Tuesday, March 10, 2015

Freeman Mbowe akiongozana na viongozi wenzake kuelekea eneo la Mwakata wilayani Kahama



Mheshimiwa Freeman Mbowe akisalimiana na mkuu wa mkoa wa Shinyanga Ally Rufunga,wa kwanza kulia ni mkuu wa wilaya ya Kahama Benson Mpesya
Mheshimiwa Freeman Mbowe (mwenye miwani kushoto) na viongozi wengine wa CHADEMA Taifa wakijadiliana jambo kabla ya kukabidhi msaada kwa wahanga wa mvua kubwa ya mawe, kushoto kwa Mbowe ni mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga.

 
Sehemu ya umati wa wafuasi wa CHADEMA walioongozana na mwenyekiti wao wa Taifa Freeman Mbowe wakati wa kukabidhi msaada wa wahanga wa mvua ya mawe iliyosababisha vifo vya watu 47.
 
Mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja akijiandaa kukabidhi msaada wa fedha kwa niaba ya waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa.

Tafadhali pokea msaada huu kwa niaba ya mheshimiwa Edward Lowassa kwa ajili ya waathirika wote waliobomolewa nyumba zao kutokana na mvua kubwa ya mawe pamoja na rambirambi kwa waliofiwa na  jamaa zao, ndivyo anavyoeleza, Khamis Mgeja (kulia)


Maskini mtoto huyu hajui kitu gani kilichowasibu hadi kuwa katika hiyo ya maisha.

Haya ndiyo makazi ya muda kwa sasa kwa wakazi wa kijiji cha Mwakata Kahama - Shinyanga.
 
VIONGOZI wawili wa kisiasa nchini wameungana na watanzania wengine katika kuwapa pole na kuwafariji wahanga wa mvua kubwa ya mawe iliyonyesha na kubomoa nyumba kadhaa za wakazi wa kijiji cha Mwakata wilayani Kahama mkoani Shinyanga na kusababisha vifo vya watu 47 huku familia 450 zikibaki bila makazi.

Viongozi hao ni pamoja na mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa ambao kwa ujumla wao walikabidhi msaada wa fedha jumla ya shilingi milioni 15.
Akikabidhi msaada kwa niaba ya familia ya waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa, mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja alisema mara baada ya kutokea kwa maafa yaliyotokea, waziri mkuu mstaafu na familia yake waliguswa na tukio hilo na hivyo kuona umuhimu wa kuwasaidia wahanga wa maafa hayo.

“Mheshimiwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga na wakazi wote wa kijiji cha Mwakata, kwa niaba ya familia ya waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa, naomba nikabidhi msaada wa shilingi milioni tano kwa ajili ya wahanga waliokumbwa na tatizo hili ikiwa ni pole na rambirambi kwa familia ya watu waliopoteza maisha,”

“Binafsi yeye mwenyewe alikuwa aje lakini kutokana na majukumu aliyonayo ameniomba mimi mjumbe mwenzake wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) nifikishe salaam za pole na mchango wa kusaidia matatizo yaliyojitokeza hapa, pia ameniomba niwaeleze kuwa anaungana na watanzania wote kutoa pole zake za dhati kwa janga hili lililotokea,”

“Anasema yeye yuko pamoja nanyi na anaungana na watanzania wengine wote na kwamba janga hili siyo lenu peke yenu bali ni la watanzania wote na ameahidi kuendelea kushirikiana nanyi kwa hali na mali mpaka pale hali zenu zitakaporejea kuwa za kawaida, na pia anatoa pole kwa uongozi wa serikali mkoani Shinyanga,” alieleza Mgeja.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CHADEMA wa Taifa Freeman Mbowe mbali ya kukabidhi msaada wa shilingi milioni 10 kwa niaba ya chama chake aliwataka watanzania wote hasa viongozi wa CCM kutochanganya mambo ya siasa pale panapotokea janga lolote la kitaifa na kwamba tukio la Mwakata ni janga la Taifa.
Mbowe alisema kwa kawaida maafa yanapotokea hayana itikadi ya chama chochote cha siasa na kwamba si vizuri kwa viongozi wa vyama vya kisiasa kugeuza maafa ya kitaifa kuwa mashindano ya kisiasa na hakuna sababu yoyote ya kushindana kuona nani katoa zaidi katika kuwafariji wahanga.

“Ndugu zangu sisi CHADEMA tumeguswa sana kwa tukio hili, kwa hali hiyo tumeona tutoe kitu kidogo ili kuwasaidia wenzetu walioathiriwa na mvua hii kubwa, kwa sasa tutatoa shilingi milioni 10 ambazo hata hivyo tutaomba mtueleze ni vitu gani mnavyohitaji, kama ni vifaa au vyakula mtueleze,”

“Tunasema hivi kwa sababu tunaweza kuja na unga hapa kumbe kinachohitajika ni mafuta ya kula, au tukaja na maharagwe kumbe wengine wameishaleta ya kutosha na kinachohitajika ni mabati au mifuko ya saruji, hivyo baada ya msaada huu wa leo, tunatarajia kufanya mkutano mkubwa mjini Kahama kwa ajili ya kuchangia wahanga,” alieleza.

Akipokea misaada hiyo mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga aliwapongeza waziri mkuu mstaafu Lowassa na Mbowe kwa jinsi walivyoonesha kuguswa na tukio hilo na kwamba misaada waliyoitoa itasaidia kupunguza makali ya matatizo yaliyojitokeza baada ya mvua kubwa iliyoleta madhara kwa wakazi wa Mwakata.

“Kwa niaba ya mkoa wa Shinyanga tunawashukuru wote walionesha moyo wa upendo wa kuwasaidia wahanga hao, na kwa upande wa mheshimiwa Mbowe nikupongeze binafsi kwa jinsi ulivyoamua kuweka kando masuala ya kisiasa na kutanguliza mbele uzalendo, tunakushukuru sana, mpaka sasa tunaendelea kupokea misaada mbalimbali kwa ajili ya kaya 649 zilizoathiriwa na mvua hiyo,” alieleza Rufunga.

Mpaka Machi 9, mwaka huu idadi ya watu waliokufa kutokana na mvua kubwa ya mawe iliyopewa jina la Tornado iliyonyesha hivi karibuni ilifikia watu 47 baada ya majeruhi mwingine aliyekuwa amelazwa katika hospitali ya serikali mjini Kahama kufariki dunia juzi.  Majeruhi wanne walikuwa wakiendelea na matibabu katika hospitali rufaa ya Bugando jijini Mwanza.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog