Sunday, October 11, 2015


KOCHA Mkuu wa Tanzania, Charles Boniface Mkwasa amechagua kumuanzisha kinda Farid Malik Mussa badala ya mkongwe Mrisho Khalfan Ngassa katika mchezo wa leo dhidi ya Malawi.
Taifa Stars inamenyana Malawi kuanzia Saa 8:00 mchana Uwanja wa Kamuzu katika mchezo wa marudiano hatua ya kwanza ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 Urusi.
Na Mkwasa ‘Master’ ameanzisha viungo watatu, mmoja zaidi kutoka mchezo wa kwanza Dar es Salaam ambao alishinda 2-0 Jumatano.
Himid Mao Mkami na Said Hamisi Ndemla walianza peke yake Dar es Salaam na leo katika kuiongezea uimara safu hiyo ambayo Wamalawi waliitawala mchezo wa kwanza, ameongezeka Mudathir Yahya Abbas.
Kwa ujumla kikosi cha Stars kitakuwa sawa na kile kilichoanza katika ushindi wa 2-0 Dar es Salaam, kasoro Ngassa tu amempisha Mudathir.
Langoni kama kawaida, ‘TZ One’ Ally Mustafa Mtinge ‘Barthez’ atalindwa na Shomary Salum Kapombe kulia, Mwinyi Hajji Mngwali kushoto, Kelvin Patrick Yondan na Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’ katikati.  
Viungo Himid Mao Mkami, Said Hamisi Ndemla na Mudathir Yahya Abbas, wakati washambuliaji ni Farid Malik Mussa, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu.
Ulimwengu na Farid watakuwa wanacheza pembeni zaidi, wakati Samatta atacheza mbele ya lango la wapinzani.
Leo kutakuwa na mechi tatu za marudiano na nyingine 10 Jumanne na washindi wa jumla wataungana na timu nyingine 27 kwa mechi za mwisho za mchujo Novemba na Tanzania ikiitoa Malawi itamenyana na Algeria.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog