Thursday, August 21, 2014


Na Adam Mbwana, Dar es salaam
Ilikuwa ni vita kali kati ya mafahali wawili ambao naweza kusema kila mmoja wao alikuwa na azimio tofauti kichwani mwake juu ya mwenzie. Vita hii huwezi kuifananisha na na zile za mwaka 1914 na 1939 ambazo ndio vita kubwa kuwahi kutokea duniani pale ambapo mataifa makubwa yalikuwa yalikuwa yakiwania utajiri kwa kutumia silaha kali na hatari duniani, lakini pia vita hii huwezi kuifananisha na ile maarufu ya miaka ya 1960 kati ya Urusi na Marekani wataalamu wakiita vita baridi ambayo haikutumia silaha kama sehem ya mapigano bali silaha ikitumika kama sababu kubwa ya vita hiyo
Lakini vita hii ni tofauti kabisa kwani inapiganwa katika mji ambao hauonekani kwa macho huku vyombo vya habari vikitujuza uwepo wake wakati wahusika wake wakuu wakiwa ni Romelo Lukaku na Josee Mourinho vita ambavyo havikuhitaji usuluhishi bali kuisha kwake kulihitaji mmoja wao akubali masharti ya mwenzake au kama si hivyo basi ilihitaji watu hawa kutengana kwa muda kama sio moja kwa moja.
Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho

Wahusika hawa walikuwa na mawazo tofauti vichwani mwao, Lukaku akihitaji kuhakikishiwa namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha Chelsea huku Mourinho naye akimtaka Lukaku apiganie nafasi yake katika timu mbele ya washambuliaji wengine kwenye timu kama Fernando Torres, Diego Costa na Didier Drogba. Na hapo ndipo vita iliponoga zaidi.
Tangu kusajiliwa kwake Chelsea August 2011 akitokea katika klabu ya Anderlecht ya Ubelgiji kwa paundi milion 17,  Romelo Lukaku ameshindwa kabisa kuonyesha uwezo mkubwa katika klabu hiyo ya Chelsea kama ambavyo wengi walitegemea.
 Wengi walidhania kuwa Lukaku ndiye atakuwa mrithi sahihi wa Didier Drogba katika safu ya ushambuliaji ya Chelsea kutokana na ukweli kwamba wawili hawa wanafanana sana kwa maumbo yao makubwa, staili ya kucheza kwa kutumia nguvu na hata kuwa na uwezo wa kuhimili beki zaidi ya mmoja. 
Diego Costa

Lakini hata hivyo mshambuliaji huyo mzaliwa wa Anrwerp nchinj Ubelgiji alimaliza msimu wake wa kwanza darajani akiwa mchezaji wa kikosi cha akiba.
Hali hiyo ilimfanya kupelekwa kwa mkopo msimu uliofuata wa mwaka 2012 katika timu ya Westbromwich Albiol ambapo aliweza kufunga magoli 17 na kumaliza katika nafasi ya sita ya wafungaji bora wa ligi kuu ya uingereza kwa msimu huo. Msimu uliofuata wa 2013-2014 alipelekwa tena kwa mkopo katika klabu ya Everton ambapo ambako nako alizifumania nyavu mara 15  katika mechi 31 alizocheza na kuisaidia Everton kumaliza katika nafasi ya 5 ya ligi huku akiwa na uwiano mzuri wa magoli zaidi ya washambuliaji wa chelsea Fernando Torres, Samuel Eto'o na Demba Ba ambao kwa pamoja waliweza kufunga magoli 19 tu.
Maneno yalianza kuibuka katika vyombo vya habari huku wachambuzi wa soka wakihoji nafasi ya Lukaku katika safu ya ushambuliaji ya Chelsea ambayo ilionekana kupwaya msimu uliopita chini ya kocha Josee Mourinho ambaye mara kwa mara alikuwa akiwalalamikia washambuliaji wake hao kwa kushindwa kuzifumania nyavu mara kwa mara.
Didier Drigbo amerudi Chelsea

Wachambuzi hao walimpa Lukaku sababu ya kuanza kudai nafasi ya kudumu katika kikosi cha Chelsea baada ya kumalizika kwa mkataba wake wa mkopo na Everton huku Mourinho akiweka pamba msikioni na kuendelea na mpango wake wa kumsajili mshambuliaji Diego Costa kutoka Atletico Madrid baada ya kuondoka kwa Samuel Eto'o na Demba Ba.
Kwa Lukaku hizi zilikuwa ni habari mbaya sana na ikawa ni moja ya sababu kubwa ya kuchochea vita kati yake na Mourinho kwani yeye alitegemea baada ya kuondoka kwa Etoo na Ba kungempa yeye nafasi ya kurudi kuchukua nafasi yake aliyokuwa akiisubiri kwa muda mrefu lakini badala yake akaletewa kipingamizi kingine ambaye ni Costa huku Mourinho akimpaka mafuta kwa mgongo wa chupa na kumwambia kuwa apiganie nafasi yake. Lakini kilichommaliza nguvu kabisa Lukaku na kurejea kwa Drogba klabuni hapo. Hapo ndipo Mourinho akamthibitishia Lukaku hakumuhitaji tangu mwanzo. Kwahiyo Lukaku alishuhudia makombora na vifaru vya kivita vikiingia kwenye ghala la silaha la Mourinho huku naye akishuhudia kwa macho yake.
Hatimaye Lukaku yakamshinda baada ya kuona adui yake hawezekaniki. Sasa ameamua kubwaga manyanga na kunyoosha mikono juu kama ishara ya kusalimu amri baada ya kukamilisha usajili wake wa kudumu katika klabu ya Everton wenye thamani inayotajwa kufikia paundi million 28.
Lakini suala la msingi la kujiuliza hapa ni Je, Mourinho alikuwa anataka nini cha ziada kutoka kwa Lukaku ili aweze kumpa nafasi? na Je, madai ya Mourinho kuwa Lukaku hakutaka kugombania nafasi kikosini ni ya kweli au ni kujisafisha tu mbele ya vyombo vya habari? na swali la mwisho ni Je, kwanini Torres abaki kikosini na kumuuza Lukaku ambaye msimu uliopita amefanya mambo makubwa zaidi ya Torres licha ya kuwa na umri mdogo?

Waswahili husema "funika kombe mwanaharamu apite". Hicho ndicho alichokifanya Lukaku baada ya kuamua kukubali kushindwa dhidi ya Mourinho. Ameamua kuanza maisha mapya Everton huku akimuacha Mourinho na pamba zake masikioni. Ama kweli asiyekubali kushindwa sio mshindani.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog