Saturday, September 12, 2015



Staa wa mchezo wa Tennis, Serena Williams na superstaa wa muziki wa Hip hop Drake wamekuwa topic kwenye mitandao mingi baada ya tetesi nyingi kusambaa kuwa wawili hao wapo kwenye mahusiano ya kimapenzi.
drake
Yote yalianza siku ambayo mapaparazzi walimnasa Drake kwenye picha akiwa kwenye mashindano ya Serena Williams huko Australia… haikuishia hapo, baada ya Serena kushinda Australia Open Championships, Drake alionekana tena kwenye mashindano yake ya French Open (Roland Garros), Wimbledon na haya ya jana U.S Open Championships.
drake2
Sasa jana staa huyo wa tennis aliweka headlines tofauti baada ya kukosa ushindi kwenye U.S Open dhidi ya Roberta Vinci wa Italy… Cha kushangaza zaidi mashabiki wamemshambulia Drake na kumlaumu sana kwa kitendo cha Serena Williams kukosa ushindi huo!
drake5
Mashabiki wanadai kuwa Drake amekuwa kikwazo kwenye mashindano haya na amemchanganya sana Serena kiasi cha kumfanya ashindwe kuweka akili yake yote kwenye mashindano hayo, mashindano ambayo kama Serena Williams angeshinda basi angeweka historia ya kuwa mwanamke mweusi kushinda mashinano yote hayo kwa mfululizo!
drake4
Nimefanikiwa kuzinasa baadhi ya tweets za mashabiki kwenye Twitter wengi wanatumia hashtag ya #BlameDrake kuelezea hisia zao..


LIGI KUU VODACOM, VPL [Vodacom Premier League], inaanza Jumamosi kwa Mechi 7 na Jumapili Mabingwa Yanga kushuka Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam kucheza na Coastal Union.
Hiyo Jumamosi, Washindi wa Pili wa VPL, Azam FC, wako kwao Azam Complex, huko Chamazi kwenye Viunga vya Jiji la Dar es Saalam kucheza na Prisons wakati Vigogo Simba kusafiri kwenda Mkwakwani, Tanga kuivaa African Sports iliyopanda Daraja Msimu huu.
Mechi nyingine ni Ndanda FC ya Mtwara kuwa wenyeji wa Mgambo Shooting Uwanjani Nagwanda Sijaona mjini Mtwara, Wana Lizombe Majimaji wakiwa wenyeji wa Maafande wa JKT Ruvu katika Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Stand United FC watawakaribisha Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Toto Africans watawakaribisha Mwadui FC Uwanja wa CCM Kirumba na Mbeya City watacheza na Kagera Sugar katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Jumapili VPL itaendelea kwa mchezo mmoja tu utakaochezwa katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es salaam ambapo Mabingwa Watetezi Yanga watawakribisha Wagosi wa Kaya Coastal Union.


Mabingwa Watetezi Barcelona na Real Madrid, Wikiendi hii wanarejea tena kwenye La Liga baada ya kusimama kwa Wiki 2 kupisha Mechi za Kimataifa na wote wapo Ugenini wakibadilishana Miji ambayo ndio makazi yao.
Jumamosi, Barcelona wako Ugenini huko Jiji la Madrid kucheza na Atletico Madrid Uwanjani Vicente Calderon wakati Real Madrid wako Jijini Barcelona kucheza na RCD Espanyol Uwanjani Estadi Cornellà-El Prat.
Mbali ya kubadilishana Miji, Barca na Real kila mmoja anamvaa Mpinzani wa Jadi wa mwenzake lakini kitu kingine cha kuvutia ni kutaka kuona kama Masupastaa wa La Liga, Cristiano Ronaldo na Lionel Messi kama wataweza kufungua hesabu zao za Magoli Msimu huu mpya baada ya kutoka kapa katika Mechi 2 za La Liga kwa Timu zao hadi sasa.
Kwa Wikiendi hii La Liga itaanza Ijumaa kwa Mechi 1 kati ya Levante na Sevilla na Jumamosi zipo Mechi 4 na Jumapili 4 huku Jumatatu ikichezwa Mechi 1.
LA LIGA
RATIBA
Ijumaa Septemba 11

2130 Levante v Sevilla FC
Jumamosi Septemba 12

1700 RCD Espanyol v Real Madrid CF
1915 Sporting Gijon v Valencia C.F
2130 Atletico de Madrid v FC Barcelona
2300 Real Betis v Real Sociedad
Jumapili Septemba 13
1300 Granada CF v Villarreal CF
1700 Athletic de Bilbao v Getafe CF
1915 Celta de Vigo v Las Palmas
2130 Malaga CF v SD Eibar
Jumatatu Septemba 14
2130 Rayo Vallecano v Deportivo La Coruna
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kwa udhamini wa kampuni ya Azam Media kupitia Azamtv Sports leo wamezindua kombe la Shirikisho litakalofahamika kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) ambalo litaanza kutimua vumbi mwezi Novemba mwaka huu kwa kushirikisha timu 64 nchini.

Kurudishwa kwa michuano hii imekua ni faraja kwa wapenzi na wadau wa mpira miguu nchini baada ya kukosekana kwa takribani miaka 13 michuano hiyo, ambapo sasa Bingwa wa kombe la Shirikisho ataiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika (CAFCC).

Akiongea na waandishi wa habari wakati wa uzindizi wa michuano hiyo na kuchezeshwa droo ya awali, Rais wa TFF Jamal Malinzi amemshukuru Mkurugenzi wa Azam Media Rhys Thorrington kwa kuweza kudhamini michuano ambayo itongeza ushindani zaidi nchini.

Malinzi amesema anaviomba vilabu vitakavyoshiriki michuano ya kombe la hilo, vionyeshe ushindani mkubwa kwani ndio nafasi pekee ya kuweza kuitangaza na kuonekana kwa kuwa michuano hiyo itakua ikionyeshwa moja moja na luninga ya Azamtv.

Aidha Malinzi amesema kila timu inayoshiriki michuano hiyo itapata fedha ya usafiri shilingi milioni 3, na vifaa vitakavyotolewa na mdhamini kampuni ya Azam Media.

Naye Mkurugenzi wa Azam media Rhys Thorrington amesema uhdmaini huo wa miaka mine una thamani ya fedha za kitanzania bilioni 3.3 ambapo timu zitakazoshiriki michuano hiyo zitapata nafasi ya kuonekana moja moja katika nchi zaidi ya saba barani Afrika kupitia kituo chao cha azamtv.

Mshindi wa Kombe la ASFC linalodhaminiwa na kampuni ya Azam kupitia Azamtv Sports, atajinyakuliwa kitita cha shilingi milioni hamsini (TZS 50,000,000), jumla ya timu 64 kutoka Ligi Kuu (VPL), ligi daraja la kwanza (FDL) na ligi daraja la pili (SDL) zitashirki katika kombe hilo.
Jamal Malinzi, Rhys Thorrington
Timu zote 24 za ligi daraja la pili na 8 za ligi daraja la kwanza 3, zilizopanda daraja na 5 zilizoshika nafasi za chini kwenye makundi yote zitashiriki katika raundi ya kwanzamwezi Novemba kwa kucheza mechi 16 na kupata washindi 16 ambao wataingia raundi ya pili.

Timu 16 zilizoshinda raundi ya kwanza na 16 zilizofanya vizuri ligi daraja la kwanza zitachanganywa na kupangwa kucheza mechi 16 nyingine za raundi ya pili mwezi Desemba.

Washindi wa raundi ya pili wataingia raundi ya tatu ambapo watachanganywa na timu 16 zilizopo ligi kuu na kuchezwa mechi 16 nyingine ambazo washindi wake wataingia raundi ya nne. Raundi hii ya tatu itafanyika mwezi Januari 2016.

Timu 16 zilizoshinda raundi ya tatu zitaingia raundi ya nne zitapangwa ili kucheza hatua hii ambayo itakuwa na mechi 8 na washindi 8 wataingia katika hatua inayofuata ambayo ni raundi ya tano au robo fainali. Raundi hii ya nne itachezwa Februari 2016.

Washindi wa raundi ya nne watapata nafasi ya kuingia raundi ya 5 ambayo pia ni robo fainali, droo itapangwa. Raundi hii ya tano itachezwa mwezi Machi 2016.

Washindi wa raundi ya tano au robo fainali watapangwa kucheza nusu fainali au raundi ya 6 mwezi Aprili.

Washindi wa nusu fainali watapambana katika fainali na kumpata bingwa wa Azam Sports Federation Cup 2015/16. Mechi ya fainali itachezwa wiki moja baada ya ligi kuu kumalizika na Bingwa atakabidhiwa kombe na zawadi ya fedha tasilimu shilingi milioni 50.

Mechi za raundi ya kwanza na raundi ya pili kama mshindi hatapatikana ndani ya dakika 90 basi mshindi atapatikana kwa kupigiana penati moja kwa moja. Mechi za raundi ya tatu na nne kama mshindi hatapatikana ndani ya dakika 90 mechi itarudiwa katika uwanja wa timu iliyokuwa mgeni mechi ya awali.

Mechi za robo fainali au raundi ya tano kama mshindi hatapatikana ndani ya dakika 90 hatua ya penati tano tano itaamua mshindi.

Kwa mechi za nusu fainali na fainali kama mechi itaisha kwa sare ndani ya dakika 90, dakika 30 za nyongeza zitachezwa, na kama hakutakuwa na mshindi penati zitaamua mshindi.

Raatiba ya raundi ya kwanza:
AFC -Arusha Vs Polisi Mara, Polisi -Tabora Vs Green Worries -Dar es salaam, Karikoo Lindi Vs Changanyikeni -Dar es salaam, Mkamba Rangers –Morogoro Vs Mvuvuma - Kigoma, Rhino Tabora Vs Allicane - Mwanza, Panone Kilimanjaro Vs Coca Cola Mbeya, Polisi Morogoro Vs Mshikamo Dar es salaam, Sabasaba Morogoro Vs Abajalo Tabora.

Magereza Iringa Vs Polisi Dar es salaam, Milambo Tabora Vs Town Small Ruvuma, Abajalo Dar es salaam Vs Transit Camp Dar es salaam, Ruvu Shooting Vs Cosmopolitan Dar es salaam, JKT Rwamkoma Mara Vs Villa Sqaud (Dar es salaam), Wenda FC Mbeya Vs Madini Arusha, Pamba FC Mwanza Vs Polisi Dom, Singida United Vs Bulyanhulu FC Shinyanga

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kitatoa tuzo kwa Rais Jakaya Kikwete pamoja na wanamichezo 10 waliofanya vizuri zaidi katika miaka 10 akiwa Rais wa Tanzania.
Taarifa ya Mweyekiti wa TASWA, Juma Abbas Pinto imesema kwamba tukio hilo ambalo pia litahudhuriwa na Rais Kikwete, litafanyika Oktoba 8, mwaka huu ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam likiwa na lengo la wanamichezo kumuaga Rais Jakaya Kikwete.
Pinto amesema TASWA itakabidhi tuzo maalum kwa Rais ikiwa ni kuthamini mchango wake kwa maendeleo ya michezo wakati wa miaka 10 ya uongozi wake na imebariki tukio hilo kama  ‘JK na Wanamichezo’.

Rais Jakaya Kikwete akikata utepe wa jengo la studio za Azam FC wakati wa uzinduzi Machi 6, mwaka huu. Kulia ni Mwenyekiti wa makampuni ya Bakhresa Group, wamiliki wa Azam Media Limite, ambao ndiyo wamiliki wa Azam TV, Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na kushoto ni Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara.

Amesema licha ya kutoa tuzo kwa Rais na wanamichezo 10 waliofanya vizuri zaidi, pia TASWA itatoa vyeti maalum kwa kampuni mbalimbali zilizosaidia kwa kiasi kikubwa kudhamini michezo katika miaka 10 ya Rais Kikwete.
Amesema maandalizi muhimu yamekamilika kuhusiana na tukio hilo, ambapo wawakilishi kutoka vyama vyote vya michezo hapa nchini pamoja na wanamichezo wataalikwa kuhudhuria tukio hilo la kihistoria.
Amesema TASWA inamshukuru Rais Kikwete kwa kukubali kujumuika nao siku hiyo ili kuagana na wanamichezo, ambao wameshuhudia mambo mazuri akiwafanyia katika uongozi wake, ambao utafikia tamati baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
"Pia TASWA inaishukuru Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa ushirikiano mkubwa iliotoa kuhakikisha tukio hilo linafanikiwa. Tayari wadhamini mbalimbali wamejitokeza kusaidia na tunaomba wengine watuunge mkono, ambapo Jumanne Oktoba 15, TASWA itafanya mkutano na waandishi wa habari kutangaza mdhamini mshiriki mmoja, mkutano utakaofanyika ukumbi wa City Sports Lounge, Dar es Salaam,".
TASWA imeona umuhimu wa wanamichezo kuagana na Rais Kikwete na kumpa tuzo kutokana na masuala mbalimbali aliyofanya kwa miaka yake 10 katika kusaidia kukuza michezo na sanaa hapa nchini.
Miongoni mwa mambo hayo ni serikali yake ilivyolipia makocha wa michezo ya soka, netiboli na ngumi na pia serikali ilipeleka wanariadha wetu China, Ethiopia na New Zealand kwa maandalizi ya mashindano ya kimataifa.
Pia tutamkumbuka Rais Kikwete kwa uamuzi wa kurejesha michezo shuleni pamoja na mashindano ya michezo kwa shule za msingi na sekondari (UMISHUMTA na UMISETA).
Yapo mambo mengi ambayo tukiyataja yote aliyofanya kuhusu michezo yatachukua nafasi kubwa, hivyo tuna kila sababu wanamichezo kujitokeza na kuagana na Rais wetu.

waliotembelea blog