Thursday, July 23, 2015

YANGA SC wamezinduka katika michuano ya Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame, baada ya jioni ya leo kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Telecom ya Djibouti, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga SC iliyoanza vibaya mechi za Kundi A kwa kufungwa 2-1 na Gor Mahia ya Kenya, sasa inaweza kwenda Robo Fainali iwapo itashinda mechi zijazo dhidi ya KMKM na Khartoum N ya Sudan.
Katika mchezo huo, uliochezeshwa na refa Issa Kagabo wa Rwanda aliyesaidiwa na Lee Okello wa Uganda na Yeatyew Belachew wa Ethiopia, hadi mapumziko, Yanga SC walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Malimi Busungu akipongezwa na Msuva na Tambwe baada ya kufunga bao la kwanza

Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji mpya kutoka Mgambo JKT ya Tanga, Malimi Busungu dakika ya 26 baada ya kufumua shuti la kitaalamu akiwa katikati ya msitu wa mabeki wa Telecom, kufuatia krosi ya beki wa kulia, Mghana Joseph Tetteh Zuttah.
Yanga SC wangemaliza kipindi cha kwanza wanaongoza kwa mabao zaidi, kama wasingepoteza nafasi tatu za wazi za kufunga na kukosa pia penalti mbili.
Dakika ya 10 Busungu alipewa pasi nzuri na beki wa kushoto, Mwinyi Hajji Mngwali aliyepanda kusaidia mashambulizi, lakini shuti lake likaokolewa na kipa Mrundi, Jeff Nzokira. 
Dakika ya 16, mshambuliaji Amisi Tambwe alipiga juu ya lango akiwa amebaki yeye na Mrundi mwenzake, kipa Nzokira ndani ya 18 baada ya kupasiwa na Busungu. 
Tambwe akapiga nje mkwaju wa penalti dakika ya 39 baada ya winga Simon Msuva kuchezewa rafu kwenye boksi na Warsama Ibrahim Aden.
Warsama Ibrahim Aden akasababisha penalti nyingine, baada ya kuunawa mpira ulioinuliwa na Msuva dakika ya 43, lakini shuti dhaifu la mfungaji huyo bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania likapanguliwa na kipa Nzokira.
Malimi Busungu akimtoka beki wa Telecom
Beki Hussein Botoyi wa Telecom akimpitia Mrundi mwenzake, Amissi Tambwe wa Yanga


Beki wa Yanga SC, Mwinyi Hajji Mngwali akitafuta njia ya kuwapita wachezaji wa Telecom
Simon Msuva alisababisha penalti mbili, moja akakosa mwenyewe, nyingine akakosa Tambwe


Kipindi cha pili, kocha wa Yanga SC aliwatoa wote wakosa penalti, Msuva na Tambwe na kuwaingiza Godfrey Mwashiuya na Mliberia Kpah Sherman.
Yanga SC ikafanikiwa kupata bao la pili dakika ya 66, mfungaji Yule Yule, Busungu akimalizia krosi nzuri ya Mwashiuya. 
Mwashiuya akafungua akaunti yake mabao Jangwani baada ya kufunga bao la tatu dakika ya 77 baada ya kufumua shuti kali kutoka umbali wa mita 19 ‘lililomsumbua’ kipa Nzokira kabla ya kudondokea nyavuni.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Joseph Zutah, Haji Mwinyi, Kelvin Yondani, Salum Tela, Simon Msuva/Godfrey Mwashiuya dk46, Haruna Niyonzima, Amisi Tamwe/Kpah Sherman dk46, Malimi Busungu na Deus Kaseke/Andrey Coutinho dk87.
Telecom FC; Jeff Nzokira, Said Hassan Elmi/ Warsama Hussein Said dk52, Daoud  Wais Ali, Mohamed Kader Daher, Warsama Ibrahim Aden, Moussa Ahmed Hassan, Mohamed Meraneh, Abubakar Dharar Djama, Mohamed Moustafa/ Anwar Sadad Ibrahim dk82, Eninga Freddy na Hussein Butoyi.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog