Bingwa mara tatu Ujerumani na
bingwa mara mbili Argentina zitagombania dola milioni 35 kwenye mechi ya
fainali ya kombe la dunia Jumapili Julai tarehe 13 mjini Rio De
Janeiro.
Shirikisho la kimataifa Fifa limetoa jumla ya dola milioni 576 kushindaniwa kwenye mashindano ya mwaka huu nchini Brazil.
Mshindi ataweka kibindoni dola milioni 35 na wa pili $25 milioni, wa tatu $22milioni wa nne $20 milioni.
Timu nne zilizoondolewa kwenye robo-fainali
zitapokea $14 milioni kila mmoja, timu nane zilizong'olewa raundi ya
pili $9 milioni na timu 16 zilizoondolewa raundi ya kwanza $8 milioni
kila mmoja.
Ujerumani imefuzu kwa fainali baada ya kuiadhibu
Brazil mabao 7-1 na Argentina ikaiondoa Uholanzi mabao 4-2 ya penalti
mechi ya nusu-fainali. Kwa jumla timu 32 zimeshiriki mashindano ya mwaka
huu kwenye mechi 64 na wachezaji 736 wakajitosa uwanjani.
Miongoni mwa wachezaji nyota kwa upande wa
Ujerumani ni mfungaji bora zaidi kwenye mashindano haya Miroslav Klose
huku Argentina ikijivunia Lionel Messi mshindi wa tuzo la mchezaji bora
duniani mara nne.
Hii ni mara ya tatu Ujerumani na Argentina
wanakutana fainali ya kombe la dunia, mara ya kwanza ikiwa mwaka wa 1986
nchini Mexico Argentina ikashinda 3-2 kisha wakapatana tena mwaka wa
1990 nchini Italia na Ujerumani ikalipiza kisasi kwa kuinyoa Argentina
bao 1-0.
Wadadisi wengi wa kandanda wanasema Ujerumani
wana nafasi nzuri zaidi ya kuibuka mshindi kwani wameonyesha kiwango cha
juu zaidi ya Argentina kufikia sasa.
Lakini mpira unadunda hivyo basi Argentina nao
pia waeza kuibuka mshindi ikikumbukwa kwamba hamna timu ya bara Ulaya
imewahi kunyakua ubingwa wa dunia mashindano haya yakifanyika Marekani
Kusini.
Kwa jumla mataifa ya Marekani Kusini yameibuka
mshindi mara tisa kwenye kombe la dunia na ya Ulaya mara kumi Italia na
Ujerumani wakiongoza kwa kushinda mara tatu kila mmoja na Brazil ikiwa
juu Marekani Kusini kwa kushinda mara tano, Argentina na Uruguay mara
mbili kila mmoja.