Na Boniface Wambura, Dar es salaam
Timu ya
Nigeria (Flying Eagles) imewasili nchini kwa ajili ya mechi ya michuano ya
Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 dhidi ya Tanzania (Ngorongoro
Heroes) itakayochezwa Jumapili (Mei 11 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam.
Flying
Eagles yenye msafara wa watu 32 imewasili leo (Mei 8 mwaka huu) alfajiri kwa
ndege ya Ethiopian Airlines ambapo imefikia hoteli ya Sapphire. Mechi hiyo ya
kwanza ya raundi ya pili itafanyika kuanzia saa 10 kamili jioni.
Nigeria
inayofundishwa na kocha Manu Garba itafanya mazoezi leo (Mei 8 mwaka huu) saa
10 jioni itafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa ambao ndiyo utakaotumika kwa
mechi siku ya Jumapili.
Viingilio
katika mechi hiyo vitakuwa sh. 2,000 kwa sehemu zote wakati upande wa VIP
itakuwa ni sh. 5,000. Tiketi zitauzwa uwanjani siku ya mechi katika magari
maalumu.
Ngorongoro
Heroes ambayo katika raundi ya kwanza iliitoa Kenya kwa jumla ya mabao 4-3
inaendelea kujinoa jijini Dar es Salaam chini ya Kocha wake John Simkoko na
Msaidizi wake Mohamed Ayoub kujiweka sawa kwa mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu
na washabiki wa mpira wa miguu nchini.
Nigeria
kama ilivyo kwa nchi nyingine 12 imeanzia moja kwa moja raundi ya pili kutokana
na ratiba iliyopangwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF). Nchi hizo
ni Afrika Kusini, Angola, Benin, Burkina Faso, Cameroon, Gabon, Ghana, Jamhuri
ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Mali, Misri, Morocco na Zambia.
0 maoni:
Post a Comment