Tuesday, July 22, 2014


'Messi deserved Golden Ball'
Imechapishwa Julai 22, 2014, saa 4:00 asubuhi

WAKATI mabishano ya kama kweli Lionel Messi alistahili tuzo ya mchezaji bora wa kombe la dunia 2014 nchini Brazil yakipoa `mdogo mdogo`, mchezaji mwenzake wa Barcelona, Sergi Roberto ameibuka tena akisema jamaa yake alistahili kutwaa tuzo hiyo.
Nyota huyo wa Argentina aliyaanza kwa kasi mashindano yaliyomalizika Brazil, lakini alizimika kadiri mashindano yalivyoendelea na alikuwa mchezaji tegemeo katika kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Ujerumani, mechi ya fainali uwanja wa Maracana.
Licha ya nyota huyo mwenye miaka 27 kutajwa kuwa mchezaji bora wa kombe la dunia-maamuzi ya kumpa tuzo hiyo yalipokolewa kwa hisia tofauti na wachezaji, makocha na mashabiki wa soka duniani kote.
Ingawa kwa upande wa Roberto bado ana msimamo kuwa Messi alistahili tuzo hiyo na ametaka aheshimiwe kwa kiwango chake.
“Nilimuona Messi kombe la dunia kama ilivyokuwa miaka mitatu iliyopita,lakini mwaka huu alikuwa kwenye ubora wake.” Aliwaambia waandishi wa habari.
“Anastahili zawadi na kumkosoa sio haki, alitaka kushinda kombe la dunia, anastahili heshima kubwa. Ameisaidia sana klabu yake na Argentina”.
Roberto mwenye miaka 22, pia aliwasifu Real Madrid kwa usajili wa karibuni wa Toni Kroos kwa kuzingatia ubora wake wa siku za karibuni katika kikosi cha Bayern na timu ya Taifa ya Ujerumani.

“Ni mchezaji mzuri sana, amethibitisha hilo kombe la dunia na klabu ya Bayern. Hajajiunga na sisi, lakini mchezaji yeyote bora anakaribishwa Barcelona”.

MWAMBUSI AJIANDAA KUCHEZA `FAINALI 26` LIGI KUU BARA

Na Baraka Mpenja, Dar es saalam

Imechapishwa Julai 22, 2014, saa 3:36 asubuhi

MSIMU uliopita wa ligi kuu soka Tanzania bara, Juma Mwambusi wa Mbeya City fc alichaguliwa kuwa kocha bora wa msimu baada ya kuiongoza klabu hiyo mpya kushika nafasi ya tatu katika msimamo.
Mbeya City fc walizisumbua klabu kubwa za Simba na Yanga, hata mabingwa Azam fc. Walimaliza nafasi ya tatu mbele ya mnyama Simba kwa kujikusanyia pointi 49 kibindoni.
Walishinda mechi 13, wakatoka sare mechi 10 na kufungwa mechi 3. Walikula kipigo cha kwanza cha bao 1-0 kutoka kwa Yanga ndani ya uwanja wa Taifa. Wakalala 2-0 dhidi ya Wagosi wa Kaya, Coastal Union, Mkwakwani Tanga. Na mechi ya tatu kufungwa ni ile ya 2-1 dhidi ya Azam fc.
Mechi hii ilipigwa uwanja wa Sokoine na kimsingi ndio iliamua ubingwa kutua mikononi mwa wana Lambalamba.
Mwambusi ni kocha maarufu nchini, kila timu anayoifundisha inapata mafanikio. Kumbuka alipokuwa na wajelajela Tanzania Prisons hali ilikuwaje.
Msimu uliopita, Mwambusi alikuja na kikosi chenye wachezaji wapya kabisa katika michuano ya ligi. Walikuwa vijana wadogo wasio na uzoefu, lakini aliwaamini kwasababu alitoka nao ligi daraja la kwanza ambapo alipanda kucheza ligi kuu bila kufungwa mchezo wowote.
Mwambusi ni mtu wa kuthubutu na ukizingatia nyuma yale alikuwepo msaidizi imara, Maka Andrew Mwalwisyi, ingawa kocha huyu mwenye leseni B ya CAF ameamua kuachana na klabu hiyo.
Anapotajwa kuwa kocha bora wa msimu, manake aliwazidi wenzake mbinu . Mwambusi alikuwa na timu changa na alipambana na makocha wenye timu kubwa kama Hans van Pluijm (aliyekuwa kocha wa Yanga), Joseph Marius Omog wa Azam na Zdravko Logarusic wa Simba.
Wakati Omog, Pluijm, na Loga wakiwa na wachezaji wa kimataifa katika vikosi vyao, Mwambusi alikuwa na vijana wa Kitanzani, tena wengi wao wanatoka nyanda za juu kusini, hususani Mbeya.
Kwa mafanikio aliyopata kuzingatia timu aliyokuwa nayo, tuzo ya kocha bora ilimfaa.
Lakini Mwambusi anatambua ugumu uliopo mbele yake baada ya kuwa kocha bora msimu uliopita?
Kocha huyu anasema msimu ujao utakuwa na changamoto kubwa kwake kwasabababu timu zote zinajiandaa na yeye ataingia kama mshindani wa ubingwa, huku akiamini kuwa timu zitacheza naye kwa nguvu kama ilivyo kwa Simba, Yanga na Azam fc.
Kocha wa Mbeya City fc, Juma Mwambusi (katikati) akizungumza na wachezaji wake Hassan Mwasapili (kushoto) na Peter Richard (kulia).

Mwambusi aliongeza kuwa maandalizi ya msimu mpya yanakwenda vizuri na atapiga kambi nje ya nchi ambapo atacheza mechi kadhaa za kirafiki.
Tayari uongozi wa klabu hiyo ulishapewa programu ya kocha wao, na mwenyekiti wake, Mussa Mapunda alisema watakwenda Malawi na Zambia ambapo watacheza angalau mechi mbili mbili za kujipima ubavu.
Kocha Mwambusi alisema: “Ligi msimu ujao itakuwa ngumu na mbele yetu kuna changamoto kubwa, lakini siku zote tunajiandaa kwa mechi zote 26. Kila mchezo kwetu huwa unakuwa muhimu, kwahiyo tunajiandaa vizuri”.
“Falsafa yetu sio kusajili majina makubwa, tunawaamini vijana wetu. Timu yangu imebaki vilevile, ingawa nimeongeza wachezaji wawili watatu”. Aliongeza Mwambusi.
Kocha huyo alisema hatishiki na makocha wa kizungu kwasababu mbinu za mpira ni zile zile, hivyo anajiandaa vizuri kukabiliana na changamoto hizo.
Msimu ujao, wachezaji wa Mbeya City wanaweza kufanya vizuri ukizingatia watakuwa na uzoefu wa msimu mmoja. Kuongezeka kwa Them Felix `Mnyama` aliyesajiliwa kutoka Kagera Sugar kutaifanya safu ya ushambuliaji kuwa na nguvu zaidi.

Them atafanya kazi na akina Mwegane Yeya, Paul Nonga, Deus Kaseke na Peter Mapunda.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog