Friday, November 1, 2013


SERIKALI iko katika mazungumzo na nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Burundi ili kushirikiana kwa baadhi ya maeneo, hasa kutokana na ukweli kuwa baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Rwanda, Kenya na Uganda, zimeonesha mwelekeo wa kujitenga.
 
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, alisema hayo jana alipokuwa akitii mwito wa Spika, Anne Makinda, kujibu maswali ya wabunge, waliokuwa wakihoji kwa nini Tanzania nayo isijitenge.
 
“Kiuchumi sisi ni majirani zaidi na DRC… Rwanda inaangalia barabara tunayoshirikiana kuijenga kufika Burundi, ila ujenzi wa reli ya Uvinza-Msongati itaokoa wenzetu wa Burundi, kwani wakitumia bandari ya Mombasa kwenda Bujumbura, kwao ni mbali kwa zaidi ya kilometa 900, tofauti na Dar es Salaam kwenda Bujumbura,” alifafanua Sitta.
 
Kabla ya kutoa ufafanuzi huo, wabunge walitaka Serikali isikubali kuchezewa na baadhi ya nchi za EAC na kuitaka ijitoe mara moja na ikiwezekana, iunde Jumuiya yake ikishirikisha Burundi na DRC.
 
Aliyeibua suala hilo la kutaka Tanzania ijitenge ni Mbunge wa Viti Maalumu, Rukia Ahmed (CUF), ambaye katika swali lake la nyongeza aliitaka Serikali ieleze inasubiri nini kujitoa katika Jumuiya hiyo kutokana na kuendelea kutengwa na marais wa Rwanda, Kenya na Uganda ambao wamekuwa wakikutana bila Tanzania na wanajumuiya wengine kushirikishwa.
 
Pia, alitaka nchi ijitoe kwa kutumia Ibara ya 145 ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya hiyo na kunukuu kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kuwa Tanzania inasubiri talaka kutoka jumuiya hiyo.
 
Mbali na swali hilo la nyongeza, katika swali la msingi, Mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba (CCM), alisema kabla ya Rwanda na Burundi kujiunga na EAC, hali ilikuwa tulivu na yenye maelewano makubwa.
 
Aliongeza kuwa baada ya nchi hizo kujiunga na Jumuiya, sasa hali ni tete na kuhoji ni kitu gani kilisababisha nchi hizo kujiunga na Jumuiya na kwa nini Tanzania isijitoe kama ilivyofanya kwenye Soko la Pamoja la Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA).
 
Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango-Malecela (CCM), alitaka Tanzania isitishe kushiriki shughuli zote za Jumuiya kwa kile alichosema inaelekea kufa. Kutokana na uzito wa suala hilo, Spika wa Bunge, Makinda alimtaka Waziri Sitta, kujibu maswali hayo kwa pamoja. Kero, kususa Sitta alisema ni kweli inakera kuona wanajumuiya wengine wanaizunguka Tanzania na kusema hawajakaa kimya katika kushughulikia suala hilo.
  
Alisema kwa sasa mambo yote yanayohusu Jumuiya, ambayo baadhi ya nchi wanachama wamekutana kwa siri na kuyatolea msimamo na kuja nayo katika mikutano ya pamoja, Tanzania haitashiriki. Alitoa mfano wa mambo yanayohusu sera za mambo ya nje, ambapo alisema yeye hatashiriki vikao vyote, ambavyo wanajumuiya wengine tayari wana msimamo.
 
“Kesho (leo), Burundi kuna mkutano, nimemwambia Naibu Waziri asihudhurie, Katibu Mkuu wa Wizara atakwenda lakini hatatoa msimamo wowote wa Serikali, maana si kazi yake, bali yetu sisi wanasiasa,” alisema Sitta.
 
“Tulishamhoji Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa EAC kuhusu hili, kama tutaendelea na uongo wa kitoto tutakuja bungeni, kwenu waheshimiwa wabunge na kumaliza hili, hatutakubali liendelee, lakini kwa sasa tufuatilie mpaka mwongo aumbuke,” alisema Sitta.
 
Alisisitiza kwamba huu ni wakati wa kufuata ushauri wa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, aliyepata kusema “Mtu mwongo mwongoze”, na kuongeza kuwa kama wana Jumuiya wengine wana hila, itajulikana tu, kwa kuwa hata juzi walikutana Kigali, Rwanda bila kushirikisha Tanzania. Sitta alisema baada ya wiki mbili, majibu ya Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo, yatatolewa na hapo nchi itatoa uamuzi.
 
Akijibu swali la nyongeza la Komba, aliyetaka kujua kwa nini Jumuiya hailaani vitendo vya kuunda Jumuiya mpya ndani ya nyingine na kuitaka Tanzania iunde Jumuiya yake na DRC na Burundi, na swali la Ahmed aliyetaka Tanzania isisubiri talaka kujitoa, Sitta alisema haijaanzishwa Jumuiya nyingine, ila wapo katika harakati fulani.
 
Kuhusu kutosubiri talaka, Sitta alisema asilimia 52 ya eneo la Afrika Mashariki, linaundwa na Tanzania huku asilimia 48 ikichukuliwa na nchi nyingine, hivyo suala la nani anatoa talaka, lina uzito kwetu zaidi na kuongeza kuwa, kama ni nani mwoaji, Tanzania ndiyo imeoa na labda ndiyo itoe takala na si kupewa.
 
Msimamo Sitta akijibu swali la Msingi la Ahmed, aliyetaka kujua msimamo wa Serikali wa mambo yanayohusu Jumuiya hasa kutokana na mkutano uliofanyika Mombasa siku ya ufunguzi wa bandari hiyo, kujadili pamoja na mambo mengine, masuala ya biashara, miundombinu na Shirikisho la Afrika Mashakiri, alisema mikutano ya wakuu wa Kenya, Rwanda na Uganda bila kuishirikisha Tanzania, ilianza Entebbe, Uganda Juni 24 na 25.
 
Alisema mkutano wa pili ulifanyika Mombasa Agosti 28 kwa kigezo cha uzinduzi rasmi wa gati namba 19, ambayo imepangwa mahususi kushughulikia mizigo ya Rwanda na Uganda.
 
"Pamoja na suala hilo la bandari ya Mombasa, ilijitokeza kwamba wakuu hao wa nchi tatu walijadili pia masuala ya uanzishwaji wa Himaya Moja ya Forodha, uanzishwaji wa hati moja ya kuishi katika nchi hizo (viza) kwa watalii, matumizi ya vitambulisho vya Taifa kwa nchi zao na harakati za Shirikisho la Kisiasa la nchi zao.
 
“Kwa kuzingatia kuwa masuala hayo yapo katika hatua mbalimbali za majadiliano katika Jumuiya na nchi zote tano hushiriki, Tanzania katika mkutano wa 27 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya uliofanyika Arusha Agosti 31, tulidai ufafanuzi," alisema Sitta.
 
Alisema walimtaka Mwenyekiti wa Baraza kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu mikutano hiyo ya utatu inayoendeshwa sambamba na mikutano ya kawaida ya kalenda za Jumuiya na kwamba kikao cha Baraza hilo cha kutathmini hali hiyo, kinatarajiwa kufanyika wiki ya pili ya mwezi ujao Arusha.
 
Sitta alisisitiza wakati taarifa hiyo ikisubiriwa, msimamo wa Tanzania ni kuwa masuala yote yanayojadiliwa na kuamuliwa nje ya utaratibu wa Jumuiya, haitayatambua kama uamuzi wa Jumuiya na utekelezaji wake utahusu nchi husika pekee.
Kifo kujirudia? Iwapo sintofahamu hii itaendelea kama ilivyo na hata kufikia hatua ya Tanzania kujitoa, EAC itakuwa inasambaratika kwa mara nyingine, baada ya kutokea hivyo mwaka 1977.

Tukio la mwaka 1977 lilitokana na nchi tatu wanachama wakati huo, Tanzania, Kenya na Uganda, kutofautiana kisiasa huku Tanzania na Uganda zikiwa katika uhusiano mchungu uliosababisha vita baina yao.
 
Wakati Jumuiya ya kwanza ikivunjika, nchi hizi zilikuwa zikiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania, Mzee Jomo Kenyatta wa Kenya na Dk Milton Obote wa Uganda, ambao wote sasa ni marehemu.
 
Novemba 30, 2001 Jumuiya ilifufuliwa chini ya marais Mwinyi (Tanzania), Daniel arap Moi (Kenya) na Yoweri Museveni wa Uganda katika sherehe zilizofanyika Arusha.
 
Rwanda na Burundi zilijiunga rasmi na Jumuiya hiyo Juni 18, 2007 katika mkutano wa marais wa EAC jijini Kampala, Uganda, na kushuhudiwa na marais Mwai Kibaki (Kenya), Museveni, Jakaya Kikwete (Tanzania), Paul Kagame (Rwanda) na Pierre Nkurunziza (Burundi).

waliotembelea blog