KWA muda mrefu tumekuwa
tukizungumzia suala la klabu kuwa na viwanja vyake vya soka kwa ajili ya
mazoezi huku mkazo wetu ukiwa katika klabu za Ligi Kuu.
Hoja yetu hii kwa wakati wote imekuwa
ikizinyooshea kidole klabu kongwe za Simba na Yanga ambazo hazijalipa
umuhimu wa kipekee suala hili.
Klabu hizi ambazo zimeanzishwa miaka zaidi ya 70
iliyopita hadi sasa havina viwanja vyenye hadhi japo kwa ajili ya
kufanyia mazoezi.
Hili ni jambo la aibu ambalo tumekuwa tukilikemea
mara zote hasa inapotokea timu kama Azam ambayo imeanza kutamba katika
Ligi Kuu katika kipindi kisichozidi miaka mitano iliyopita kumiliki
uwanja wenye hadhi ya kucheza hata mechi za kimataifa.
Hivyo hivyo na Mtibwa Sugar ambayo haina miaka 20
katika ligi ya juu nchini lakini inamiliki uwanja wake unaofaa kwa
mazoezi na hata mechi za ligi.
Kilio chetu hicho walau kimesaidia kuiamsha Simba
ambayo imeanza harakati za ujenzi wa uwanja wake maeneo ya Bunju B nje
kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Hali ni hivyo hivyo kwa Yanga ambao tofauti yao na
Simba ni kwamba wao wana eneo lakini hawalijali na hawaonyeshi nia ya
dhati ya kulifanya liwe uwanja wenye hadhi japo ya mazoezi.
Wakati Yanga na Simba wakionekana kupuuza hoja
hiyo, juzi Jumanne Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
Boniface Wambura alinukuliwa akisema kwamba kuanzia mwaka ujao hakuna
klabu ya Ligi Kuu itakayoruhusiwa kushiriki mashindano yanayoandaliwa na
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) bila ya kuwa na leseni ya shirikisho
hilo pamoja na uwanja.
Ni dhahiri kwamba Agizo hilo la CAF ambalo limo
kwenye katiba ya TFF linaziumbua klabu hizi na nyinginezo zilizodhamiria
kushiriki michuano inayoandaliwa na CAF.
Kwa kuwa Yanga na Simba ndizo ambazo zimekuwa
zikichuana mara kwa mara kuwania tiketi ya kushiriki mashindano ya CAF,
agizo hilo ni mtihani mwingine kwao.
Ni vyema viongozi wa klabu hizo wakaweka mikakati
thabiti ya kuepukana na fedheha ambayo itajitokeza siku za mbele kwa
kujikuta wakihaha kutafuta uwanja wa kuazima wakati wana uwezo wa kuwa
na viwanja vyao.
Tunaamini kwamba iwapo CAF watawabana, watatafuta
viwanja vya kuwalinda ambavyo vina hadhi lakini jambo hilo kwetu
tunaliona kuwa ni la aibu.
0 maoni:
Post a Comment