Friday, July 18, 2014


Mbwana Samatta akishangilia moja ya goli aliloifungia Taifa Stars mechi za nyuma
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Julai 18, 2014, saa 9:00 asubuhi
TAIFA Stars chini ya kocha, Mholanzi, Mart Nooij, inakabiliwa na mechi muhimu dhidi ya Msumbiji `Black Mambas` , kuwania kupangwa hatua ya makundi kusaka tiketi ya kwenda kushiriki fainali za mataifa ya Afrika, AFCON , mwakani nchini Morocco.
Mechi hiyo ya kwanza itapigwa jumapili (julai 20 mwaka huu) ndani ya uwanja wa Taifa,  jijini Dar es salaam , ambapo Stars watalazimika kupata  ushindi wa mabao angalau 3-0 ili kujiweka mazingira mazuri ya kusonga mbele katika mechi ya marudiano itakayochezwa wiki mbili baadaye mjini Maputo nchini Msumbiji.
Kuelekea katika mechi hiyo ya jumapili, unaweza kusema kikosi cha Taifa Stars kipo kamili gado kwasababu nyota wake wote wa ndani na nje wapo tayari kwa kazi.
Mwinyi Kazimoto Mwitula alitua jana asubuhi akitokea nchini Qatar anakocheza soka la kulipwa tayari kwa kuongeza nguvu katika kikosi cha Stars.
Uzoefu wa Mwinyi katika soka la kimataifa utasaidia sana kuimarisha safu ya kiungo itakayomkosa Frank Domayo  `Chumvi` kwasababu ni majeruhi.
`Majembe` mawili ya Stars yanayokipiga TP Mazembe ya DR Congo, Mbwana Ally Samatta na Thomas Ulimwengu yapo nchini tangu juzi.
Kuelekea katika mechi hiyo, Mart Nooij ana wigo mpana wa kuamua nani aanze katika safu ya ushambuliaji.
Samatta amesema kwa upande wake, maandalizi ya mechi hiyo yamekamilika na amefurahi kwasababu ni mzima wa afya tofauti ni ilivyokuwa kwa mechi iliyopita mjini Harare nchini Zimbabwe.
“Maandilizi  kwa mimi kama mimi yako vizuri , kwasababu tulikuwa katika maandalizi ya ligi ya mabingwa, tulikuwa tunafanya mazoezi magumu. Kwahiyo maandalizi yako vizuri kwangu na kwa Thomas pia”. Alisema Samatta.
Thomas Emmanuel Ulimwengu
Ulimwengu kwa upande wake, kauli aliyoitoa jana jioni ni kwamba mechi ya jumapili itakuwa ngumu, lakini watajitahidi kupambana ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.
“Maandilizi ni mazuri, tumefanya mazoezi, tunaamini tutafanya kazi nzuri. Mechi itakuwa ngumu, lakini tutafanikiwa kwa umoja”.
“Tutafanya kazi, tuwaombe watanzania waje kwa wingi uwanjani, ushindi wa pili ni kwa upande wao”. Alisema Ulimwengu.
Mshindi wa jumla kati ya Tanzania na Msumbiji atakata tiketi ya kupangwa katika hatua ya mwisho ya makundu kutafuta safari ya Morocco.
Tanzania iliitoa Zimbabwe kwa kuifunga bao 1-0 uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam na kulazimisha sare ya mabao 2-2 mjini Harare.
Msumbiji wao waliifunga Sudan Kusini mabao 5-0 mjini Maputo na walipoenda ugenini walilazimisha suluhu ya bila kufungana.

Kila la kheri timu ya taifa ya Tanzania, Taifa stars kuelekea mechi muhimu na `Black Mambas`.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog