuliaji mwingine wa Yanga, Mbrazil, Andrey Coutinho yupo hatarini kukosa mechi hiyo kutokana na majeruhi ya mguu aliyoyapa jumatano ya wiki hii katika mechi ya kirafiki dhidi ya Polisi Dar es salaam.
Mechi hiyo iliyomalizika kwa suluhu pacha ya bila kufungana ilipigwa uwanja wa Shule ya Sekondari, Loyola, Mabibo jijini Dar es salaam.
Kwa sasa Yanga wameweka kambi katika Hoteli ya Tansoma, iliyopo eneo la Gerezani, Dar es salaam.
Baada ya Coutinho kuumia siku hiyo, leo hii Polisi Dar wamesikitishwa na majeruhi hayo  na kumuombea dua njema ili awe fiti kwa ajili ya mechi ya keshokutwa uwanja wa Taifa.
Kocha na mratibu wa Polisi Dar, Kennedy Mwaisabula ‘Mzazi’ kwa niaba ya klabu hiyo amemtakia afya njema Coutinho akimuombea apone haraka.
“Kama kocha na mratibu wa Polisi Dar,  kwa niaba ya timu yetu tunamtakia afya njema na apone haraka Andrey Coutinho mchezaji wa Yanga,  Raia wa Brazil aliyeumia kwa bahati mbaya mno dhidi ya  mechi yetu siku ya jumatano.” Amesema Mwaisabula dakika chache zilizopita kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii ya facebook.
Coutinho ameonekana kuwateka mashabiki wa Yanga kwa uwezo wake wa kupiga mashuti ya mbali, kumiliki mpira, kupiga mipira ya adhabu ndogo na kupiga pasi za uhakika.
Nyota huyo amemzidia kete, Mbrazil mwenzake, Geilson Santos Santana ‘Jaja’ ambaye mpaka sasa hajakubalika miongoni mwa mashabiki wa Yanga wakidai ni mzito sana anapokuwa uwanjani.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog