Saturday, February 8, 2014


Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Jamali Malinzi (katikati) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari jana kuhusu siku 100 tangu walipoingia madarakani. Kulia ni msaidizi wa Rais masuala ya Ufundi, Pelegrinius Rutahyuga na kushoto ni Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura.



Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameelezea hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa Ilani yake siku 100 tangu alipoingia madarakani.


Akizungumza na waandishi wa habari leo (Februari 7 mwaka huu) katika mkutano uliofanyika katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam, Rais Malinzi aliainisha maeneo kadhaa yaliyopewa kipaumbele na tayari yameanza kufanyiwa kazi pamoja na changamoto zilizopo.


Alisema muundo wa Idara ya Ufundi umebadilishwa kwa kuundwa vitengo vya ufundi, elimu na maendeleo ya mpira wa miguu huku maeneo ambayo tayari yameanza kufanyiwa kazi kuwa ni;


Ujenzi wa kituo cha mpira wa miguu (football centre of excellency), timu kupanda daraja, kuanzisha mashindano mapya na kufufua ya zamani, mpira wa miguu wa wanawake, maandalizi ya vijana (grassroot football), tiba, walimu na makocha, utawala, uhusiano na Zanzibar, klabu za mpira wa miguu, wachezaji, masoko na uwekezaji, kitengo cha habari, viwanja na timu ya Taifa (Taifa Stars).


Rais Malinzi amesema changamoto zilizopo kwa sasa ni matumizi ya tiketi za elektroniki, ufinyu wa bajeti, madeni, nidhamu, maadili na uchezeshaji wa waamuzi.


Ametoa mwito kwa wadau wote nchini wakiongozwa na Serikali, Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Afrika (CAF), Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), vyombo vya habari, mashirika ya umma na kampuni binafsi kushikamana na kuwa kitu kimoja kwa nia ya kuinua kiwango cha mpira wa miguu Tanzania.
TANZANIA  FOOTBALL  FEDERATION
TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA ILANI YA UCHAGUZI
YA RAIS WA TFF
Ndugu zangu,
Uchaguzi mkuu wa TFF ulifanyika  tarehe 27 Oktoba, 2013 na kukamilika alfajiri ya tarehe 28 Oktoba, 2013 ambapo Kamati ya Utendaji ya TFF ilitangazwa rasmi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa TFF Ndugu Hamidu Mbwezeleni.
Katika kuelekea uchaguzi mkuu huo niliitisha mkutano na waandishi wa habari ambapo nilitangaza ilani yangu ya uchaguzi.  Lengo la ilani ilikuwa ni kuwaeleza wadau na wapenzi wa mpira wa miguu Tanzania dira ambayo ingeongoza mpira wetu iwapo ningechaguliwa kuwa Rais wa TFF.  Aidha niliahidi iwapo ningechaguliwa tungekutana katika chumba hiki hiki  baada ya siku 100.  Ninapenda nichukue fursa hii  kuwashukuru na kuwapongeza wajumbe wote wa Mkutano Mkuu wa TFF, walionipa kura na ambao hawakunipa kura, kwa kukamilisha vyema zoezi la uchaguzi huo.  Uchaguzi umekamilika kazi iliyobakia mbele yetu ni kutekeleza majukumu yetu kama viongozi wa mpira miguu Tanzania.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog