Thursday, July 24, 2014


KOCHA wa Yanga, Marcio Maximo amesema pamoja na kumpa mkataba wa miaka miwili mshambuliaji Geilson Santana Santos ‘Jaja’, bado anahitaji kuona uwezo wa washambuliaji wawili raia wa Uganda, Hamisi Kiiza na Emmanuel Okwi.
Yanga inalazimika kuachana na mchezaji mmoja wa kigeni kama kanuni za usajili zinavyoagiza, baada ya sasa kuwa na wachezaji sita wa kimataifa ambao ni Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite, Andrey Coutinho, Jaja, Kiiza na Okwi. Kanuni za usajili zinaruhusu timu kusajili wachezaji watano wa kigeni.
“Nalazimika kuwaona mazoezini Okwi na Kiiza ndiyo nitakuwa na jibu la kusema, lakini kwa sasa bado ni mapema mno kusema nitampunguza nani, kwa sababu hata katika rekodi za klabu naona wachezaji hawa wamekuwa na mchango mkubwa ndani ya timu ukitoa usumbufu ambao inasemekana wanao,” alisema Maximo.
Maximo alisema anaufahamu fika uwezo wa kiungo wa Rwanda, Niyonzima hana shaka naye, lakini naye pia alazimika kumuangalia kwa mara nyingine uwezo wake ili ajiridhishe kwa sababu ni muda mrefu tangu amuone akicheza.
“Ninachokitaka ni kuwa na kikosi imara ambacho hakitakuwa kikitegemea baadhi ya wachezaji na ndiyo sababu ya kutaka kuwaona wachezaji hao ili nijue uwezo wao na baada ya hapo nitaweka hadharani nani ambaye hatutakuwa naye,” alisema Maximo.
Baada ya Maximo kumsajili Jaja wanachama na mashabiki wa timu hiyo wamekuwa wakiumiza kichwa kutaka kujua mchezaji gani kati ya Kiiza na Okwi atakatwa kwenye usajili wa msimu ujao huku kila mtu akiwa na mapendekezo yake.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog