Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
WAZEE wa kale walishasema, `Bahati haiji mara
mbili`!. Kumekucha kwa Watanzania kuwaona `laivu` magwiji waliotikisha soka la
dunia ngazi ya klabu na michuano ya kimataifa ikiwemo kombe la dunia.
Magwiji waliocheza kwa mafanikio makubwa katika
klabu ya Real Madrid wanatarajia kufanya ziara ya siku nne nchini kuanzia
Agosti 22 mwaka huu ambapo watacheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya kikosi
maalum cha nyota wa Tanzania.
Ziara hiyo ni mwaliko wa kampuni ya Tanzania Sisi
ni Nyumbani (TSN), chini ya mkurugenzi wake mkuu, Farough Baghozah na meneja wa
ziara hiyo ni Dennis Ssebo.
Akizungumza na mtandao huu mchana wa leo, Dennis
Ssebo amesema maandalizi ya ziara hiyo yanakwenda vizuri na watanzania
watarajie kuwaona wachezaji wakubwa waliotamba miaka ya nyuma kama vile Ronaldo
Delima, Luis Figo, Roberto Carlos, Zinedine Zidane na wengineo.
“Ninaloweza Kusema ni kwamba, Watanzania wakae tayari kupokea wachezaji 27 wa
zamani wa timu ya Real Madrid na mashabiki 23
kutoka Hispania wanaokuja kuwashangilia magwiji wao. Kwahiyo jumla
tunapokea watu 50 kutoka Hispania kwa ajili ya ziara hii”. Alisema Ssebo.
“Ni ziara ambayo tulifikiria itakuwa fupi, lakini
wenzetu kumbe wameipenda nchi na wanaifahamu, kwahiyo ni ziara ambayo itachukua
takribani siku nne”. Aliongeza.
Ssebo alisema Magwiji hao wataingia nchini Agosti
22 mwaka huu na watacheza mechi maalumu ya kirafiki Agosti 23 ndani ya dimba la
kisasa la Taifa, jijini Dar es salaam.
“Baada ya mechi wataenda Arusha Agosti 25 kuangalia
vivutio vya utalii na watalala huko. Watalala tena Dar es salaam na kuondoka
tarehe 26 ya mwezi wa nane”.
“Kwahiyo ni ziara ambayo ni ndefu kidogo, watu ni
wengi, tulifikiri timu ingekuja peke yake, kumbe kuna mashabiki wanaotoka
Hispania kuwashangilia hao magwiji, nafakiri Watanzania tukae mkao wa kula,”.
Alifafanua Ssebo.
Kuhusu viingilio vya mechi hiyo, Ssebo alisema
watakuwa na kiwango cha chini kinachoweza kulipwa na watanzania wengi.
“Tunawahakikishia watanzania kuwa wataangalia
mechi hii kwa kiwango cha chini kabisa.”
“Naweza kuthubutu kusema kuwa kiwango cha chini
kabisa kitakuwa shilingi elfu 5 ambacho tunaamini Watanzania wa kawaida
wataipata kwasababu tumewaambia mapema kwa mwezi mzima.” Ssebo alisema.
“ Lakini
kikubwa zaidi, ni kuwahakikishia watanzania kuwa ziara hii itafungua milango ya
kujiuza na kuuza vivutio vyetu vya utalii”.
“ kwahiyo ni zaidi ya mpira na sisi tunaamini
kabisa kuwa tutakuwa na uwezo wa kuuza vitu vyetu, kwasababu wao watakuja na
mashabiki, halafu Real Madrid TV watakuja kurekodi ziara nzima timu ikiwa
Tanzania”. Alisema Ssebo.
Hii ni ziara ya kwanza kabisa kwa klabu ya Real Madrid kufanya barani Afrika, hivyo ni bahati kwa Tanzania kuwa nchi ya kwanza kutembelewa na timu kubwa ya Real Madrid.
0 maoni:
Post a Comment