Tuesday, September 23, 2014



Warembo 15 kati ya 30 wanaoshiriki shindano la Redds Miss Tanzania 2014 wakisindikizwa na mkali wa Bongo Fleva kutoka Jijini Dar es Salaam, Tunda Man, wametoa burudani kali wakati wa shindano dogo la awali la kumtafuta mrembo mwenye kipaji lililofanyika Babati Mkoani Manyara. Pichani juu ni washindi wa tano waliofanikiwa kuingia fainali ya shindano hilo la vipaji litakalofanyika jijini Dar es Salaam baada ya wengine 15 kufanyika Arusha mjini.


Warembo hao walishindana vikali katika kucheza na kuimba miziki ya aina mbalimbali.

Jopo la majaji likifuatilia kwa makini shindano hilo



Kila aina ya stile za uchezaji zilioneshwa na warembo hao jukwaani...

Warembo wenzao waliobakia wakishangilia burudani ya vipaji kutoka kwa washiriki wenzao.

wadau wa sanaa ya Urembo Babati wakifuatilia shindano hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Christina Mndeme aliye mwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Manyara, akiwa na waratibu wa show hiyo, Mzee Ally Sumaye (kushoto) na Mfanyabiashara Mohamad Bajwa.

Msanii wa Bongo Fleva Tunda Man akitoa burudani kwa wadau wa urembo Babati.


Tunda Man aliburudisha vilivyo ukumbini hapo.

Ilikuwa ni shwangwe kwa warembo hao ambao wapo Mikoa yua Kaskazini kwa ziara ya kimafunzo katika hifadhi za Taifa.


Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
MBEYA City fc imepata pigo baada ya wachezaji wake watatu kuumia katika mechi ya jumamosi iliyopita dhidi ya JKT Ruvu  iliyomalizika kwa suluhu ya bila kufungana, uwanja wa Sokoine, Mbeya, na watakaa nje ya uwanja kwa wiki mbili.
Afisa habari wa klabu hiyo, Dismas Ten ameiambia MPENJA BLOG mchana huo kuwa baada ya mechi iliyopita, wachezaji watano walipata majeruhi, lakini wawili kati yao watarejea uwanjani jumamosi ya septemba 27 kuchuana na Coastal Union.
“Kwanza nianze na majeruhi; baada ya mechi kumalizika jumamosi iliyopita, kuna wachezaji wetu watano walipata majeraha, lakini wawili kati yao watarejea jumamosi  ijayo kucheza dhidi ya Coastal Union kwasababu maumivu yao hayakuwa makubwa sana. Wachezaji hao ni beki Deogratius Julius ‘Musafwa wa Kweli’ na kiungo mahiri, Steven Mazanda.” Alisema Dismas.
“Wachezaji wengine watatu kwa maana ya John Kabanda, Alex Seth na Eric Mawala, hawataweza kucheza kabisa siku ya jumamosi kwasababu watakaa nje kwa majuma mawili, kwa mujibu wa daktari wetu.”
Dismas aliongeza kuwa maandalizi ya mechi ya pili nyumbani yanakwenda vizuri na wachezaji wana morali ya kutafuta ushindi na kuendeleza rekodi yao ya msimu uliopita ambapo walimaliza katika nafasi ya tatu nyuma ya Yanga na mabingwa Azam fc.
“Hali ya kambi ni nzuri, tunajiandaa vizuri na tunaamini tutaibuka na ushindi. Tulicheza mpira mkubwa sana dhidi ya JKT Ruvu, sema wakati mwingine demokrasia ya mpira wa miguu inabidi tukubaliane nayo”
“Kuna kushinda, kushindwa na kutoa sare, lakini mwisho wa siku tulicheza mpira mzuri na watu waliokuwepo uwanjani waliridhika na kiwango cha timu”

“Tunataka kulipa kisasi, Coastal walitufunga na kutuharibia rekodi yetu. Tunataka kuonesha kwamba kutufunga kwao sio kwamba tulikuwa chini ya kiwango bali walitubahatisha tu”


Na Baraka Mpenja, Dar esl salaam
IMEELEZWA kuwa mshambuliaji wa Simba sc, Mkenya Paul Kiongera Mungai leo amefanyiwa vipimo hospitali ya Taifa ya Muhimbili kufuatia kuumia goti katika sare ya 2-2 dhidi ya Coastal Union, jumapili iliyopita uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Katika vipimo vya awali, Kiongera amebainika kuwa na majeruhi sugu ya goti kama ilivyowahi kuelezwa na mtandao huu siku za nyuma.
Kiongera anayekonga nyoyo za mashabiki wa Simba alitokea benchi katika dakika ya 67 dhidi ya Wagosi wa Kaya, lakini dakika mbili kabla ya mechi kuisha alitonesha goti lake kwa kugongana na kipa Shaaban Hassan Kado, hivyo kulazimika kumpisha Amri Kiemba.
Baada ya kuumia, Kiongera alionekana kubadilika katika lugha yake ya mwili ‘Body Language’ akionesha kuwa ameumia sana na hataweza kurudi uwanjani kirahisi.
Kabla ya kusajiliwa majira ya kiangazi mwaka huu, ripoti zilifafanua kuwa Kiongera ana majeruhi ya muda mrefu aliyopata wakati anacheza Kenya, lakini kutokana na Simba kukosa mfumo wa kupima afya za wachezaji kabla ya kuwasajili walijikuta wakimsainisha mkataba akiwa na ‘pancha’.
Imefahamika kuwa Kiongera anaweza kuwa nje ya uwanja kwa wiki sita au miezi miwili na litakuwa pigo kwa Wanamsimbazi wanaovutiwa na uchezaji wa Mkenya huyo.
Kwa maana hiyo Oktoba 12 mwaka huu kuna uwezekano mkubwa nyota huyo akautazama mpambano wa watani wa jadi, Simba na Yanga akiwa jukwaani na kuwaacha mashabiki wa Simba wakisikitika.
Mbali na Kiongera, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ ni majeruhi pia, wakati Haruna Chanongo aliyeumia kwenye mechi dhidi ya Coastal Union anaweza kurudi uwanjani muda wowote.
Wakati huo huo, Kiungo wa ulinzi aliyekaa nje ya uwanja kwa muda mrefu sasa, Jonas Mkude ameimarika kiasi cha kusubiri maamuzi ya kocha Patrick Phiri kumpanga katika mechi ijayo dhidi Polisi Morogoro, Septemba 27 mwaka huu uwanja wa Taifa, Dar es salaam.
Mkude hajawahi kucheza chini ya kocha Phiri wala kufanya mazoezi, kwahiyo Mzambia huyo ndiye mwenye maamuzi ya kumpanga au kumpa mazoezi maalumu ili kuimarika zaidi.
Mechi iliyopita, Piere Kwizera alicheza nafasi ya Mkude, lakini alionekana kutoimudu kwa asilimia kubwa na alikosa maamuzi sahihi hasa katika upigaji wa pasi.

Alikuwa anachelewa kuanzisha ‘Movement’ pale inapobidi na alikuwa anapiga pasi vizuri bila kukosea -kukosea, lakini nyingi hazikuwa na madhara kwa Coastal Union.


Aliyekuwa Rais wa TFF, Leodigar Chila Tenga alikuwa mchezaji muhimu wa Taifa Stars miaka ya 1980
HISTORIA inaonesha kuwa zamani mpira wa miguu ulikuwa unachezwa kutoka ngazi ya chini mpaka juu na walipatikana wachezaji wengi wa kulisaidia taifa.
Taifa Stars iliyoshiriki michuano ya mataifa ya Afrika nchini Nigeria miaka ya 1980, ni ushahidi tosha juu ya suala hilo.
Katika kipindi hicho kisichosahaulika miongoni mwa wadau wengi wa soka nchini, wachezaji waliounda Taifa  Stars walitoka timu mbalimbali za chini na za juu. Klabu kubwa za Simba na Yanga hazikutoa wachezaji wake kwa asilimia kubwa.
Leo hii klabu moja inakuwa na wachezaji 6, 8 mpaka 10 katika kikosi cha Taifa Stars. Zamani haikuwa hivi, Simba na Yanga miaka ya 80 wakati Stars ikiifunga Kenya, Harambee Stars 5-0 zilitoa wachezaji wanne tu (kila timu wawili).
Hii ilitokana na kuwepo wachezaji wengi sana. Makocha wa Stars walikuwa na wigo mpana wa kuteua wachezaji kutoka klabu mbalimbali hadi za daraja la pili. Mashindano yalikuwa mengi mno kuanzia chini na mpira ulipigwa kila kona ya nchi.
Leo hii mambo ni tofauti kabisa, mpira hauchezwi kwa misingi mizuri. Hakuna mashindano  mengi maalumu. Taifa Stars inategemea wachezaji kutoka Yanga, Simba na Azam fc.
Kutokana na mazingira hayo, wachezaji wamebaki walewale kila siku. Leo hii kocha wa Stars, Mart Nooij akimuacha Mrisho Ngassa, unadhani ni mchezaji gani mwenye kiwango cha juu atabadili nafasi yake?
Nani anaweza kurithi vizuri nafasi ya Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbwana Samatta au Thomas Ulimwengu? Makocha wamejikuta hawana machaguo kwasababu ndio wachezaji waliopo katika kiwango cha juu kwasasa.
Taifa Stars enzi hizo ilikuwa moto wa kuotea mbali

Kocha amekosa wigo mpana wa kuchagua wachezaji wa Stars, lakini zamani kocha alikuwa anaamua mwenyewe amchukue mchezaji wa aina gani na haikuwa lazima kuzifikiria Simba na Yanga .
Ukweli ni kwamba wachezaji wengi ambao waliibuka na kuwa  nyota wa Tanzania walitoka ligi za mchangani.
Ligi hizi zilikuwa na ushindani na hamasa kubwa, kwahiyo Dr Mwaka Sports Xtra Ndondo Cup inajaribu kurudisha hali hiyo na kutoa fursa kwa vipaji vingi vilivyopo mtaani na kuvipatia jukwaa la kuonekana.
Haya sio mawazo mpya, tayari yalishafanyika huko nyuma, lakini michuano hii inakuja kwa ‘staili’ nyingine ya kileo na itatangazwa.
Wachezaji bora wa mashindano watapatikana na kutafutiwa njia ya kuweza kuwaendeleza.
Pia lengo ni kuzitengenezea klabu kubwa sehemu ya kutafuta wachezaji wapya kuliko kusajili hovyo hovyo. Kwasasa hakuna wigo mpana wa kusajili wachezaji, hivyo michuano hii inataka kuibua vipaji vingi vilivyopo mitaani.
Kwa mfano Mtibwa Sugar kila mwaka inauza wachezaji, lakini bado inaendelea kuwepo na kutafuta vipaji vipya kutoka mchangani. Wachezaji wapo wengi, lakini hakuna mashindano.
Kutokana na mazingira haya, Sports Xtra ya Clouds fm imeamua kuanzisha mashindano yanayokwenda kwa jina la DR MWAKA SPORTS XTRA NDONDO CUP.
Banner Ads Top
Michuano hii itakayoendeshwa kwa mfumo wa kisasa kabisa itashirikisha wachezaji wa mchangani kutoka timu 32.
Kivumbi kinatarajia kuanza  Septemba 27 mwaka huu ambapo mechi ya ufunguzi itawakutanisha  Friend’s Rangers na Kiluvya United katika uwanja wa Makulumla, Magomeni, Dar es salaam, majira ya saa 10:00 jioni.
Mbali na dimba la Makulumla, viwanja vingine vitakavyotumika katika mashindano hayo ni Kinesi (Shekilango), Benjamini Mkapa (Ilala) na Mizinga (Kigamboni).
Timu 32 zitakazoshiriki zimepangwa katika makundi nane yenye timu nne.
Kundi A: Boom fc, Beira Hotspurs, Tabata fc na Tuamoyo
Kund B: Sifa Politani, Vijana Ilala, Kijichi, Micco Villa
Kundi C: Friend’s Rangers, Temeke Market, Kiluvya United na Muheza fc
Kundi D: Ukonga United, Sinza Stars, Congo Shooting na Snow White
Kundi E: Zakhem, Black Six, TP Same na Makumba
Kundi F: Villa Squad, Scud fc, Nyota Afrika na Burudani fc
Kundi H: Stakishari fc, Abajalo, Shelaton na Kimara United


SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) septemba 19 mwaka huu lilitangaza kupokea kwa masikitiko makubwa taarifa zilizoandikwa kwenye baadhi ya Vyombo vya Habari zikielezea tuhuma za hujuma kwa timu ya Taifa (Taifa Stars) katika mechi za kufuzu mashindano ya AFCON.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa TFF pamoja na kutokuwa na uthibitisho wa tuhuma hizi nzito haliwezi kuzikalia kimya na litateua jopo la kuchunguza.
TFF alieleza kuwa wanafamilia wa mpira wa miguu Tanzania (Members of TFF Family) watakaohitajika kuhojiwa na jopo hilo kwa mujibu wa Ibara ya 37 ya Kanuni za Maadili za TFF watalazimika kutoa ushirikiano. Atakayeshindwa kutoa ushirikiano atachukuliwa hatua za kimaadili.
 Pia wadau wa mpira wa miguu ambao sio wanafamilia wa TFF, watakaoitwa na jopo hili wanaombwa watoe ushirikiano kwa nia ya kujenga mpira wetu.
Kufanya vibaya kwa timu ya taifa, TFF wasitafute watu wa kuwabebesha lawama kutokana na mambo ya kimjini tuliyoyazoea.
Kwasisi ambao ni wakazi wa Dar es salaam kuna mambo mengi yanazungumzwa, lakini haya ni maneno tu kwa ajili ya kusherehesha vikao, vijiwe vya kahawa na majungu.
Sababu kubwa ya mambo haya kuzungumzwa ni matatizo yanayolikabili soka la nchi hii. Tukubali tukatae, kadri siku zinavyokwenda mbele, mpira wa Tanzania unazidi kudidimia kila kukicha.
yangaa
Jumamosi iliyopita katika mechi ya ufunguzi wa ligi kuu soka Tanzania bara baina ya Mtibwa Sugar dhidi ya Yanga iliyopigwa uwanja wa Jamhuri Morogoro, Wanajangwani walikufa 2-0.
Yanga ilikuwa na wachezaji sita wa timu ya Taifa ambao ni Deogratius Munishi ‘Dida’, Oscar Joshua, Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mrisho Ngassa na Saimon Msuva pamoja na wachezaji wanne wa kimataifa ambao ni Mbuyu Twite Jr, Geilson Santos Santana ‘Jaja’ , Haruna Niyonzima na Hamis Kiiza.
Yanga ikiwa na wachezaji sita wa timu ya Taifa na wanne wa kimataifa alicheza dhidi ya Mtibwa Sugar ambayo haina hata mchezaji mmoja wa timu ya Taifa wala wa kimataifa na ikaambulia kipigo hicho.
Miaka ya 1980 wakati wengi wetu walikuwa wanazaliwa na wengine wanakua mpira ulikuwa unachezwa kwa kiwango cha juu, lakini kutokana na teknolojia kutokuwa rafiki miaka hiyo, tumejikuta tukihadithiwa tu na hakuna DVD za kuona matukio ya zamani.
Tumehadithiwa na wazee wetu na kusoma vitabu vilivyotangulia. Nakumbuka nilipata nafasi ya kukaa na mzee mmoja wa Morogoro, Mohamed Msomari ambaye alikuwa mchezaji wa zamani wa Cosmo, kocha aliyeingoza Pan Africa kuchukua ubingwa mwaka 1982 na kocha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Huyu ndiye kocha aliyeibua kipaji cha mchezaji hatari wa wakati ule, Zamoyoni Mogela.
Msomari aliniambia kwamba katika miaka ya 1980, timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars iliifunga timu ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars mabao 5-0.
Kikosi hicho cha Stars kilikuwa na wachezaji wawili tu kutoka Simba na wawili kutoka Yanga tofauti na ilivyo sasa hivi.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi

Timu ya wakati ule,  mchango wa wachezaji wa Simba na Yanga ulikuwa mdogo mno na wengi walitoka timu za madaraja ya chini. Kwa mfano; Leopard Taso Mukebezi alikuwa anacheza timu ya Balimi ya Bukoba iliyokuwa daraja la pili. Kiungo Idrissa Ngulungu alitoka Tumbaku ya Morogoro, Peter Tino kutoka African Sport ya Tanga,  Leodigar Chila Tenga,  Jela Mtagwa, Adolf Rishard walitoka Pan Africa.
Miaka hiyo ya 80 Simba ilikuwa moto wa kuotea mbali, ilikuwa ni kali kwelikweli ikiwa na wachezaji kama Nico Njohole, Abdallah Mwinyimkuu maarufu kama British, Mohamed Tall, Ezekiel Greyson ‘Juju Man’, Jumanne Hassan Masimenti.
Wachezaji hawa pamoja na ukali wao na kuichezea Simba ambayo ilikuwa kwenye kiwango cha hatari na Taifa Stars ikiitandika Kenya 5-0, hawakupata nafasi ya kuitwa, licha ya kwamba waliwahi kuichezea siku za nyuma.
Nafasi zilichukuliwa na wachezaji kutoka timu hadi za madaraja ya pili kutoka mikoani. Maana yake kulikuwa na ushindani mkubwa, wachezaji walikuwa wengi na haikuwa rahisi kuteuliwa Taifa Stars.
Leo hatuoni wachezaji kutoka kila kona ya Tanzania. Kuna tatizo sehemu fulani na hapo ndipo tunatakiwa kutumia muda mwingi kutafuta sababu  na suluhisho sahihi.
Kwa mfano ligi iliyoanza mwishoni mwa wiki iliyopita ndio moja kati ya kaburi la timu ya Taifa ya Tanzania. Haizalishi wachezaji wa kutosha, haina ushindani na kwa maana hiyo ni ndoto kuwa na Taifa Stars bora.
Badala ya Rais wa TFF, Jamal Emil Malinzi kupoteza muda kutafuta watu wanaoihujumu timu ya Taifa, inatakiwa apoteze muda mwingi kutafuta muundo bora na chombo huru cha kuendesha ligi katika uweledi wa hali ya juu.
Ligi ikishakuwa bora na ushindani kuwa mkubwa, itasababisha kujenga wigo mpana wa kuchagua wachezaji wa timu ya Taifa. Kwa kifupi,  ligi yetu ni mbovu, haivutii, haitoi wachezaji bora, sasa tujiulize, tutapata wapi timu ya Taifa iliyo bora?
Kuchunguza hujuma kwa Taifa Stars inayofanya vibaya hakuna maana, lazima tukubali kuwa hatuna mfumo wa kuzalisha wachezaji ambao wako tayari kushindana na wachezaji wa mataifa mengine.
Nimeeleza kuwa zamani walikuwa wanateuliwa wachezaji kutoka daraja la pili kuliko wanaocheza Simba na Yanga. Sababu ni kwamba mpira ulikuwa unachezwa mno na wachezaji walikuwa wengi mchangani.
Siku hizi hakuna wachezaji kabisa, na ndio maana unakuta wachezaji wengi wa timu ya Taifa wanatoka klabu za Simba, Yanga na sasa hivi Azam fc.
Siku hizi mashabiki wanakwenda uwanjani kupoteza muda, kubadili fikra, kuonana na watu tofauti waliopoteana kwa muda mrefu. Ladha ya mpira haipo uwanjani, na watu wanaenda kwa mazoea tu.
Suluhisho ni kurudi nyuma, kukaa pamoja na kuunda mpango mkakati wa kitaifa ili kuboresha soka letu kuanzia ngazi za chini mpaka juu.
Utengenezwe mfumo wa kuibua, kulea na kukuza vipaji kuanzia ngazi ya chini ili kupata wachezaji wengi wa timu Taifa kama ilivyokuwa miaka ya 1980.
TFF itafute njia za kuboresha ligi kuu na kuunda chombo bora cha kusimamia na kusiwepo kubebana wala kuoneana aibu. Vinginevyo hatutafanikiwa hata siku moja na tutaendelea kutiana moyo, kushikana uchawi na kuwekeana ahadi hewa.

Tatizo la Taifa stars sio kuhujumiwa, ni kukosa njia sahihi ya kutafuta wachezaji na sababu ni ubovu wa ligi, haina uwezo wa kutupatia vipaji mbalimbali.

waliotembelea blog