Saturday, September 12, 2015


CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kitatoa tuzo kwa Rais Jakaya Kikwete pamoja na wanamichezo 10 waliofanya vizuri zaidi katika miaka 10 akiwa Rais wa Tanzania.
Taarifa ya Mweyekiti wa TASWA, Juma Abbas Pinto imesema kwamba tukio hilo ambalo pia litahudhuriwa na Rais Kikwete, litafanyika Oktoba 8, mwaka huu ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam likiwa na lengo la wanamichezo kumuaga Rais Jakaya Kikwete.
Pinto amesema TASWA itakabidhi tuzo maalum kwa Rais ikiwa ni kuthamini mchango wake kwa maendeleo ya michezo wakati wa miaka 10 ya uongozi wake na imebariki tukio hilo kama  ‘JK na Wanamichezo’.

Rais Jakaya Kikwete akikata utepe wa jengo la studio za Azam FC wakati wa uzinduzi Machi 6, mwaka huu. Kulia ni Mwenyekiti wa makampuni ya Bakhresa Group, wamiliki wa Azam Media Limite, ambao ndiyo wamiliki wa Azam TV, Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na kushoto ni Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara.

Amesema licha ya kutoa tuzo kwa Rais na wanamichezo 10 waliofanya vizuri zaidi, pia TASWA itatoa vyeti maalum kwa kampuni mbalimbali zilizosaidia kwa kiasi kikubwa kudhamini michezo katika miaka 10 ya Rais Kikwete.
Amesema maandalizi muhimu yamekamilika kuhusiana na tukio hilo, ambapo wawakilishi kutoka vyama vyote vya michezo hapa nchini pamoja na wanamichezo wataalikwa kuhudhuria tukio hilo la kihistoria.
Amesema TASWA inamshukuru Rais Kikwete kwa kukubali kujumuika nao siku hiyo ili kuagana na wanamichezo, ambao wameshuhudia mambo mazuri akiwafanyia katika uongozi wake, ambao utafikia tamati baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
"Pia TASWA inaishukuru Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa ushirikiano mkubwa iliotoa kuhakikisha tukio hilo linafanikiwa. Tayari wadhamini mbalimbali wamejitokeza kusaidia na tunaomba wengine watuunge mkono, ambapo Jumanne Oktoba 15, TASWA itafanya mkutano na waandishi wa habari kutangaza mdhamini mshiriki mmoja, mkutano utakaofanyika ukumbi wa City Sports Lounge, Dar es Salaam,".
TASWA imeona umuhimu wa wanamichezo kuagana na Rais Kikwete na kumpa tuzo kutokana na masuala mbalimbali aliyofanya kwa miaka yake 10 katika kusaidia kukuza michezo na sanaa hapa nchini.
Miongoni mwa mambo hayo ni serikali yake ilivyolipia makocha wa michezo ya soka, netiboli na ngumi na pia serikali ilipeleka wanariadha wetu China, Ethiopia na New Zealand kwa maandalizi ya mashindano ya kimataifa.
Pia tutamkumbuka Rais Kikwete kwa uamuzi wa kurejesha michezo shuleni pamoja na mashindano ya michezo kwa shule za msingi na sekondari (UMISHUMTA na UMISETA).
Yapo mambo mengi ambayo tukiyataja yote aliyofanya kuhusu michezo yatachukua nafasi kubwa, hivyo tuna kila sababu wanamichezo kujitokeza na kuagana na Rais wetu.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog