Na Mwandishi Wetu
MWIMBAJI mahiri wa muziki wa
Injili, Rose Muhando amelalamika kuwa albamu yake ya Kamata Pindo la
Yesu Albamu anayotarajia kuizindua Jumapili wiki hii imeingizwa mtaani
na wezi wa kazi za wasanii, hivyo kuonya wananchi wawe makini kwani
albamu yake halisi itatoka Jumapili.
Taaifa kwa vyombo vya habari
aliyoitoa Muhando jana, ilieleza kuwa albamu yake halisi bado haijaingia
mtaani na kwamba hiyo wanayoiona wananchi sasa ni bandia na mtu
atakayewauzia wamripoti polisi.
“Albamu ya Kamata Pindo la Yesu
itaanza kuingia mtaani baada ya uzinduzi wangu kwenye ukumbi wa Diamond
Jubilee Jumapili wiki hii. Albamu yangu ina nembo ya TRA (Mamlaka ya
Kodi ya Mapato nchini).
“Hizi CD zinazouzwa hivi sasa si
zangu, hao ni matapeli na nawaomba wananchi tushirikiane kudhibiti
wizi. Hao ni maharamia wa kazi za wasanii wanataka kunyonyajasho langu,
naomba sana wananchi mnisaidie.
“Nasisitiza albamu yangu
sijaiachia sokoni bado mpaka uzinduzi ukamilike, Watanzania wenzangu na
mashabiki wangu kote duniani mnielewe na naomba tusaidiane katika hili
maana CD feki zimezagaa,” alisema Muhando na kuongez akuwa tayari
ameripoti taarifa hiyo kwa vyombo vya dola.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Kampuni ya Msama Promotions inayoratibu uzinduzi huo, Alex msama naye
katika taarifa hiyo ya pamoja alionya wote watakaobanika kuwa CD za
albamu ya Rose Muhando watakumbana na mkono wa sheria.
“Inasikitisha sana kuona baadhi
ya watu wanataka kutumia jasho la wengine kujinufaisha. Watanzania
kuweni macho, msubiri albamu yenyewe ya Rose Muhando Jumapili pale
ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam,” alisema Msama.
Albamu hiyo ya Muhando
itakayozinduliwa Jumapili ina nyimbo za Bwana Niongoze, Wewe Waweza,
Usiniache, Nibariki, Muongo, Kwema, Kamata Pindo la Yesu na Facebook.
Hivi sasa Rose anatamba na
albamu yake ya Utamu wa Yesu, ambapo pia amewahi kutamba na albamu za
Uwe Macho, Nyota ya Ajabu (Zawadi ya Krismasi), Jipange Sawasawa,
Kitimutimu, Mungu Anacheka na Wololo.
0 maoni:
Post a Comment