Friday, July 3, 2015



Mtendaji Mkuu wa Azam TV, Tido Mhando amesema wataboresha matangazo ya Ligi Kuu
KITUO cha Televisheni cha Azam kimepania kuboresha matangazo ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kuanzia msimu ujao, kuhakikisha yanaptikana katika ubora wa hali ya juu.
Kwa ujumla, Azam TV inayofukuzia miaka miwili tangu ianzishwe imejipanga kuwapatia Watanzania matangazo ya ubora wa kiwango cha juu sana wakati wote wa kipindi cha msimu huu wa mchakato wa uchaguzi mkuu wabunge na Urais mwaka huu wa 2015.
Mtendaji Mkuu Uhai Productions, wazalishaji wa vipindi vya Azam TV, Dunstan Tido Mhando amesema leo kwamba kwa kuwa tukio hili ni la kihistoria, Azam TV pia imedhamiria kutoa matangazo ya kihistoria kwa ubora na ufanisi ukilinganisha na aina ya matangazo ya televisheni ya matukio kama haya katika miaka ya nyuma.
Kwa kutumia teknolojia ya kisasa, vifaa bora pamoja na wafanyakazi wenye ujuzi na weledi, Azam TV hasa kwa kutumia channel yake ya Azam TWO, itatangaza matangazo ya uchaguzi wa mwaka huu kwa kipindi chote cha Uchaguzi kwa kuanzia na harakati za hivi sasa za kutangaza nia kwa wagombea mbalimbali hasa wale wa nafasi ya Urais kutoka chama tawala cha CCM na baadaye kambi ya Upinzani.
Azam Televisheni imejipanga kutangaza mfulilizo wa Matangazo ya Moja kwa moja kutoka Dodoma kwa kutumia vipindi vyake mbalimbali pamoja na vipindi vingine maalum, pilikapilika zote, harakati zote pamoja na matokeo yote ya kilele cha mpambano huo wa hatimae kupatikana kwa mgombea huyo wa Urais wa CCM.
Kuanzia Jumatano July 8 hadi Jumatatu July 13 kikosi cha wafanyikazi wa Azam Televisheni kitapiga kambi Dodoma kueleza kwa kinaga ubaga kila jambo litalokuwa linatokea huko na kwa undani sana ikitumia wachambuzi wenye ujuzi pamoja na kupata na kuzitoa habari za uhakika kwa haraka iwezekanavyo.
Matangazo haya yataanzia tangu mapema asubuhi kwenye kipindi chake cha matangazo ya asubuhi kijulikanacho kama Morning Trumpet, kipindi maalum cha saa moja wakati wa mchana kuanzia saa saba, kipindi cha jioni cha Alasiri Lounge, taarifa ya habari maalum ya saa mbili kutoka saa
mbili kamili usiku pamoja na kipindi maalum cha usiku kuanzia saa nne na nusu hadi saa sita usiku.
Wakati wa kilele cha hekeheka hizi za huko Dodoma yaani tarehe 11 July na 12 July ambapo mkutano mkuu wa CCM unafanyika, Azam Televisheni itakuwa na matangazo ya moja kwa wakati wote wa mkutano huo na baadae.
Baada ya kumalizika kwa mkutano huu, Azam Televisheni itatangaza pia mikutano na mipango mingine kama hii kwa upande wa vyama vingine vya kisiasa.
Utaratibu wa matangazo haya ya uchaguzi utaendelea hivi hivi wakati wa kipindi chote cha kampeni kuanzia mwezi wa August hadi tarehe yenyewe ya uchaguzi hapo Octoba 25.
Labda ni wakati wa kipindi hicho cha uchaguzi kamili ambapo Azam televisheni imejiimarisha zaidi kuweza kuwapatia watazamaji wake matangazo bora ya kisasa zaidi kuliko wakati wowote katika historia ya utangazaji nchini hapa.
Kwa kuzingatia umuhimu wa uchaguzi na upatikanaji wa habari za uhakika kwa watanzania Azam imeweka dhamira hii kama sehemu ya historia kwa kutimiza wajibu wa msingi wa vyombo vya habari kwa umma wa watanzania.
Kwa kutumia studio bora kuliko zote karika kanda hii ya Afrika pamoja na vifaa vingine vya kileo kabisa, Azam televisheni itatangaza mfulilizo na moja kwa moja matukio yote muhimu ya wakati huo wa kupiga kura, kuhesabiwa kwa kura na hatimae kutangazwa washindi wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, Rais wa Zanzibar, Wabunge wa bunge la Muungano na Baraza la wawakilishi, Zanzibar.
Kujiamini huku kwa Azam Televisheni katika kutekeleza lengo hili kubwa kunafuatia kuajiriwa kwa kundi la watangazaji mahiri ambao kwayo ujuzi na uelewa wao pamoja na misingi ya weledi itakayozingatiwa bila ya shaka utawezesha ari hii kutekelezwa kwa kiwango cha mafanikio makubwa.
Miongoni mwa watangazaji hao ni Charles Hilary, Ivona Kamuntu, Fatuma Nyangassa, Baruani Muhuza, Hassan Mhelela, Faraja John, Raymond Nyamwihula, Jane Shirima, Phillip Cyprian, Mwanga Kirahi, na Taji Liundi.
Tuna amini ya kwamba kundi la watangazaji hawa wenye ujuzi na wengine wachache ambao watakuja hivi karibuni wakiungana na wale vijana wasomi ambao tayari wamekuwepo wataweza kufanikisha ile ari ya kukifanya kituo cha Azam Televisheni kuwa bora zaidi katika kanda hii.
Mbali na kuimarishwa kwa kitengo cha habari lakini mipangp na mikakati bora imeandaliwa ya kupata vipindi vingine bora vya aina mbalimbali ambavyo vitatayarishwa kwa kiwango cha juu na cha hadhi ya kimataifa ikiwa ni pamoja na kuimarishwa kwa kiasi kikubwa kwa matangazo ya vipindi vya michezo na matangazo ya moja kwa moja ya mpira wa miguu ikiwa ni pamoja na yale ya ya ligi kuu ya kandanda Tanzania yaani Vodacom Premier League.
Kwa kuwapatia watazamaji wetu na watanzania kwa ujumla matangazo haya bora ya vipindi vizuri vya televisheni, tunauhakika wanunuzi wa ving’amuzi vya Azam watakuwa wanapata wakitakacho na zaidi.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog