Saturday, July 19, 2014


Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976

Imechapishwa Julai 19, 2014, saa 4:14 asubuhi

WASWAHILI wana msemo maarufu usemao`Utavuna ulichopanda`. Kama ulipanda kokoto utavuna kokoto, usitarajie kuvuna mahindi.
Kwa muda mrefu sasa, timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars imekuwa ikijiandaa kucheza mechi ya kwanza ya kuwania kufuzu hatua ya makundi kusaka tiketi ya kucheza fainali za AFCON mwakani nchini Mrocco dhidi ya timu ya Taifa ya Msumbiji `Black Mambas`.
Mechi hiyo muhimu itachezwa kesho katika dimba la Taifa,  jijini Dar es salaam ambapo Stars watahitaji kupata ushindi mkubwa ili kujiweka mazingira mazuri ya kusonga mbele kabla ya mchezo wa marudiano utakaopigwa wiki mbili zijazo mjini Maputo nchini Msumbiji.
Stars iliweka kambi ya wiki mbili nchini Botswana kwa lengo la kujiweka sawa na wakiwa huko walicheza mechi za majaribio ikiwemo ile waliyofungwa mabao 4-2 dhidi ya timu ya Taifa ya nchi hiyo.
Baadaye ilirejea nchini na kwenda kuweka kambi nyingine mjini Tukuyu, mkoani Mbeya na sasa timu ipo tayari kuivaa Mambas .
Safari hii Taifa Stars imeonekana kuwa na maandalizi mazuri chini ya kocha Mart Nooij. Kwa haraka haraka, unaweza kusema pengine inaweza kufanya makubwa na kuvuna walichopanda kwenye kambi mbili za nje na ndani ya nchi.
Nooij amewahi kuwa kocha wa timu ya Taifa ya Msumbiji na aliifunga  1-0 Taifa Stars mwaka 2007 katika dimba la Taifa kuwania kucheza fainali za mataifa ya Afrika, mwaka 2008 nchini Ghana.
Kwa mazingira haya, Nooij anawajua wachezaji wa Msumbiji na utamaduni wao. Na ndio maana jana alisema anao uwezo wa kuwafunga, japokuwa alikiri kuwa mechi itakuwa ngumu.
Thomas Emmanuel Ulimwengu yuko fiti kuwaua Mambas kesho.

Wachezaji wote wako fiti kwa ajili ya mechi isipokuwa kiungo wa Simba, Jonas Mkude kwani anasumbuliwa na maumivu ya goti na kocha Nooij alisema atakuwa tayari kwenye mechi ya marudiano.
Wachezaji wa Stars wameonekana kuwa katika morali kubwa ya kufanya vizuri ikizingatiwa wenzao wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi wamewasili mapema tofauti na siku za nyuma.
Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, ambao mara nyingi wanapata utata wa kuruhusiwa na TP Mazembe ya DR Congo, safari hii wametia miguu nchini mapema wakitokea nchini Tunisia ambapo timu yao imeweka kambi ya kujiandaa na ligi ya mabingwa.
Mwinyi Kazimoto Mwitula anayecheza nchini Qatar naye yupo nchini akiwa fiti. Wachezaji hao watatu, wamesema wapo tayari kwa mechi na watapigana kufa na kupona kuisaidia timu yao.
Maandiliizi ya Stars yanaridhisha kwa kiwango fulani, na inaonesha jinsi gani TFF ya Rais Jamal Malinzi imedhamiria kuwatoa Msumbiji.
Hili ni jambo jema, wamepanda mbegu nzuri na matunda mazuri yanaweza kuonekana siku ya kesho.
Lakini maandalizi haya ya Stars hayafuti kauli kuwa mpira wa miguu una matokeo matatu. Kuna kufunga, kufungwa na kutoa suluhu au sare.
Wachezaji wamejiandaa kadiri wawezavyo na watacheza kadiri wawezavyo ili kupata matokeo mazuri. Nao Msumbiji wana haki ya kimpira ya kushinda. Timu yoyote inaweza kupata ushindi kutegemeana na mipango.
Taifa stars ipo nyumbani na ina faida kubwa. Itakuwa na mashabiki wengi, ipo uwanja wake uliouzoea, kwahiyo wanayo mazingira mazuri kuliko Msumbiji.
Mbwana Ally Samata alisema safari hii yupo fiti kuwavaa Mambas.

Lakini Msumbiji wanayo historia ya kuifunga Stars katika mchezo wa mashindano ndani ya dimba la nyumbani. Hivyo tahahadhari kubwa inatakiwa kuchukuliwa.
Waliokuwa na majukumu ya kuiandaa timu wamefanya kazi yao, kesho ni zamu ya wachezaji kulipa maandalizi hayo.
Nao mashabiki sehemu yao ipo, wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu, kwasababu mashabiki ni mchezaji wa 12 uwanjani.
Watanzania kwa ujumla wao wanatakiwa kukaa nyuma ya wachezaji ili kuwatia moyo. Tabia ya kuwazomea wanapokosea, kutawafanya washindwe kuonesha kile walichokifuata Botswana na Tukuyu.
Kwa kikosi ambacho Nooij alitangaza kukiteua kwa ajili ya mchezo wa kesho, kuna uwezekano wa kupata matokea.
Kipa yeyoye atakayeanza kati ya Deogratius Munish `Dida` au kinda Aisha Manula anaweza kufanya vizuri, japokuwa Dida ana asilimia kubwa ya kuanza kesho.
Mabeki ambao Nooij ataweza kuwatumia na wako fiti kabisa ni Said Mourad, Ndir Haroub `Cannavaro`, Agrey Morris, Kevin Yondani na Edward Charles.
Viungo ni Erasto Nyoni, Shomary Kapombe, Shaaban Nditi, Simon Msuva, Himid Mao Mkami, Mwinyi Kazimoto, Khamis Mcha `Vialli`, Ramadhani Singano `Messi`, Haroun Chanongo na Amri Kiemba.
Washambuliaji ni Mrisho Khalfani Ngassa, Thomas Emmanuel Ulimwengu, Mbwana Ally Samatta na John Bocco `Adebayor”.
Kwa kikosi hiki, kuna kitu kinaweza kuonekana kesho uwanja wa Taifa.
Kila la kheri Taifa Stars katika mchezo wa kesho.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Taifa stars.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog