Tuesday, July 28, 2015



Mbunge wa Ilala mheshimiwa Mussa Zungu leo amefungua mashindano ya Airtel Rising Stars mkoa wa Dar es Salaam na kuwataka vijana kucheza kwa kujituma ili kuwa wachezaji bora na hatimaye kulinusuru taifa na matokeo mabaya katika medani ya kimataifa.
Zungu amelitaka Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kuhakikiha kwamba timu zote za ligi kuu na daraja la kwanza zinakuwa na timu za vijana. “Kwa bahati nzuri, mashindano ya Airtel Rising Stars yamewapa fursa nzuri na ni vema makocha wa ligi kuu wakayatumia kupata vijana wenye vipaji na kuwaendeleza”, alisema.
Alisema mbali ya kuwa jukwaa la kubaini wachezaji wenye vipaji, Airtel Rising Stars pia yanawahamasisha vijana kushiriki mazoezi hivyo kuwa na afya njema ili kukabiliana na masomo yao.

Aliwaambia vijana kwamba kwa dunia ya leo mpira ni chanzo cha kutumainiwa cha ajira kwa mamilioni ya vijana ambao wanaishi maisha mazuri kwa kuwa wanalipwa mishahara mizuri.
Aliwataka viongoizi wa soka kuchagua wachezaji watakaoshiriki fainali za taifa kwa kuzingatia uwezo na siyo upendeleo wa aina yoyote. Wakati mashindano ya mkoa yakiendelea makocha watateua vijana wenye vipaji kuwakilisha mikoa yao kwenye fainali ya taifa.
Kwa upande wake Rais wa TFF Jamal Malinzi ameishukuru kampuni ya Airtel kwa kubuni programu hii ili kutumika kama jukwaa linatotumika kubaini vipaji vya wanasoka chipukizi. Alisema kuwa mashindano ya Airtel Rising stars yameifanya kazi ya TFF ya kutafuta vipaji vya soka kuwa rahisi zaidi.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi wa IT wa Airtel Tanzania Franky Filman amewashukuru wadau wote wa soka kwa kuyaunga mkono mashindano ya Airtel Rising Stars na kuyapa umuhimu yanaostahili. Pia amewataka makocha kutumia mashindano hayo kuimarisha vikosi vyao.

Mashindano ya Airtel Rising yanajumuisha mikoa ya kisoka ya Ilala, Temeke, Ilala Morogoro, Mbeya, Mwanza na Arusha itahitimishwa kwa michuano ya taifa itakayofanyika uwanja wa kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 11 hadi 21.


Mbunge wa Ilala Musa Zungu akisalimiana na wachezaji wakati akifungua rasmi mashindano ya Airtel Rising Stars. Leo Jijini Dar-es-Salaam.

Mbunge wa Ilala Musa Zungu akiongea na wachezaji wakati wa ufunguzi wa mashindano ya Airtel Rising Stars Mbeya, Leo jijini Dar-es-Saam.

Mbunge wa Ilala Musa Zungu akipiga mpira kuashiria ufunguzi wa mashindano ya Airtel Rising Stars Mbeya, Leo jijini Dar-es-Saam.

Mkurugenzi wa IT wa Airtel Frank Filman akiongea wakati wa ufunguzi wa mashindano ya Airtel Rising Stars Mbeya, Leo jijini Dar-es-Saam.


Donald Ngoma aliyesajiliwa Yanga SC mwezi uliopita kutoka FC Platinum ya kwao Zimbabwe anatarajiwa kuwa mwiba kwa safu ya ulinzi ya Azam FC kesho
Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
WAKATI kesho Azam FC na Yanga SC zinakutana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, mchezo huo umekuwa gumzo kubwa.
Hiyo itakuwa mara ya pili, Yanga SC na Azam FC kukutana katika Kombe la Kagame, baada ya mwaka 2012 kukutana katika fainali pale pale Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam.
Ilikuwa Julai 28, mwaka 2012 katika mchezo uliochezeshwa na refa Thierry Nkurunziza wa Burundi, Yanga SC ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-0 wafungaji Hamisi Kiiza ‘Diego’ dakika ya 44 na Said Bahanunzi ‘Spider Man’ dakika ya 90 na ushei.
Moja kati ya mambo yanayozungumzwa sana kuelekea mchezo huo ni juu ya mshambuliaji mpya wa Yanga SC, Mzimbabwe Donald Ngoma aliyesajiliwa mwezi uliopita kutoka Platinum FC ya kwao.
Katika mechi nne ambazo Ngoma ameichezea Yanga SC hadi sasa amefunga mabao matatu, mawili katika mechi za kirafiki moja katika Kombe la Kagame.
Lakini Ngoma ameonyesha ni mshambuliaji mpya hatari kwa mabeki kwenye safu ya mbele ya Yanga SC, kwani ana kasi, nguvu na uwezo wa kumiliki mpira.
Anarukia mipira ya juu, ana nguvu akiwa hewani kiasi kwamba ni vigumu mabeki kumdhibiti- huo ni mtihani haswa kwa safu ya ulinzi ya Azam FC kesho.
Bahati mbaya, Ngoma ameonyesha ni mchezaji mwenye hasira, baada ya kutolewa kwa kadi nyekundu katika mchezo wa kwanza tu dhidi ya Gor Mahia na kuponza timu yake kulala 2-1.
Ilikuwa ni kadi ya pili ya njano, baada ya kumsukuma kwa nguvu kama anapiga ngumi mchezaji wa Gor Mahia, aliyetaka kumtumia kama ngao ya kuinuka baada ya wote wawili kuangukia nje ya Uwanja wakati wakigombea mpira.
Na katika mechi kubwa kama hizi, wachezaji wengine huwafanyia wachezaji wa timu pinzani mambo ya kuudhi na yenye kuzalisha hasira.
Kama wachezaji wa Azam FC watafanya mpango wa kumtia hasira Ngoma arudie makosa ya kwenye mechi ya ufunguzi dhidi ya Gor, utakuwa mtihani kwa Mzimbabwe huo.
Yote kwa yote, Ngoma ni mchezaji ambaye hata benchi la Ufundi la Azam FC chini ya kocha Mkuu, Muingereza Stewart Hall linajua ni hatari.
Lakini je, Ngoma ataweza kuupenya ukuta wa Azam FC, ambao hadi sasa haujaruhusu bao hata moja katika mashindano haya? Bila shaka dakika 90 za mchezo wa kesho zitatoa majibu.
Hamisi Kiiza (jezi namba tano) akipongezwa na wenzake jana baada ya kufunga
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uganda, Hamisi Friday Kiiza ‘Diego’ jaja amefunga bao lake la kwanza akiichezea kwa mara ya kwanza klabu yake mpya, Simba SC katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Kombaini ya Zanzibar.
Katika mchezo huo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar Simba SC ikicheza kwa mara ya kwanza chini ya kocha wake mpya, Muingereza Dylan Kerr iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Bao lingine la Simba SC lilifungwa na Nahodha mpya wa klabu hiyo, Mussa Hassan Mgosi.


waliotembelea blog