Wachezaji
wa Stand United (waliovalia jezi za rangi ya machungwa) wakingia
uwanjani kwenye moja ya mechi ya ligi daraja la kwanza msimu uliopita
KOCHA Mkuu wa Stand United, Flugency Novatus
amebwaga manyanga kuinoa klabu hiyo kuelekea msimu wa 2014/2015 wa ligi kuu
soka Tanzania bara unaotarajia kuanza kushika kasi septemba 30 mwaka huu.
Akizungumza jioni hii, kocha huyo aliyeipandisha
klabu hiyo ligi kuu msimu uliopita amesema sababu ya kuondoka kwake ni viongozi
kushindwa kutekeleza ripoti yake iliyoiwasilisha baada ya kumalizika kwa
michuano ya ligi daraja la kwanza.
“Nasikitika kukuambia kwamba kwasasa sipo Stand
United. Moja ya vitu vilivyochangia ni ile hali ya kutofanyia kazi ripoti
yangu. Kwahiyo niliona si busara kukaa na watu wenye mtazamo tofauti na mimi kama
mwalimu.Kwasasa nimerudi Mwanza, nina karibu wiki moja sasa,” Alisema Novatus.
Novatus aliongeza kuwa yeye falsafa yake imejikita
katika soka la vijana na popote anapoenda hufanya kazi kwa kusimamia misingi
hiyo na kama inakuwa tofauti haoni shida kuwajibika.
“Mimi kama mwalimu nakuwa na falsafa yangu,
kufanikiwa au kutofanikiwa inategemea na viongozi ulionao. Lakini kama unaona
huwezi kufanikiwa kwasababu tu mtu fulani hawezi kukupa ushirikiano, sidhani
kama kuna sababu ya kuendelea kuwepo,”
Aidha, Novatus aliweka wazi kuwa mkataba wake
umemalizika leo juni 30, lakini hakuna mazungumzo yaliyofanyika na viongozi wa
klabu hiyo inayokabiliwa na ligi ngumu yenye ushindani msimu ujao..
“Zamani ulikuwa unaweza kufanya kazi ukitegemea
kuwa ipo siku mtakaa muongee, siku hizi mambo ni tofauti, mambo yanaenda
kisayansi zaidi na mpira unaendelea kukua nchini kwetu. Mambo yanazidi kuwa
wazi, kwasababu hata mchezaji, huwezi kumpeleka sehemu fulani akacheza bila
kusaini mkataba,”
Pia kocha huyo alisisitiza kuwa maandalizi
wayafanyayo Stand United haoni kama angetimiza malengo yake, hivyo njia pekee
ilikuwa ni kuiacha timu na kurudi katika kituo chake cha Alliance cha Mwanza.
“Wewe kama kiongozi unajiandaaje na ligi kubwa
kama hii, ligi ya Vodacom ndio ligi kubwa kuliko zote na ndio ligi inayomtambulisha mtu. Kwasababu
umeingia, muda wowote unaweza kucheza mechi za kimataifa ukishika nafasi ya
kwanza au ya pili”
“Sasa kama kiongozi imejiandaa na hilo jambo? Kama mwalimu naona taratibu hizi tunazoenda nazo hatuwezi kwenda, kuna haja gani ya kuendelea kuwepo. Kwa falsafa yangu ya vijana, nitaendelea nayo na nimerudi katika kituo changu cha Alliance cha mwanza ambapo nilitoka nikaenda Stand,” Aliongeza Novatus.
0 maoni:
Post a Comment