Hali ya wasiwasi imekumba jimbo la Crimea.
Rais
Obama ametangaza mapendekezo ambayo huenda yakatoa suluhu kwa mzozo wa
Ukraine, ikiwemo kuwatuma wachunguzi wa kimataifa na kuanzishwa
mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Moscow na serikali mpya mjini Kiev.
Bwana Obama amejadili swala hilo kwa njia ya simu na chanzela wa Ujerumani, Angela Merkel.
Wachunguzi
hao watalenga kulinda haki za watu wa kabila la Urusi waliopo katika
jimbo la Crimea; na kwa upande wake Urusi itahitajika kuwaondoa
wanajeshi wake katika jimbo hilo. Pendekezo hilo huenda likajadiliwa
pembezoni mwa mkutano utakaofanyika nchini Ufaransa (Jumatano) ambao
utawaleta pamoja wajumbe kutoka Marekani, Urusi na kwingineko kwa ajili
ya kuijadili Lebanon.
Hapo
awali waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Marekani John Kerry,
amelaani kile amekitaja kuwa kitendo cha uchukozi kutoka Urusi dhidi ya
Ukraine. Wakati wa ziara yake mjini Kiev ambapo aliweka shada la maua
kuwakumbuka waandamanaji waliouwawa mwezi uliopita, bwana Kerry
ameshutumu Moscow kwa kutumia uongo na vitisho kuficha ukweli.
Mwandishi
wa BBC Sarah Reinsford aliyepo mjini Kiev amesema kuwa wakati akiweka
shada la maua katika maeneo walikouwawa mamia ya waandamanaji mjini
humo, John Kerry alikaribishwa na umati wa watu waliokuwa wakiomba
msaada wa marekani.
Na hilo
ndilo lililomleta hapa; kutoa msaada wa hali na mali na pia wa kisiasa
kwa serikali ya mpito ya Ukraine, na pia ahadi ya msaada wa kifedha na
wa kiufundi kusaidia katika kuimarisha uchumi, amesema mwandishi wetu.
Rais Putin.
Lakini zaidi ya yote bwana Kerry ameleta ujumbe kwa Moscow.
" Nadhani
ni bayana kwamba Urusi imekuwa ikifanya bidii kubuni dhana ya
kuiwezesha kutekeleza uvamizi zaidi. Urusi imezungumzia raia wachache
wanaozungumza kirusi ambao wamezingirwa. Ukweli ni kwamba
hawajazingirwa! Ukweli ni kwamba serikali mpya ya Ukraine imewajibika
ipasavyo kwa kuhimiza utulivu na kujiepusha na uchokozi," amesema Bwana
Kerry.
Haukuna
ushahidi, amesisitiza, kwa madai ya urusi kwamba wanajeshi wake
wanalinda raia wanaozungumza lugha ya kirusi nchini Ukraine akiishutumu
moscow kwa kutumia uongo na vitisho kuficha ukweli.
Katika
karne ya ishirini na moja, bwana Kerry ameonya, haiwezekani kuvamia
taifa jingine na kisha kuamrisha matakwa yako yatekelezwe kwa kutumia
mtutu wa bunduki. Na kisha akamhimiza rais Putin kuwaondoa wanajeshi
wake katika jimbo la Crimea na kushughulikia malalamishi yake kupitia
njia za kisheria na amani.
Lau sivyo, ameonya, kwamba Urusi itakabiliwa na vikwazo zaidi vya kiuchumi na kisiasa.