WAKATI
zoezi la upigaji kura kuchagua, mgeni rasmi, waimbaji na mikoa
itakayofanyika tamasha la Pasaka mwaka huu, baadhi ya mameneja wa
viwanja vya michezo hapa nchini wamelizungumzia tamasha hilo kwamba
ingekuwa vema lingefanyika kwenye mikoa yao.
Kwa
kutambua umuhimu wa waumini, mashabiki na wadau wa nyimbo za Injili
hapa nchini, Kampuni ya Msama Promotions kupitia Mkurugenzi wake, Alex
Msama imeyakabidhi masuala hayo mikononi mwa wadau hao ambao ndio
watachagua wanachokitaka katika tamasha hilo la kumuimbia na kumtukuza
Mungu kupitia waimbaji mbalimbali.
Msama
amendelea kuwakumbusha watanzania namna ya kuwapigia kura waimbaji,
mgeni rasmi na mikoa ambako ukitaka kumpigia mwimbaji andika Pasaka acha
nafasi kisha andika jina la mwimbaji unatuma kwenda namba 15327.
Pia
kwa mgeni rasmi andika neno Pasaka acha nafasi kisha andika jina la
mgeni rasmi unayetaka kumpigia kura tuma kwenda15327, wakati mikoa
unaandika Pasaka acha nafasi jina la mkoa unaotaka kuupigia kura tuma
kwenda namba 15327 piga kura uwezavyo ili upate mwimbaji na mgeni rasmi
na mkoa unaopenda tamasha lifanyike.
Aidha
Msama alitoa wito kwa mashabiki kupiga kura kwa wingi kuchagua maeneo
hayo matatu yatakayofanikisha tamasha hilo, kwani litafanikiwa baada ya
wao kufanya hivyo.
Meneja
wa uwanja wa Majimaji, ambaye ni Katibu Msaidizi wa Chama cha Mapinduzi
(CCM) Mkoa wa Ruvuma, Nebret Mwinisongole anasema Pasaka ni sikukuu
ambayo inaelezea jinsi mkombozi wetu Yesu Kristo alivyoshinda mateso na
kueleza kwamba tuendelee kuwa na imani naye kupitia sikukuu hiyo.
Mwinisongole
anasema Watanzania waendelee kudumisha amani ya nchi ambayo tumepewa
na Mungu ambayo inatakiwa idumishwe zaidi na viongozi waliopo.
Katibu
huyo alifika mbali zaidi kwa kueleza kwamba, Mkoa wa Ruvuma ndio mkoa
unaoongoza kwa kuzalisha chakula kingi hapa nchini, hivyo kwa neema hiyo
wanawakaribisha waimbaji mbalimbali wa Kimataifa mkoani kwao kujionea
vivutio vilivyoko mkoani humo.
“Mashabiki
wa muziki wa Injili waje kwa wingi kusikiliza maneno ya Mungu kupitia
waimbaji mbalimbali watakaokuwepo kwenye tamasha hilo,” alisema
Mwinisongole.
Meneja
wa uwanja wa Samora mkoani Iringa, Lazaro Manila anasema mashabiki wa
Mkoa wa Iringa kupiga kura kwa wingi ili mkoa huo upate nafasi ya
Tamasha hilo kufanyika mkoani humo.
Manila
anasema iwapo, Iringa watapata nafasi ya kuchaguliwa kufanyika kwa
tamasha hilo mkoani kwao itasaidia kuongeza chachu ya waimbaji wazawa
kuongeza juhudi za kufikia walipo wenzetu waliopiga hatua.
Meneja
wa uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Rich Urio anasema matamasha
yanayoandaliwa na Msama Promotions ni bora na ni muhimu kwa sababu
yanazungumzia amani na kuongeza hofu ya Mungu.
Urio
anasema mkoa wa Dar es Salaam hasa uwanja wa Taifa ni eneo muhimu
ambalo linakusanya idadi kubwa ya waumini, hivyo anatoa wito kwa wakazi
wa mkoa huo kupiga kura kwa wingi kuuchagua mkoa huo.
Urio
anasema Msama afanikishe tamasha hilo katika mikoa mingi zaidi kwa siku
moja Jumapili ya Pasaka kwa sababu ndio siku muhimu duniani.
“Matamasha
yanayoandaliwa na Msama Promotions yana mvuto zaidi hasa
wanavyowashirikisha waimbaji kutoka nje kama Solly Mahlangu na
Ambassodors of Christ ambao wanafikisha neno la Mungu inavyotakiwa,”
alisema Urio.
Urio
anasema viingilio vinavyopangwa na kampuni hiyo ni sahihi kwa sababu
haviwaumizi waumini wanaohudhuria kwenye matamasha hayo.