BADO Mji wa Mafinga wilayani Mufindi mkoani hapa haujakaa sawa kufuatia
vifo vya watu 50 waliopoteza maisha kwa ajali ya kontena kudondokea Basi
la Majinja lenye namba za usajili T 438 CED iliyotokea Machi 11, 2015,
Uwazi limechimba.
Ajali hiyo ilitokea maeneo ya Changarawe mjini Mafinga ambapo kontena
hilo lilikuwa kwenye lori la mizigo la Scania lenye namba za usajili T
689 APJ mali ya Kampuni ya Cipex lililokuwa likitokea Dar kwenda Mbeya
huku basi hilo likitokea Mbeya kuelekea Dar.
KILICHOTOKEA BAADA YA AJALI
Kilichotokea
baada ya ajali hiyo ni kuonekana kwa Mkono wa Mungu ambapo mtoto
anayekadiriwa kuwa na umri wa mwaka mmoja mpaka miwili kunusurika katika
ajali hiyo huku watu 50 wakipoteza maisha.
“Mimi
naweza kusema ni Mkono wa Mungu kwa sababu, yule mtoto alikutwa
hajaumia popote lakini wazazi wake wakiwa wamepoteza maisha. Huoni kama
ni uwezo wa Mungu mwenyewe?” alisema askari polisi mmoja aliyekuwa
miongoni mwa waliokuwa wakisimamia zoezi la uokoaji.
WAZAZI WA MTOTO
Akisimulia
ilivyokuwa kwa wazazi wa mtoto huyo ambaye jina lake halijajulikana,
mmoja wa abiria walionusurika, Aidan alisema kuwa, kabla ya kuanza
safari jijini Mbeya, mtoto huyo alibebwa na mama yake akiwa ameongozana
na abiria wengine.
“Wazazi wa mtoto waliingia na kukaa siti ya tatu tu kutoka kwa dereva.
Hakuna aliyehisi kwamba mbele ya safari kuna janga kubwa kama hili.“Basi
lilianza safari, kila abiria alikuwa akizungumza na mwenzake, wengine
walikuwa wakiongea na simu. Wapo waliokuwa wakichati, nadhani ni wale
wanaotumia WhatsApp. Kumbe bwana shetani alikuwa anatembea na sisi,”
alisema abiria huyo akiwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Mufindi.
KABLA YA AJALI
Kwa
mujibu wa majeruhi mwingine wa ajali hiyo, baada ya kufika eneo la
Changarawe, kwa mbele lilionekana lori hilo likiwa katika mwendo wa
kawaida na hakuna aliyewaza kwamba litaangukia basi lao.
“Mbele
tuliliona lile lori likija, lakini mimi nimekuwa nikisafiri mara kwa
mara kwa kutumia barabara hiyo. Najua eneo hilo lina shimo lakini sikuwa
na wazo kwamba shimo lile litakuwa mtoa roho wa abiria wa basi letu.
“Wakati
tunapishana sasa, lori linapita kulia kwetu, mimi nilikaa siti ya nyuma
upande wa abiria. Ghafla nilishtuka kuona kama giza linatanda upande wa
dereva, mara nikasikia watu wakianza kulia.
“Kabla sijajua ni nini, nikasikia kishindo kikuu. Puuu! Abiria wengine
walisikika wakisema wanakufa, wengine wakiwa kimya! Ndipo nikajua
tumeangukiwa na kontena lakini sikuweza kufuatilia ilikuaje kwani akili
zikawa kama zimeniruka,” alisema abiria huyo bila kutaja jina lake.
KILICHOMTOKEA MTOTO HUYO
Baadhi
ya waokoaji waliofika mapema mara baada ya ajali hiyo waliliambia Uwazi
kwamba, wakati wanahangaika kuitoa miili ya majeruhi na marehemu,
walishangaa kumkuta mtoto huyo akiwa chini ya siti ya nyuma kabisa
maarufu kwa jina la ‘kwa balozi’, akiwa hana michubuko.
“Baadhi ya abiria walionusurika wakatuambia huyu mtoto alikaa na wazazi
wake kwenye siti ya tatu kutoka kwa dereva. Sasa amefikaje kule nyuma
kwa balozi? Nadhani anayejua ni Mungu.“Unajua watoto wadogo wana mkono
unaowalinda. Mara nyingi katika ajali wao wanasalimika kwa njia ya ajabu
sana,” alisema askari mmoja wakati wa uokoaji.
Picha ya mtoto huyo ilipigwa na mpiga picha Francis Godwin kwenye Wadi
Namba 3 kwa kusaidiwa maelekezo na polisi wa kike na muuguzi mmoja
aliyekuwa na orodha ya watu walionusurika. Watu wengine wawili kitandani
hapo walikuwa ni wasamaria wema waliokuwa wakimsaidia mtoto huyo ambapo
wazazi wake wanasadikiwa walipoteza maisha.
Polisi wakiwa eneo la tukio.
MGANGA MKUU NA MKUU WA MKOA
Juzi,
Uwazi lilizungumza na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Salimin Mahimbo
kuhusu ajali hiyo ambapo alisema mpaka sasa, majeruhi waliolazwa ni saba
baada ya mmoja kufariki dunia na majeruhi mwingine kupelekwa Hospitali
ya Taifa Muhimbili (MNH) kutokana na hali yake kuzidi kuwa mbaya.
“Mpaka sasa tuna majeruhi saba tu, mmoja alifariki dunia. Mmoja
amekimbizwa Muhimbili kwa matibabu zaidi, hali yake si nzuri, hawa saba
wanaendelea vizuri,” alisema Mahimbo.Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina
Masenza alisema mpaka juzi, marehemu wote walishatambuliwa na ndugu zao
na waliolazwa wametambuliwa pia.