Aliyekuwa Kocha mkuu wa Yanga sc, Hans Van Der Pluijm ( wa
kwanza kulia) akiwa na wasaidizi wake, Boniface Mkwasa ( wa pili kulia)
na Juma Pondamali ( wa tatu kulia)
KOCHA mkuu
wa Young Africans, Mholanzi, Hans Van der Pluijm amepata kazi mpya nchini Saudi
Arabia na tayari ameshaaga rasmi mchana huu kwa wachezaji wake, viongozi,
wapenzi na wanachama wa klabu hiyo.
Pluijm
aliyejiunga na Yanga mapema januari mwaka huu umepata shavu hilo katika klabu
ya Al Shoalah FC inayoshiriki ligi kuu soka nchini Saudi Arabia.
Mholanzi
huyo amemaliza mkataba wake wa miezi sita na klabu ya Yanga, lakini mbaya zaidi
ameshindwa kuwasaidia wanajangwani kutetea ubingwa wao msimu huu uliomalizika
aprili 19 mwaka huu.
Yanga
chini ya Pluijm ilimaliza katika nafasi ya pili, huku Azam fc chini ya kocha
Mcameroon, Joseph Marius Omog wakibeba taji lao la kwanza tangu wapande ligi
kuu msimu wa 2008/2009.
Pluijm alirithi mikoba ya mholanzi mwenzake, Ernie
Brandts aliyetimuliwa mwezi desemba mwaka jana baada ya kufungwa mabao 3-1 na
Simba katika mechi ya Nani Mtani Jembe.
Brandts aliondoka pamoja na wasaidizi wake Fredy
Felix Minziro na kocha wa makipa Mkenya Razak Ssiwa na nafasi zao kuchukuliwa na Pluijm, Charles Boniface Mkwasa na Juma
Pondamali `Mensah`.
Taarifa rasmi kutoka Yanga inaeleza kuwa Pluijm
aliyeiongoza Yanga kwa miezi mitano imesema kuwa Puijm ametoa shukurani zake kwa
ushirikiano mkubwa aliokuwa anapewa kwa
kipindi chote alichokaa na Yanga.
Pluijm amekaririwa akisema: "Najua wengi
itawashangaza kuona naondoka, lakini
ukweli ni kwamba nilikua na hii dili hata kabla ya kuja Yanga”.
“ Nilikuwa na makubaliano na timu ya Al Shoalah FC,
ambayo yanaanza mwezi ujao, hivyo nilikubaliana na viongozi wa Yanga kuja
kufanya kazi kwa kipindi cha miezi sita tu”.
“Nashukuru tumefanya kazi salama na baada ya
mkataba huo kumalizika nipo tayari kurudi kuja kufanya kazi Tanzania"
alisema Pluijm.
Aidha , Pluijm alieleza kuwa tayari ameshajaza
fomu ya uanachama wa Yanga, hivyo
anajiona ni sehemu ya klabu hiyo yenye makazi yake makutano ya Twiga na Jangwani,
Kariokoo, jijini Dar es salaam.
Kocha huyo aliongeza kuwa yupo tayari kuisaidia
Yanga kupata wachezaji wazuri watakaoisaidia klabu katika michuano ya ligi kuu
soka Tanzania bara msimu ujao na michuano ya kombe la shirikisho.
Pluijm anaondoka leo nchini kwenda Ghana kisha atakwea
pipa kwenda nchini Saudi Arabia tayari kwa kujiandaa na maandalizi ya msimu
ujao wa ligi kuu nchini humo.
Mkataba wa Pluijm na klabu hiyo ya Saudia ni wa
mwaka mmoja.
Tayari
kocha huyo ameshakabithi ripoti jana, kinachofuata ni viongzoi kuifanyia
kazi na baadaye kuweka wazi nini mapendekezo yake.
0 maoni:
Post a Comment