Friday, August 8, 2014

 
Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,


Hussein Shariff, Manyika Peter Manyika, Mohammed Hussein, Abdi Banda, Elius Maguli, Saad Kipanga watatambulishwa kesho katika Tamasha la ‘ Simba Day’ katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Tamasha hilo la kila mwaka ambalo hufanyika tarehe 8, Agosti ya kila mwaka lilianza kufanyika kwa mara kwanza msimu wa kiangazi mwaka 2009 chini ya waasisi, Mzee Hassani Dalali na aliyekuwa katibu mkuu wa klabu hiyo, Mwina Kaduguda kwa lengo la kutambulisha wachezaji wapya, jezi mpya za klabu huku pia lengo kiuchumi likiwemo .
Wachezaji hao wazawa wataungana na wachezaji wapya wa kigeni, Paul Kiongera raia wa Kenya, Mrundi, Pierre Kwizera, na washambuliaj raia wa Botswana, Jerome  Ramathakwane na Ousainou Manneh kutoka nchini Gambia katika mchezo maalumu dhidi ya Zesco ya Zambia. Ambao watajaribiwa kwanza na kocha Zdravko Logarusic kabla ya kusajiliwa.
Hussein Sharrif 'Casillas' naye atambaulishwa kesho

Tamasha hilo litafanyika kesho Agosti 9, kufuatia siku ya leo kuwa na Tamasha la Matumaini na mashabiki wa Simba watapata fursa ya kuona na kununua jezi mpya za klabu hiyo ambazo watazitumia msimu ujao. Simba imejipanga kuhakikisha inaimarisha zaidi kikosi chake ndiyo maana wamekuwa ‘ busy’ kusaka wachezaji wakati huu dirisha la usajili likikaribia kufungwa.
WACHEZAJI SABA WA KIGENI
Donald Musoti, Amis Tambwe, Joseph Owino, Kiongera, Kwizera, Jerome, na Manneh watakuwepo uwanjani siku ya kesho. Wachezaji hao wote ni raia wa kigeni na wamekuja kwa ajili ya kuifufua Simba baada ya kuwa na misimu miwili mibaya katika ligi kuu ya Tanzania Bara. Simba inaweza kuwasaini wachezaji wote hao kama mwalimu Logarusic ataridhika na viwango vyao kwa sababu sheria ya wachezaji wa kulipwa itabadilishwa na kufikia wachezaji saba.
Abdi Banda atatambulishwa kesho 'Simba Day'

Hii ni mara ya kwanza kwa Tamasha la Simba Day kuwa na wachezaji saba wa kigeni na ni wakati mwafaka kwa mashabiki wa klabu hiyo kujitokeza uwanjani siku ya kesho kwa lengo la kwenda kuitazama timu yao mpya ambayo inasukwa katika mtindo wa kimataifa.
Ligi kuu inataraji kuanza kutimua vumbi lake, Septemba 20, hivyo baada ya Tamasha hilo timu itakuwa na muda mrefu wa kujiandaa na kutengeneza timu kabambe ambayo itaweza kutoa ushindani kwa timu za Yanga SC, Azam SC, Mbeya City ambazo zimeoneka kufanya usajili makini zaidi licha ya kumaliza katika nafasi tatu za juu msimu uliopita.
Wachezaji kama nahodha Nasorro Masoud ‘ Collo’, Amri Kiemba, Issa Rashid, William Lucian, Jonas Mkude, Said Ndemla, Miraji Adam, Abdallah Seseme, Ibrahimu Twaha, Ramadhani Singano, Haroun Chanongo, Uhuru Suleimani, Ivo Mapunda wataungana na wachezaji wapya waliosajiliwa klabuni hapo siku ya kesho huku mwanamuziki nyota nchini, Diamond Platnumz akitaraji kutumbuiza kabla ya zoezi la utambulisho wa wachezaji kuanza. Itakuwa siku ya aina yake kwa wapenzi wa klabu hiyo.
NI SIKU NZURI KWA KUSAIDIA UJENZI WA UWANJA WA KLABU
Wiki iliyopita Simba ilianza kufanya mazoezi katika uwanja wake wa wazi huko Bunju nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, na juzi wanachama wa tawi la ‘ Home Boys Wazo Hill’ waliahidi kutoa tani 10 za mifuko ya saruji ili kusaidia uendelezaji wa ujenzi wa uwanja wa klabu hiyo ambao unaendelea. Simba inaweza kutumia Tamasha hilo kuwaunganisha wanachama wake ambao walikuwa katika tofauti miaka ya karibuni kutokana na uongozi mbaya wa utawala uliopita. Kila mwanachama wa Simba anaweza kujitolea kwa namna anavyoweza kwa sababu wanachama ndiyo sehemu muhimu ya kuijenga klabu  hivyo ushirikiano ni muhimu kuanzia kwa viongozi, wanachama, wachezaji na benchi la ufundi. Simba Day ina maana kubwa na wanachama wanaweza kutumia nafasi yao kusaidia kwa hali na mali klabu yao. Kila la heri Tamasha la Simba Day…..

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog