Thursday, May 8, 2014




 DSC_4575
Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
MOJA ya kilio kikubwa cha watanzania ni kutaka kuona timu ya Taifa ya Tanzania,  Taifa stars inafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
Tangu iliposhiriki kwa mara mwisho fainali za kombe la mataifa ya Afrika mwaka 1980 nchini Nigeria, Taifa Stars haijafanikiwa kupata nafasi kama hiyo.
Kuelekea fainali za mataifa ya Afrika, AFCON zitakazofanyika mwakani 2015 nchini Morocco, uongozi wa shirikisho la soka Tanzania TFF umeanza kampeni za kuisaidia Stars ifuzu kushiriki fainali hizo.
Kabla ya kuondoka kwake, kocha wa Taifa stars aliyevunjiwa mkataba mwaka huu, Kim Poulsen aliweka mikakati ya kuivusha Taifa stars kucheza fainali za AFCON mwakani.
Mara zote Kim alikuwa anasema ndoto zake zinaweza kutimia kwa kutumia wachezaji waliopo sasa Taifa stars na kutafuta wengine wapya wanaoshiriki michuano ya ligi kuu.
Moja ya mkakati wa Kim ilikuwa ni kutafuta wachezaji wengi zaidi na akalazimika kuwa na timu mbili za Taifa.
Moja ilibaki kuwa Taifa Stars iliyozoeleka, lakini akaongeza  nyingine ya `Young Future Taifa Stars`.
Timu hii ya `Young Future Taifa stars`  ilijumuisha wachezaji wanaotoka klabu za ligi kuu, lakini hawakuwa na nafasi timu ya Taifa.
Lengo la Kim lilikuwa ni kupata uwanja mpana wa kutafuta wachezaji wa kumsaidia kufuzu AFCON mwakani.
Hakika mpango huu uliungwa mkono na wadau wa soka na wengi wao walijenga hoja yao kuwa ungewashitua wachezaji waliopo Stars kuwa kuna wenzetu wapo nyuma yetu kama watazembea.
Chini ya Kim, Taifa stars ilibadilika kiuchezaji, japokuwa haikufanikiwa kufanya vizuri katika mashindano makubwa.
Lakini iliweza kuzifunga timu kama Morocco, Zambia, Gambia, Cameroon na kuonesha kiwango kizuri.
Baada ya mabadiliko ya uongozi ndani ya TFF, Rais mpya wa shirikisho hilo, Jamal Malinzi alikuja na mipango yake.
malinzi
Rais wa TFF, Jamal Malinzi
Moja ya vitu alivyofanya siku za kwanza ni kubadili watu katika maeneo mengi ya uongozi wake.
Malinzi aliwaondoa watendaji wengi waliokuwa chini ya Rais aliyemaliza muda wake, Leodger Chila Tenga.
Rungu hili la mabadiliko lilimwangua  kocha wa Taifa stars, Kim Poulsen ambaye alivunjiwa mkataba kwa madai ya kushindwa kuifanikisha Taifa stars na amelewa Mholanzi, Mart Nooij.
Kilio kikubwa cha makocha wengi na wapenda soka nchini Tanzania ni kukosa mfumo mzuri wa soka la vijana.
Makocha wengi wanadai wachezaji wengi wa kitanzania wamekosa mambo ya msingi katika mpira kwasababu wengi wao wameanza kujifunza mpira ukubwani.
Kwa misingi hiyo, makocha wengi wanapendekeza nguvu kubwa kuwekezwa katika maendeleo ya soka la vijana.
Malinzi alikuja na mpango mzuri wa soka la Tanzania, na moja ya vitu vikubwa alivyoahidi kuwekea mkazo ni kuifanikisha Taifa stars kufuzu AFCON mwakani nchini Morocco.
Pia alisema anataka kujenga vituo kadhaa vya kukuza viapji vya vijana yaani akademi.
Lengo si kuandika ahadi zake, lakini makala hii inajaribu kuona mpango wa Malinzi na Taifa stars.
Rais huyo aliwashitua wengi baada ya kuja na mpango mpya wa maboresho ya Taifa stars.
Alitumia makocha wengi wa soka waliocheza soka zamani kujadili namna ya kuboresha Taifa stars.
Kwa pamoja, makocha hawa walikubaliana kuwa Tanzania kuna vipaji vingi  vilivyofichika, hivyo liundwe jopo la kuzunguka mikoani kutafuta vijana wa kuwaingiza Taifa stars.
Toka mwanzo, makocha wengi wa kisasa walikuwa na mashaka na mfumo huu, lakini TFF wakasisitiza utasaidia sana kuipeleka Stars AFCON.
Malinzi alisema watatafutwa vijana wengi na kuchujwa ili kupata wachache watakaojiunga na Stars. Na kweli zoezi likaanza na kupatikana vijana hao.
Wachezaji hawa wa maboresho ya Taifa stars waliwekwa kambini mjini Tukuyu na kwa mara ya kwanza waliletwa jijini Dar es salaam kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya timu ya taifa ya Burundi.
Staz
Taifa Stars ya maboresho iliyochapwa mabao 3-0 na Burundi aprili 26 mwaka huu uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam
 Mechi hii ilikuwa siku ya maadhimisho ya miaka 50 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar aprili 26 mwaka huu, na hamu ya wapenzi wengi wa soka ilikuwa kuiona Stars ya maboresho iliyosifiwa na baadhi ya wadau walioshauriana na Malinzi.
Kama kawaida, vijana hawa walitandikwa mabao 3-0, na si kufungwa tu, hata mpira walichezewa.
Katika mechi hiyo walioonekana kucheza ni wale wanaocheza ligi kuu kama akina Saimon Msuva, Frank Domayo na wengine wachache, lakini vijana wa maboresho kila mtu aliona walichofanya.
Baada ya mechi hiyo, jambo jipya likalipuka ambapo TFF walikosolewa kwa mpango huu na nadhani wao pia waliona hakuna walichofanya.
Mechi dhidi ya Malawi kule Mbeya, Kocha mkuu, Mart Nooij aliwabwaga wachezaji wote wa maboresho ya Taifa stars na kuwadhihirishia TFF na makocha waliopanga mfumo huu na watanzania wote kuwa tumepoteza pesa bure.
Wadau wengi wamekuwa wakikosoa mfumo huu wa Malinzi na kupendekeza wakae tena na makocha wao kubuni njia mbadala ya kuisaidia Taifa stars.
Kila binadamu ana udhaifu wake, na kwa bahati mbaya Watanzania wengi huwa hatukubali kirahisi  kukosolewa.
Mnapokaa makocha 40 kujadili namna ya kuendeleza soka la nchi ndani ya chumba, mnaweza kukubaliana mfumo fulani utumike kama huu wa mabaoresho kwasababu tu mnafafana mawazo.
Lakini kuna jambo moja la msingi  sana hapa, sidhani kama makocha wote kwa moyo mmoja waliunga mkono mfumo huu. Naamini wapo walioona kabisa ni kupoteza muda, lakini walishindwa kushauri kwasababu zao .
Inawezekana walikuwa waoga kwasababu walikuwa nyuma ya mwamvuli wa watu fulani. Labda kuna watu yatari waliingia na majibu yao kwa maana ya mpango kupangwa na makocha kuitwa ili waubarik na kuanza kusaidia kuzunguka kuzunguka mikoani.
Lakini kama kweli walikuwa na nia ya dhati ya kuisaidia Stars ifuzu AFCON, hatudhani kama wangekuja na mpango huu wa maboresho.
Haya sasa, ukweli umeonekana, cha msingi ni TFF kukubali kukosea na kujipanga upya.
Kukosea jambo la kawaida, lakini kukabiliana na kosa ni jambo jema zaidi.
Nadhani TFF ni wasikivu na wanasikia kilio cha watanzania kuwa mfumo wa huu wa maboresho ya Taifa stars ni mzuri, lakini unahitaji muda na si mpango wa haraka.
Huwezi kutafuta wachezaji wa timu ya taifa mikoani zaidi ya timu hizi za ligi kuu.
Wachezaji ni hawa hawa akina Ngassa, Domayo, Bocco, Canavaro, Yondan, Nyoni, Singano, Msuva, Kiemba, Samatta, Ulimwengu na wengineo. Hawa wa maboresho si wakutupeleka AFCON mwakani.
Waongezwe wengine kutoka timu za ligi kuu au waliopo waandaliwe vizuri.
TFF mkipata nafasi ya kujadili tena na kutathimini mavuno ya mpango wa maboresha ya Taifa stars, fikirieni upya juu la wazo lenu ili mje na njia sahihi.
Ongezeni makocha wa kisasa waje na mipango mipya na msitumie historia kuwa fulani alitolewa mkoani akaja kuisaidia Taifa stars.
Maisha yamebadilika na soka la kisasa linahitaji utaalamu, lakini kwa haraka haraka kazaneni na mpango wa akademi, hapo nadhani kutakuwa na jambo zuri la kuzungumza.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ikiwa chini ya Kocha mpya, Mart Nooij tayari ipo jijini Mbeya kujiwinda kwa mechi hiyo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya mashindano dhidi ya Zimbabwe itakayochezwa jijini Dar es Salaam kati ya Mei 16 na 18 mwaka huu.
Kukubali kosa si dhambi hata kidogo. Asubuhi njema kwako msomaji wetu.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog