Tuesday, July 22, 2014


Makamu Mwenyekiti Mtendaji  wa Manchester United, Ed Woodward, amewaambia Mashabiki wa Klabu hiyo kuwa wategemee ujio wa Wachezaji wapya kadhaa na pia kuhama kwa baadhi ya Wachezaji katika Wiki chache zijazo.
Hadi sasa Man United imetumia Pauni Milioni 50 kuwanunua Luke Shaw na Ander Herrera na kauli hii ya Woodward inaleta imani kuwa Meneja mpya Louis van Gaal atapata Wachezaji wengine wapya kabla Msimu mpya kuanza. 

Kwa sasa, Wachezaji wanaohusishwa kuhamia Man United ni pamoja na Arturo Vidal, Daley Blind, Kevin Strootman na Thomas Vermaelen.
Woodward ametamka: “Hamna kiwango cha Bajeti kilichowekwa. Kifedha tuna nguvu sana, zipo Fedha za Uhamisho. Louis ndie Bosi na anatathmini nini kinaendelea lakini tumekuwa na mazungumzo na walengwa na kazi inaendelea nyuma ya pazia. Tunasonga mbele kwa baadhi ya walengwa hao…hivyo kaeni chonjo hapa!” 

Aliongeza: “Louis anapata muda zaidi wa kufanya tathmini yake na ikibidi tutabadilisha maamuzi na kufanya mengine. Tunataka kuchukua hatua thabiti ili kutwaa Ubingwa!”
Msimu uliopita Man United walimaliza Nafasi ya 7 kwenye Ligi Kuu England na hivyo Msimu ujao hawatashiriki Mashindano ya Klabu Barani Ulaya, ikiwa ni mara ya kwanza tangu 1996, lakini Woodward amedai hilo haliathiri wao kupata Wachezaji wapya.

Ameeleza: “Nimeongea na Mawakala na Wachezaji wengi na sisi bado ni kivutio kikubwa kwa Wachezaji Dunia nzima. Hilo halina wasiwasi. Tayari tumeshapata Wachezaji wawili hodari kabisa!”

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog